Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba na mimi nichukuwe nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pili kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mapenzi yake mema kwa sisi wananchi wa Tanzania. Pia, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Fedha pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri za kuhakikisha tunaijenga Tanzania kwa umoja na kuhakikisha maendeleo ya Tanzania yanawafikia Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimesimama hapa, kwa nini nimeanza na shukrani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza na shukrani kwa sababu, kwanza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pesa zilizokuja katika maeneo yetu ni nyingi sana, haijawahi kutokea. Mbili, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu, ni hivi karibuni tu kule Kaliua sisi tunahifadhi misitu vizuri sana, wameweza kutupatia fedha karibu shilingi bilioni 16, fedha ya kaboni, wanasema ya ukaa. Mheshimiwa Jaffo nakushukuru sana na Wananchi wa Kaliua wanakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba fedha ambazo mmezibajeti na kuzileta Kaliua mzisimamie vizuri sana, ili manufaa yale yaweze kutokea katika Jimbo la Kaliua. Jambo la pili ambalo naishukuru Serikali ni kuhakikisha kwamba, sasa Wakulima wa Mkoa wa Tabora, Wakulima wa Kaliua, lile ombi ambalo tulikuwa tunaomba siku zote, mmeonesha usikivu mkubwa sana, ni kutupatia ruzuku ya mbolea. Ruzuku kwenye tumbaku (NPK) tulikuwa hatuna, lakini mwaka huu wakulima wa Jimbo la Kaliua, Wakulima wa Mkoa wa Tabora, tunakwenda kunufaika na mbolea za ruzuku. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Bashe hayupo, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali hii ya Awamu ya Sita, tunashukuru sana kwa jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina ombi. Mwaka jana Mwezi wa Tisa sisi Mheshimiwa Rais alituondolea vijiji ambavyo vilikuwa hifadhi, karibu vijiji kumi na sita na baada ya kuviondoa tulipata changamoto ya barabara. Tulikuja kwako na tukapata fedha ambapo Mtendaji Mkuu wa TARURA alipitisha pamoja na Waziri wa TAMISEMI. Sasa mezani kwako bado kuna ombi la shilingi bilioni tatu, ili kuhakikisha vijiji hivyo tunafungua barabara zake zote. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, fedha hizo uweze kuziruhusu, ili sisi wananchi wa Kaliua tuweze kujenga miundombinu ambayo ilikuwa ni sehemu ya hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ninamuomba Waziri wa Maliasili ni kuhusiana na vijiji vyetu viwili, Kijiji cha Usinga na Kijiji cha Ukumbi Kakoko. Walikuja Mawaziri awamu ya mwisho; awamu ya kwanza timu ya kwanza ilikuja ikaruhusu kwamba, Mheshimiwa kawaonea huruma wananchi waishi. Nataka niweke kumbukumbu vizuri kwamba, vile vijiji viwili vya Ukumbi Kakoko na Usinga vipo pale kuanzia Mwaka 1973, ni vijiji ambavyo vimesajiliwa TAMISEMI. Kwa mapendekezo ambayo mlikujanayo muelewe kwamba, ni vijiji halali na vinatawaliwa na Sheria ya Ardhi, Sheria Namba 5 ya 1999.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwamba, wale wananchi mlikuwa mnasema habari ya kifuta jasho; hakuna cha kifuta jasho pale, wananchi watakuwa wanastahili malipo halali, lakini mimi sioni kama kuna tija. Tumekuwa na tabia ya kuwaondoa wananchi bila sababu za msingi kwenye maeneo ambayo wameishi, kwenye maeneo ambayo wazazi wao na wazee wao wamezikwa. Hebu tuangalie utaratibu mzuri wa kwenda na jambo hili na ninawaomba Wizara ya Maliasili, ninamuomba Waziri wa Ardhi, tulishazungumza, jambo lile liangalieni vizuri, ili wanavijiji waendelee na kazi zao kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ninaomba ni ile miji 28 ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia ametoa fedha, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha, wanufaika wa Mradi wa Maji wa Ziwa Viktoria ni pamoja na Kaliua. Kwanza nawapongeza watu wa maji wa Tabora kwa kazi nzuri kwa sababu, ule mradi unaopeleka maji Skonge, unaopeleka maji Urambo, unaopeleka maji Kaliua upo asilimia 40, lakini ninawaomba kwa sababu, sasahivi wamemalizia tanki la lita milioni mbili. Mimi ninaomba waanze kusambaza mabomba katika Kata zote za Jimbo la Kaliua ambazo zinapitiwa na ule mradi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba ule unaisha mwakani Mwezi wa Saba. Nawaomba, kama upo uwezekano wa kumaliza mradi mkubwa kama huu mapema itakuwa ni manufaa makubwa sana kwa wananchi. Mimi nina changamoto, nimefurahishwa kwa sababu, najua Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu