Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii nzuri ya kuchangia kwenye bajeti kuu ya Serikali na Mpango wa bajeti kwa mwaka huu. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa sababu ya kutupatia fursa hii ya kujadili bajeti kwa ajili ya watanzania takribani milioni 61 kwa ajili ya mwaka huu unaofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwapongeza Mawaziri wote wawili, nawapongeza vilevile wataalam na Makatibu Wakuu wote na Katibu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Mipango kuendelea kufanya kazi nzuri ambayo tuliitarajia kuiona wakati tunapoenda kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha unaokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninasoma taarifa hii ukurasa namba 11 ukanionesha wazi kwamba, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika mradi mkubwa wa SGR lot one imekamilika, SGR hiyo imetekelezwa kwa lot one mpaka asilimia 83.55. Lot two imekwenda asilimia 57.57 lakini ilikutwa kwenye asilimia hizo na sasa imekamilika. Kwa hiyo, ninachokiona hapa ni kwamba, lile neno Kazi Inaendelea linaonekana kwenye bajeti hizi, kwa sababu pale lot one ilipokutwa sasa imekamilika inaweza kuanza kutumika lakini lot two ilipokutwa imekamilika inaweza kuanza kutumika. Maana yake nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa matokeo mazuri ya kwanza hayo ya SGR lot one na lot two. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo lot nyingine zinazofuata ambazo nazo zinakwenda kwenye utekelezaji, kila moja ipo katika kiwango chake tofauti tofauti mpaka lot saba. Kuna uboreshaji wa bandari kina kufikia mita 15.5 na upana wa mita 200 ambayo kazi hii nayo inatarajiwa kuendelea ili meli zetu kubwa ziweze kutua katika bandari hiyo ya Dar es Salaam ambayo tunatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile bandari yetu kavu ya Kwala imefikia sasa takribani asilimia 96 hii yote ni kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ninayasema haya ili ninapo mpongeza isionekane ninampongeza tu kwenye plain surface. Nampongeza kwa sababu ya vile ambavyo vimetokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Msalato kwenye miundombinu umefika takribani asilimia 56.9 lakini kwenye upande wa majengo sasa tumefikia asilimia 22. 56, maana yake kuna kazi inaendelea hapa, inawezekana tunaishi Dodoma lakini hatujaenda Msalato kuona kinachoendelea hiyo yote ni kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya ujenzi tumeona kazi kubwa zinaendelea kwenye ujenzi wa barabara na maeneo mengine ambayo nisingeweza kuyataja yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii ukiangalia kwenye bajeti iliyopita ukiangalia kwenye sekta ya nishati utagundua wazi kwamba, Bwawa la Nyerere lilipochukuliwa mara ya kwanza Mheshimiwa Rais anaingia madarakani lilikuwa asilimia 37 na sasa limefika asilimia 97.43 na tayari tumeshafanya majaribio na Megawati 235 zinafanya kazi kwenye mtambo namba tisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu na ushauri kwa Serikali hapa ni kufanya ile mitambo mingine kuanzia mtambo namba moja mpaka nane iingizwe sasa ili tuweze kupata hizi megawati 2,115 zote na hizo interface substations iliyopo Lemugul kule Arusha na nyingine zinayojengwa huku kwenye Southern Regions ziweze kufanya kazi ili tuuze umeme au tu-import umeme kutoka kwa wenzetu tunapokuwa na matatizo ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, REA nimeona wazi kwamba, kuna takribani vijiji 11,973 vimeunganishwa ambavyo ni takribani asilimia 97 tumeshaviingiza, nchini hii imeshakuwa na umeme kwa kiwango hicho. Vitongoji takribani 32,827 kati ya Vitongoji 64,359 vimepata umeme, hapa vilevile nitoe ushauri kwa sababu karibu asilimia 50 ya vitongoji havijapata umeme tuendelee kujikita kuona tunapata wapi fedha kuhakikisha kwamba, vitongoji vyote