Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ili na mimi niweze kuchangia kwenye hii Hotuba ya Wizara ya Mipango pamoja na Wizara ya Fedha. Awali ya yote ninachukua nafasi hii, kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi yake nzuri ambayo ameendelea kuifanya na ninyi mkiwa kama wasaidizi wake katika kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mchango wangu kwa leo utagusa pande zote mbili na ningependa nianze na Mheshimiwa Prof. Mkumbo, Waziri wa Mipango. Kwetu sisi, kama Wabunge, maadamu kazi yetu ni kushauri mimi ninapenda nishauri kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kwenye upande wa nishati tunayo ambayo tunatumia kwenye upande wa kuzalisha umeme, tunatumia gesi lakini vilevile tunatumia maji. Sasa kwenye upande wa maji maana yake ukichukua Bwawa la Julius Nyerere, ukachukua Mtera, ukachukua Kihansi na vyanzo vingine vyote vya maji naamini kwamba kabla ya kufika mwisho wa mwaka huu tutakuwa tunazalisha Megawatt zisizopungua 2,500 kwenye upande wa maji peke yake lakini mahitaji yetu au matumizi yetu mpaka kufika mwisho wa mwaka huu tutakuwa tunaelekea labda sana sana Megawatt 2,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa maneno mengine Mheshimiwa Waziri, ni kwamba upande wa gesi ni kwamba tunaweza kuiondoa kwenye upande wa uzalishaji wa umeme kwa sababu uki-compare katika hivyo vyanzo viwili maji ni nafuu zaidi kuliko gesi. Kama hivyo ndivyo sasa hii gesi hebu tuitafutie mahali ambapo tutaona inaweza ikatusaidia. Leo Mheshimiwa Waziri, ukiangalia pale Dar es Salaam, Mtwara na Lindi tunayo chance nzuri ya kutumia gesi kama power ya kuendeshea magari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivyo ndivyo kazi yetu kubwa ambayo tulipaswa kufanya sasa hivi ni kuwahamasisha wananchi wa hiyo mikoa mitatu kwa kuhakikisha kwamba kwanza tunawawekea vivutio vya kuwafanya waweze ku-convert magari yao yaweze kutumia gesi. Hiyo ni pamoja na kuondoa ushuru wote ambao unatumika kwenye ile conversion ya gas to power.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo watu wengi zaidi watatumia gesi na kwa sababu tunayo maji ya kutosha basi tunaweza kupata, magari ya hiyo mikoa mitatu yapo tayari sasa wengi zaidi wanaweza kuingia kwa kutumia gesi. Kwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba kwanza itatusaidia sasa kupunguza matumizi ya mafuta ya diesel pamoja na petrol. Kama tutapunguza mafuta ya diesel na petrol maana yake ni kwamba badala ya kutumia fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya importation ya diesel na petrol tutakuwa na gesi ambayo tunatumia fedha za kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya muda sasa leo maana ni kwamba nasema hilo kwa sababu Mheshimiwa Waziri, umesema leo unashauri kuongeza ushuru kwenye gesi wakati gesi yenyewe ambayo tunaongeza ushuru tunategemea ni gesi ambayo ni vituo vitatu peke yake ndiyo vilivyopo; kile cha Ubungo, kile cha Airport na pale TAZARA. Sasa leo vituo vitatu tunavitungia sheria ya kusema kwamba tuweze kuvi-charge matokeo yake ni kwamba hata wale ambao tungewavutia wengi wakaingia humo baadaye mwaka kesho sasa tukaanza kuwatoza tukapata fedha za kutosha matokeo yake ni kwamba hawatafanya ile conversion kwa sababu gari moja dogo siyo chini ya shilingi milioni mbili kuli-convert.