wetu yupo na ni makini, nadhani sasa Kaliua tunaongoza kwa kukatika katika umeme wakati mradi mkubwa wa Mwalimu Nyerere umeingiza umeme kwenye gridi ya Taifa, sisi kule bado shida ni kubwa sana. Mimi nakuomba Waziri wa Nishati, hebu fuatilia sana kuna shida gani Kaliua? Yaani umeme kwa siku unakatika zaidi ya mara 20, ni meseji kuanzia asubuhi mpaka jioni, naomba sana ulifuatilie jambo hili, ili tuelewe kuna nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natambua kuna mradi pale unau-push toka umeingia. Nakupongeza umesababisha ule Mradi wa Uhuru pale umekwenda kwa kasi sana, lakini sisi tunachohitaji ni umeme. Yaani hizi process zote wananchi hawazihitaji, wanahitaji matokeo, matokeo ni uwepo wa umeme. Watu wanahitaji kuangalia mpira, watu wanahitaji kufanya mambo mbalimbali kwenye mitandao, umeme hamna, wanahitaji mambo ya kuchomelea na mambo mengine. Nakuomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu tusaidie sana Kaliua, ili twende pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ambalo ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Rais ni, wiki hii nimepata taarifa sisi tunapelekewa fedha Kaliua, ametuongezea sekondari tatu, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sasa katika Kata ya Ushokola tunakwenda kuongeza sekondari mbili, sekondari ya kwanza inakwenda kujengwa kwenye Kijiji kinaitwa Sanja Ndugu na sekondari ya pili inakwenda kujengwa kwenye kijiji kinaitwa Ibara Upina na katika Kata ya Ingwisi sekondari inakwenda kujengwa Mahalaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anapofanya majukumu yake mazuri kama haya, Serikali yake inapofanya mambo mazuri kama haya, mimi nasimama kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Kaliua kumshukuru sana kwa mapenzi yake ya dhati. Miradi inayoendelea katika Jimbo la Kaliua ni mizuri sana, ni miradi ambayo tunaitegemea na kwa hilo tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha naendelea kusisitiza, lile dokezo lipo mezani kwako. Tafadhali sana, shilingi bilioni tatu, chondechonde kabisa na ikiwezekana hata ukituma meseji muda huu wakaanza kuitoa, ili mimi nikifika kwenye ziara zangu za Mwezi wa Saba napita tu kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine. Wilaya ya Kaliua kwa sababu ni miongoni mwa zile Wilaya zilizokuwa mpya, nakuomba Mheshimiwa Waziri, tunajenga Ofisi ya TRA, ahsante sana, lakini TRA inakwenda kwa kusuasua. Naomba ulifuatilie jambo hili, ili Ofisi ya TRA katika Jimbo la Kaliua ikamilike haraka iwezekanavyo, ili wananchi waendelee kupata huduma kwa ufanisi na kwa ubora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kumalizia na kusisitiza hapa, namuomba sana Waziri wa Ujenzi, Kaliua ni miongoni mwa Wilaya ambazo zinachangia sana mapato ya ndani katika Taifa, lakini barabara kubwa ambayo inatuathiri kwa sasa ni kutoka Mpanda – Kaliua – Kahama. Sisi tukipata korido ya barabara hii yote inayotokea Mpanda kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kapufi anayepiga makofi hapo, ikapita kwangu, ikapita kwa Mheshimiwa Rehema Ulyankulu, ikaenda Ushetu, ikaingia kwa kaka yangu Mheshimiwa Kishimba, ile korido kiuchumi sisi itakuwa imetuinua sana. Ile Kaliua ni kama hub kwa sababu, ndiyo maana kuna njiapanda hata za reli na ukiangalia hata reli tunaendelea kujenga sasahivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana narudi kusisitiza kwamba, barabara ile ni muhimu sana kiuchumi. Inawezekana msiamini, lakini ninachowaambia ni ukikuta Wilaya kama Kaliua inakuwa na wananchi karibu 768,000 hivi kweli tunajadiliana jambo kama hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wale wote wanahitaji huduma kubwa, ukiunganisha na hao tunaongelea watu zaidi ya milioni tatu. Nawaomba ndugu zangu, barabara hii tuipe msukumo wa pekee ni barabara ambayo imekuwepo kwenye Ilani ya uchanguzi kwa mihula mitatu ya nyuma yote imekuwepo pale. Kwa hiyo, nawaomba sana, pelekeni fedha, tuwekeeni wafadhili, ili barabara hii iweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naendelea kupongeza jambo moja la kuhusiana na kikokotoo, lakini Waziri wa Utumishi sio mbaya sana. Hatua mliyoifanya ya kutusikiliza ni nzuri, lakini if possible endeleeni kuangalia, kuwapa nafuu hawa watumishi. Watumishi wengi wa umma kwa sababu, mishahara, na ninajiuliza hivi kwa nini siku hizi hela haikai sana? Mnaweza mkajifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema kwamba, naunga mkono bajeti kuu. Nashukuru sana, ahsante sana. (Makofi)