Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, niweze kusimama kwenye Bunge lako Tukufu na kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kwimba kwa kunipa ushirikiano mkubwa ili niweze kutimiza wajibu wangu wa kuwaletea maendeleo. Pia niwapongeze wananchi kwa michango mingi wanayotoa kwenye miradi mbalimbali na nisiwasahau Waheshimiwa Madiwani kwa kunipa ushirikiano mzuri niweze kutimiza wajibu wangu, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea miradi mingi ya maendeleo ndani ya Jimbo la Kwimba. Nikianza kutaja moja baada ya nyingine ni miradi mingi sana naomba niseme machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la sekta ya elimu. Ndani ya awamu hii tumeweza kujenga Shule za Msingi tatu. Shule ya Lunene, Mwaluleho na Mwamaya pia Shule za Msingi mpya tatu zimejengwa. Pia, Shule za Sekondari tatu zimejengwa za Hungumalwa, Kilabhoya na Mpamwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye suala la afya tumeweza kujenga Hospitali ya Wilaya mpya, tumepata ambulance mpya, vituo vya afya viwili vimejengwa vya Hungumalwa na Kikubiji. Hungumalwa imeshaanza kutoa huduma pia pale tumeletewa ambulance nyingine. Kikubiji pia inaanza kutoa huduma mwezi ujao. Pia, tumejenga zahanati mbili ambazo ni Mang’ombe na Sangu na zahanati zote zimeanza kutoa huduma. Kwa kweli kwenye afya tumepiga hatua kubwa namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa msaada mzuri na miradi mingi aliyotuletea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kwenye suala la maji. Kwenye maji tuna changamoto. Sisi Wilaya na Jimbo la Kwimba tuna mtandao wa bomba, tunategemea maji kutoka KASHWASA. KASHWASA ndiyo wanazalisha maji Ihelele Wilaya ya Misungwi, wanatuingizia maji kwenye tank letu ya Mhalo. Kutoka Mhalo maji yanasambazwa mpaka kwenda Ngudu Mjini. Tumejenga matenki mawili ya lita milioni mbili Ngudu Mjini. Changamoto tuliyonayo sasa hivi ni kwamba KASHWASA hawatuletei maji ya kutosha, tumeanza kuwa na mgao wa maji. Wanatuletea maji tunapata mara moja kwa wiki maana yake Mji wa Ngudu watu wanapata maji mara moja kwa wiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mateso makubwa sana wananchi wanapata kwenye huduma ya maji. Wanasema KASHWASA kwa sababu wanapanua wanakwenda mpaka Singida sijui Tabora lakini huku nyuma wanatuacha, wanasema sisi ni wateja wadogo maana yake hawaoni umuhimu wetu sisi. Ningeomba Wizara ya Maji ifuatilie KASHWASA, huduma zao zimeharibika sana. Sasa hivi sisi hatupati maji ya kutosha, mahitaji yetu ni makubwa hawatupatii, wanatupatia mgao. Kwa nini watupatie mgao wakati miundombinu ipo na maji yapo, kwa nini wanashindwa kutusukumia maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba suala la maji liingiliwe na Wizara ya Maji wafuatilie KASHWASA kwa nini maji imekuwa ni mgao kwa wananchi wa Ngudu? Tumepata mgao ni mkubwa sana wananchi wanateseka. Tuna hospitali mpya ukija utawahurumia wagonjwa pale, hakuna maji kwenye vyoo, wanenda na madumu, wanajisaidia nje. Kwa kweli hali yetu siyo nzuri, hospitali mpya lakini imechakaa kwa sababu hakuna maji. Kwa kweli, maji ni tatizo kubwa naomba waweze kutusaidia angalau maji yapatikane kwenye Wilaya yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la barabara. Kwenye suala la barabara niwapongeze TARURA wakati wa mvua za El Nino TARURA kwa kweli wamefanya kazi nzuri, wameweza kuboresha miundombinu iliyoharibika, wameendelea kukarabati na tunaenda vizuri. Tukifika TANROADS tuna maombi ya barabara ya lami kutoka Hungumalwa – Ngudu – Bukwimba – Magu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni awamu yangu ya tatu. Miaka 10 mimi naongelea hili suala. Miaka 10 naongelea suala la barabara ya lami wananiambia tumeweka kwenye utaratibu, tukipata fedha tutaanza. Sasa lini watapata fedha miaka 10 nipo hapa naongelea hili suala moja? Hata jana nashukuru Mbunge mwenzangu wa Sumve wa Wilaya yetu ameongelea hili suala ni tatizo. Tumeiomba