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtu anajaribu ku-weigh aangalie gharama za ku-convert halafu wakati huo diesel pamoja na gesi vinalingana matokeo yake ni kwamba hawataenda huko wataendelea kubaki kwenye diesel na petrol halafu tutaendelea kuwakosa na huku maji tunayo na tuna umeme wa kutosha na gesi ipo. Kwa hiyo matokeo yake ni kwamba tutaendelea kutumia fedha za kigeni kwa ajili ya importation ya diesel na mafuta ya petrol. Kwa hiyo huo ni ushauri wangu kwenye upande huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande mwingine hili ni kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Wote tunatambua kwa nchi kama zetu hizi changa tatizo kubwa tulilonalo ni tatizo la ajira, kwa hiyo watu wetu wanahitaji wapate ajira zaidi. Leo ukizungumza ajira, tutapata ajira kwenye upande wa kilimo lakini tutapata ajira kwenye upande wa viwanda. Kwa hiyo lazima bajeti yetu ielekezwe upande huo tuone namna gani kilimo kinaweza kikachochea katika watu wetu kupata ajira lakini vilevile pamoja na viwanda ili tuweze kupata hizi fedha za kigeni na tuache kuwa wategemezi zaidi kwa kila wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivyo ndivyo, ndiyo maana leo tunashukuru kwamba tunavyo viwanda vingi kama viwanda vya cement. Leo tumefika mahali mpaka viwanda vya sukari na vyenyewe vimekuwa vingi. Jana Mheshimiwa Waziri, niliweza kugusia kidogo kwamba leo tunapozungumza kwa mfano mimi nakumbuka siku moja tulikaa na watu wa CTI wakaweza kusema, mwaka juzi kulikuwa na upungufu wa sukari kwa tani 30,000. Mwaka jana upungufu uliyojitokeza ulitokana na El Nino, mwaka huu kwa mujibu wao CTI wanasema wanatarajia kuwa na tani zisizopungua 520,000 mpaka 550,000. Mahitaji yetu ni 480,000 mpaka 500,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivyo ndivyo kumbe sasa hata hivi viwanda vyetu navyo sasa vimefika mahali ambavyo tunajitosheleza kwa sukari lakini vilevile tunaelekea sasa ku-export ili tupate fedha za kigeni. Kama hivyo ndivyo sasa ushauri wangu kwa hapo nini kifanyike, maana ulileta hapa Muswada wa NFRA kuweza kuagiza sukari. Mimi nikasema hivi, badala ya NFRA kuagiza sukari wao tuwape tu kazi moja. Kwanza, Mheshimiwa Waziri, tukienda kwenye hali halisi kazi tu ya kununua mazao ya wakulima mashambani yale mahindi imewashinda.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunafika mahali tunasema hebu tuwaongezee na kazi yaku-import ambapo tusipoangalia ni kwamba hata hivyo viwanda tulivyonavyo tutaendelea kuviua na ushahidi Mheshimiwa Waziri upo wazi kwamba kwa mwaka huu peke yake tulisema kwamba gap sugar ni kati ya tani 60,000 mpaka 100,000 lakini tumetoa vibali vya tani 410,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukisema kwamba NFRA tuendelee kuwapa kazi hiyo matokeo yake hata hivi viwanda ambavyo tulipaswa kuvilinda tutashindwa kuvilinda. Tukishindwa kuvilinda na vikafa maana yake ajira kwa wale watu wetu tumeua lakini hata fedha za kigeni ambazo tulikuwa tunazinusuru basi tena tutaanza kurudi kule kule kwenye ile habari ya ulanguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilichokuwa nakiomba au naishauri Serikali kwamba kama tunadhani wale watu wenye viwanda wana tatizo la cartel, ujanja wa kufanya ni mmoja tu na kama tunadhani NFRA wanao uwezo wa ku-import sukari, wale wenye viwanda wafanye kazi moja; wazalishe na ile sukari yote wanunue NFRA na NFRA wasimamie namna yaku-distribute. Kwa kufanya hivyo hata kama kuna gap linabaki, lile gap lililopungua basi NFRA waweze kupata nafasi yaku-import. Tofauti na hapo mimi naamini kuna siku moja mtakuja kuniambia baada ya viwanda vyetu kuwa vimekufa tunarudi kule kule tulipotoka. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nadhani hilo nilidhani niweze kulishauri kama tutaona ni jema basi tunaweza kulifuata na...

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo tunadhani kwamba tutakuwa tumeendelea kulinda viwanda vyetu na hata viwanda vingine. Hii ndiyo itakayotufikisha mahali tukapunguza tatizo la ajira kwa ajili ya watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni hivi viwanda vyetu vya SIDO. Viwanda vya SIDO...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Manyinyi, kengele ya pili hiyo.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)