Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Bajeti Kuu. Mimi naanza kumnukuu Mheshimiwa Rais alipokuwa akipokea gawio, ya kutoridhishwa na mwenendo wa ufanisi wa mifuko ya hifadhi ya jamii. Vilevile, akasema makosa ya wengine na akasema ikiwepo na Serikali tusiwaonee watumishi wa umma. Pia, amezungumzia uwekezaji usio na tija kwenye maeneo mbalimbali kupitia fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii. Nashukuru mwenyewe ameliona, wengine tuliongea humu zaidi ya miaka sita hatukusikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Kamati ya Bajeti kupitia ukurasa wake wa 87 wamezungumzia uwekezaji usio na tija na kuathiri mifuko. Hii ndiyo inasababisha leo watumishi wa nchi hii wanapunguziwa mafao yao kwa mkupuo. Tuliongea hapa tangu 2018 mnaleta sheria si kwa ajili ya kulinda mifuko, mnaleta sheria baada ya kujua mifuko ipo hohehahe na mnataka kuwadhulumu watumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 101 unasema eti umerudisha kikokotoo 40% yaani kama zawadi 40%. Watu waliokuwa wakichukua mafao kwa mkupuo kwa 50% na walikuwa wakiendelea kulipwa pensheni za kila mwezi kwa miaka 15, nyinyi vyote hivyo mmepunguza halafu mnasema eti lengo ni kuwasaidia watumishi wa umma wa nchi hii kwa pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuangalie kiini, kiini mmeenda kuwekeza kwenye miradi isiyolipa na miradi ile inatengeneza hasara. Mimi nilitegemea mtasema mtaenda kulipa fidia kwenye zile pesa ambazo watu wameenda kuwekeza muweke kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Nilitegemea mtasema Serikali mnadaiwa zaidi ya shilingi trilioni mbili sasa hivi zile za P1999 muwalipe ili waweze kufanya kazi zao vizuri na wataweza hata kujipangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaweza kuwalipa zaidi hata ya 60% kama ambavyo wanafanya wengine. Halafu leo eti mnarudi mnasema 40% yaani kana kwamba mmefanya jambo kubwa. Leo mngekuwa ile mifuko ipo stable msingechukua pesa kwenda kuwekeza kiholela, leo ile mifuko ilikuwa ina uwezo wa kumlipa mtumishi hata 60% mafao kwa mkupuo na ilikuwa ina uwezo wa kumlipa kwa kila mwezi mfululizo hata miaka 18.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya umekuja umesema mnasimamisha eti mtalipa mpaka 2030, sasa 2029 mnalipa ninyi kama nani? Tumetunga Sheria 2018 imetaja wazi mwenye mamlaka ya kulipa wastaafu ni Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Ukienda kwenye Sheria ya mwaka 2018 kwa upande PSSSF Sheria Kifungu cha 6(3) kinaeleza mamlaka ya kulipa wanayo Mifuko. Ukienda NSSF kwenye Sheria ya mwaka 2018 Kifungu cha 3(2) kinaeleza wenye mamlaka ya kulipa mafao ni wastaafu yaani mnataka mvunje sheria kuficha makosa yenu! Solution siyo kuvunja sheria, solution ni kushughulika na kiini cha kuenda kulipa madeni, kushughulika na kiini kwenda kulipa fidia kwenye maeneo ambayo mmewekeza miradi isiyolipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu unasema eti unaleta 40% unalipa kwa formula ipi? ya 1 ya 580? Wenyewe hawataki, wanataka irudi formula ya 1 ya 540 kama ilivyo mwanzo. Hapa hakuna mnachomsaidia mtumishi hapa na wamenuna na wanasema achene kuwatisha Wawakilishi wao, haya mambo mnakaa wenyewe mnajifungia mnaamua bila kuwashirikisha, ndiyo maana leo mnaenda kuchukua mamlaka siyo yenu. Hizi pesa mnazosema mnalipa pelekeni wenyewe kwenye Mifuko walipe, walipeni madeni fanyeni Mifuko iwe stable ili siku moja watumishi wa nchi hii wanaoifanyia kazi kwa jasho na damu waamue leo tunachukua mafao yetu kwa mkupuo asilimia 70, inashindikana nini kama Mifuko ipo imara? Hilo nalisisitiza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nilikuwa nataka kuzungumzia hebu mkija kujibu hapa mtuambie hebu vipi hukusu mortgage? Maana mliiwekea kwenye Sheria, Kifungu cha Sheria Kifungu Namba 42 cha Sheria ya 2018 maana ile ilikuwa danganya toto. Wakati mnawa-lobby wakubali na asilimia 33 inatekelezeka? Maana najua Kanuni tayari za mwaka 2024, GN. tayari imeshatoka namba 140 tangu tarehe 8 Machi, 2024 kiko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mliwaambia tutawapa asilimia 33 halafu mtakuwa mna uwezo wa kwenda kukopa kupitia pesheni zenu muweze kujenga nyumba ili hata mkipata kidogo muwe na uafueni mna maeneo ya kuishi. Hizi hela zingine mtazitumia kuandaa Maisha! Leo hakuna mtu pale anaye ruhusiwa kwenda kukopa. Kwanza, watakopa lakini vilevile riba, haya mtu ambaye anapata milioni 17 anaenda kukopa nusu ya hapo atajenga nyumba? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani hawa Wafanyakazi siyo watoto wadogo, wana familia ni kwamba tu hawawezi kuandamana wanaandamana kwenye mioyo. Tunapitisha trilioni 49 hapa halafu mnategemea waende kuzisimamia watu ambao wana manung’uniko, watu wanaodhulumiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa tukitoza tozo kwenye mafuta ya petroli na gesi ili ziende kwenye Mfuko wa Maji, Mfuko wa Nishati Vijijini, Mfuko wa Barabara. Kwa miaka mitatu mfululizo pesa hizi hazijaenda na hizi ni pesa mahsusi za kazi mahsusi zipo kwenye ring fence kisheria, kutopeleka pesa hizi ni kuvunja Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi kwenye Mfuko wa Maji, hazijaenda bilioni 285, nishati vijijini hazijaenda bilioni 267, Mfuko wa Barabara hazijaenda bilioni 598, fedha ambazo hajizaenda kwa miaka mitatu mfululizo trilioni moja na bilioni mia tatu arobaini na saba. Sasa mnategemea barabara vijijini zitapitika? Mnategemea miradi ya maji kwenye Majimbo yetu itakamilika? Mnategemea miradi ya umeme itakamilika miaka mitatu mfululizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria inavunjwa, pesa zipo kwenye uzio hazipaswi kutumika kwa matumizi mengine yoyote, yoyote yale. Tunatoza tozo kwenye mafuta na gesi mafuta ya petroli na diesel ili watu waende wakaone maendeleo kwenye haya maeneo ninayoyasema. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulaya, kuna taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilipanga nimjibu wakati wa kuhitimisha ile hoja ya kwanza ya mafao ataona matamko ya wapokeaji wenyewe, lakini taarifa tulizonazo ni kwamba wamefurahishwa sana na hatua ya Serikali iliyofanya. Nilichosimama kutaka kumpa taarifa anasema fedha hazijaenda, hili ni jambo limenishtua fedha hazijaenda wapi? Fedha za Mifuko zipo kwenye Mifuko hazijaenda wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za mifuko zipo kwenye mifuko na zinatumika kufuatana na mahitaji, Mheshimiwa Mbunge asichanganye fedha zinazotumika kwenye maintenance na fedha zinazotumika kwenye barabara mpya. Kwa hiyo, fedha za Mifuko zipo kwenye Mifuko. (Makofi)