hii barabara kwa miaka mingi sana tatizo ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tena nitaongelea hili suala limekuwa ni kama kero. Miaka mitatu iliyopita tukaambiwa wanajenga kilomita 10. Mwaka mzima umepiata hakuna kilichojenjwa, tena wakasema kilomita 10. Tumekaa kwenye Road Board ya Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Mwanza umeielekeza TANROADS kwamba, nendeni mkaanze kujenga hii ndiyo priority ya Mkoa wa Mwanza. Meneja TANROADS wa Mkoa wa Mwanza akachukua taarifa hiyo akasema anakwenda kuifanyia kazi, mpaka leo hakuna majibu, zaidi ya RC wanne wameshabadilika maagizo ni yaleyale, sitasema Mawaziri wangapi wamebadilika lakini maagizo ni haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili iliyopita Makamu wa Rais alifanya ziara Wilaya ya Kwimba, tulizungumza nae pale Hungumalwa akaagiza kwamba, TANROADS mwambieni Waziri mwenye dhamana aje hapa Kwimba aangalie tatizo la barabara hii. Mtu wa TANROADS akasema hadharani ndiyo Mkuu nimesikia. Mpaka leo sijamuona Waziri kuja kututembelea kujibu hoja ya Makamu wa Rais, maana yake ni dharau! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala kwa kweli limekuwa ni kero kwa wananchi wetu wa Kwimba, tunaomba mara hii Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo na wao wanasema hawana fedha. Sasa yeye atujibu hata mwenyewe alishaahidi huko nyuma kwamba, kuna fedha ya mradi fulani inafika tutapeleka fedha kwenye mradi huu tunaanza, tunasubiri majibu yake leo. Waziri wa Ujenzi na yeye yupo anatusikiliza hapa Mheshimiwa Bashungwa tunakutegemea utusaidie, utukomboe kwenye suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine tuna barabara ya kutoka Ngudu – Jojiro – Mabuki ni kilomita 21 barabara inayounganisha Wilaya kwenda kwenye Makao Makuu. Ni Wilaya peke yake ambayo haijaunganishwa na lami. Nawashukuru wameanza kilomita tatu angalau mkandarasi yupo barabarani anaanza kujenga lakini tunaomba ipo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hiyo barabara inatakiwa ikamilike. Tuna miaka miwili tunaenda mwaka wa 2025 kwenye uchaguzi, tunasemaje kuhusu utekelzaji wa hiyo ahadi tuliyoitoa kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kuzungumza ni kwamba kwenye Mfuko wa Jimbo tumeletewa fedha kutoka Februari, tumegawa fedha hazijafika kwenye benki. Wale Watendaji wa Vijiji wanaenda benki wana-bounce, wanarudi wanasema Mbunge hakuna fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwezi wa Saba hapa tunanza kwenda Majimboni, tunaendaje huko? Hizo fedha tulishazigawa na hazijafika huko, tunategemea tutapata maswali tutajibu nini? Tunaomba angalau Mheshimiwa Waziri wa Fedha hizi fedha zimefika wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ningependa kuongea la ujumla ni kwamba niwapongeze Serikali kwa mradi wa mwendokasi Dar es Salaam ni mradi ambao ni mzuri sana wanaujenga kwa fedha nyingi sana, milioni ya dola wanazitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kushauri Serikali, hamuwezi mkajenga mradi mkauendesha wenyewe, hizo barabara mmezijenga mimi, ningewashauri watangaze tenda, watanzania ambao wana uwezo wa kuleta mabasi 50 na kuendelea makubwa yanayofanana na ya mwendokasi, mtu awekeze mabasi 50 mapya na kuendelea aje atumie barabara zenu aweke barabara private. Mtu akitaka kupanda basi zake atapanda ata-charge pesa yake, ili mradi huduma ipatikane. Tumeweka miundombinu Dar es Salaam yote imechafuka kwa sababu ya mwendokasi lakini hakuna mabasi. Barabara zipo tupu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeshauri sana Serikali isitegemee kununua mabasi itoe kibali wafanyabiashara wa Tanzania wapo, wanunue mabasi 50 na kuendelea, watumie zile barabara kutoa huduma. Sisi tunachotaka ni huduma ipatikane kwa wananchi wa Dar es Salaam, sasa hivi mnajenga barabara lakini hakuna huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina machache hayo ya kusema nashukuru sana, naunga hoja. Ahsante sana. (Makofi)