Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kuweza kuandaa bajeti na kusimamia Wizara kiujumla. Kwa sababu dakika ni tano, naomba kwa ufupi tu nisemee kwanza suala la wachimbaji wadogo wa madini ambao wapo katika Jimbo langu la Nsimbo, Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya kuna watu wanaopewa leseni ambazo ni ndogo (Primary Mining License), wamekuwa wakishirikiana vizuri na wananchi katika uchimbaji wa madini, lakini pale inapotokea mtu anapopanda daraja anaenda leseni kubwa, (Mining License - ML) anakuwa sasa na masharti magumu ya kushirikiana na wananchi katika uchimbaji wa madini. Hii imepelekea kuwa na mgogoro mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mfano mzuri, mwaka huu imetokea Kampuni ya Sambaru, imeweza kuingia kwenye mgogoro na wananchi wa Kijiji cha Ibindi mpaka ikahatarisha amani. Sasa ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri; tuna takriban vijiji 10 ambavyo wananchi hawa ndipo wanapata kipato. Tunaomba maeneo haya yawe ni kwa ajili ya wachimbaji wadogo tu na tusiweke uchimbaji mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunasema hivi? Maeneo haya yapo kilometa 15 mpaka 20 kutokea mjini na ndiko ambako inapatikana dhahabu.
Watu wanachimba na uchimbaji wao mdogo mdogo na wanaweza kukidhi maisha yao ya kila siku; kulipa ada na vitu mbalimbali katika maisha. Sasa tukiwekea namna hii, itakuwa inapelekea mgogoro na kuhatarisha amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika mlolongo mzima wa kazi za Wizara, tumewahi kupata taarifa, kuna ule ufadhili wa World Bank kwenye kusaidia wachimbaji wadogo wadogo tu, ufadhili takriban Dola milioni nne. Sasa katika vile vituo saba vya mfano, namwomba Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo, maeneo ya Jimbo la Nsimbo yawe ni moja ya Kituo cha mfano katika hivyo vituo saba ambavyo vitapata msaada wa Benki ya Dunia katika huo ufadhili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wachimbaji wadogo wana malalamiko kuhusiana na gharama za upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Gharama kwa hekta moja ni takriban sh. 1,500,000/= kwa mtu ambaye ameingia kufanya machimbo maeneo ya hifadhi ya misitu. Wakati huo huo, kwa hekta moja kwa upande wa madini, analipia sh. 80,000/=. Sasa imekuwa inawawia ngumu kuweza kukidhi hizi gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Wizara hizi mbili zikae kwa pamoja ziweze kuona namna gani hizi gharama zinapunguzwa ziendane na uhalisia wa uharibifu unaotokana na uchimbaji. Ni mara kumi zaidi watu wachajiwe kulingana na miti ambayo imeharibika kuliko kuchukua tu eneo wakati watu wengine wanachimba hata miti mingi anakuwa hajaikata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vile vile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa awamu ya II ya REA. Nashukuru Jimbo langu Kata nne zimeweza kupata umeme, lakini bado Kata nane. Kwa hiyo, naomba katika hii Awamu ya Tatu, ule upembuzi yakinifu ambao tayari umeshafanyika, wasiruke vijiji. Maana kuna vijiji vingine wamepitisha umeme lakini hawakuweka zile transformer na wenyewe waweze kufaidika na umeme huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.