vinapata umeme kwa sababu umeme sasa siyo anasa tena kila Mtanzania ana uhitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maji nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kule tu Jimboni Busanda kuna mradi wa takribani bilioni 6.2 umefikisha maji kutoa Njia ya Korongo kuja pale Mji Mdogo wa Katoro, matarajio ya maji kupatikana yalikuwa ni changamoto lakini maji yamefika na sasa yanaanza kutumika tupo kwenye ugawaji sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna miradi mingine mbalimbali Jimboni kwangu ambayo inaendelea kuwepo kusambaza maji Nyarugusu takribani milioni 700 imekwenda pale kufanya hiyo kazi na maeneo mengine mengi. Yote haya nimeyasema kwa sababu nataka tuoneshe kwamba yapo mambo makubwa yanafanyika kwa bajeti zilizopita na bajeti ya mwaka jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye elimu, nilisikia Mbunge mmoja nasema hapa wiki iliyopita tulipigiwa simu kuhakikishiwa wazi kwamba sasa fedha imekwenda kwa ajili ya ujengaji wa sekondari za SEQUIP. Mimi nimepigiwa simu nikaambiwa sekondari mpya inatakiwa kujengwa kwenye Kata ya Nyamigota kwenye Kijiji cha Chibingo na pesa ina kwenda wiki hii. Kwa hiyo, ninaamini kesho ni Ijumaa lakini ninaamini kazi huko itakuwa imeanza, hii yote ni kazi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuende kwenye bajeti hii ambayo sasa tunaenda kushughulika nayo ambayo imetuonesha vipaumbele kadhaa. Ukiangalia maeneo ya mpango yana hoja gani? Yanasema yanataka kuchochea uchumi shindani na shirikishi. Hapa hoja kubwa ni kwamba, lazima wananchi wengi washirikishwe kwenye uchumi wa nchi hii na hapa ndipo tunaenda kuwaona wakulima wengi ambao hawajashiriki kwenye kilimo hawachangii pato la nchi hii, matokeo yake mapato yetu yanakuwa kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo, ina nafasi kubwa ya kufanya mchango huu uwe mkubwa kwamba, wale wananchi ambao ni asilimia 66 wakiwezeshwa kupitia skimu za umwagiliaji hii kazi inawezekana kuona tuna mchango mkubwa na mapato yakaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya sana ni kwamba, kwenye maeneo kwa mfano ninayotoka mimi bado hata upembuzi yakinifu uliosema mwaka jana haujafanyika. Kwa hiyo, ninaamini wale wananchi wangu wanachangia kidogo sana kwenye Pato la Taifa kwenye kilimo, lakini na maeneo mengine inawezekana ikawa hivyo. Kwa hiyo, niwaombe sana Wizara ya Kilimo, wahakikishe kwamba wale watu wengi asilimia zaidi ya 66 wapate hizo skimu za umwagiliaji na wawezeshwe ili kuweza kupata mchango mkubwa wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na kwa watoa huduma kukuza bidhaa na uwekezaji na kuchochea maendeleo ya watu na kuzalisha rasilimali watu. Hapa watu wengi wamesema juu ya ajira na sipendi niparudie sana. Kazi kubwa ambayo tumeiona kwenye section 10 Ukurasa namba sita ni kukamilisha miradi ya kielelezo na miradi ya kimkakati ambayo nimekwisha isema. Kwa hiyo, ninaamini kabisa hii trilioni 49.35 inakwenda kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja tu ni kwamba tumekuwa tunasema kila wakati lakini tunapokwenda kwenye utekelezaji tunakutana na changamoto kwamba pamoja na utekelezaji mzuri unaoenda kufanyika kuna maeneo mengi yanakuwa hayakuguswa. Ukiangalia tumepata ukisoma kwenye page six section 12, utagundua imeelezwa wazi kwamba, umewekwa uwekezaji mkubwa kwenye uthibiti wa matumizi mabaya ya Serikali. Maana yake nidhamu ya fedha inaenda kuwa nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda hapo hapo ukaenda mbele utekelezaji wa bajeti iliyopita utagundua fedha iliyotoka mpaka Aprili ni asilimia 80.5 fedha ambayo haitatoka ni asilimia 19.7. Sasa hoja yangu ni nini, kuna miradi ambayo haijaanza kabisa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Magessa kengele ya pili hiyo.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)