Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nakushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye hii bajeti kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mimi nitajikita sana kwenye ushauri lakini awali ya yote tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai wa kuweza kukutana jioni hii. Vilevile, nipeleke shukurani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa kwa maono yake ya kutenganisha Wizara hizi mbili, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza ushauri wangu kwenye Wizara ya Mipango. Mheshimiwa Rais alipotenganisha Wizara hizi mategemeo yake makubwa aliyotaka kuyaona ni kuona bajeti zetu au bajeti hii ya kwetu inakwenda na mipango ambayo nchi yetu imejiwekea. Bajeti ambayo inakwenda kutekeleza mpango na siyo kutekeleza tu mpango, ni mpango endelevu na mpango wenye tija. Kama Taifa hatuna tatizo la kupanga mipango. Tatizo letu ni mipango yetu inatupeleka wapi, tunaimalizaje na tunaitekelezaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo shida kwenye utekelezaji wa mipango. Tumekuwa wapangaji wazuri sana na wakati mwingine ziko nchi zinakuja kukopa namna tunavyopanga mipango yetu lakini shida ni kwamba tunatekelezaje. Nitoe mfano, tunao mpango wa pale Dar es Salaam wa ujenzi wa barabara zile za BRT. Barabara ya Kimara imeisha miaka 10 sasa, kwenye mipango yetu kwa namna tulivyoipanga na tukipima leo tumefanikiwa kwa kiwango gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ukiniuliza nitakwambia tumefeli kwa sababu leo pale mabasi hayatoshi na msongamano ni ule ule. Tulitegemea kupunguza daladala, ndiyo kwanza zinaongezeka. Kwa hiyo, pale mimi naweza nikasema kwamba tumefeli. Pamoja na kufeli kule bado tunaendelea na mipango mingine, tumejenga Mbagala. Mbagala sasa hivi imeisha ina mwaka lakini hakuna basi hata moja. Pia kama haitoshi tumeenda Gongo la Mboto, ambayo kesho au kesho kutwa itaisha. Sasa ukiwauliza wanakwambia magari yako kwenye manunuzi. Tulivyokuwa tunapanga, tulikuwa hatujui kwamba mradi huu unakwenda kukamilika lini ili uendane na uletaji wa mabasi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, pale tumepanga lakini hatuku-foresee kwamba tunakwenda kufanya nini. Leo ukiniambia mimi kwamba magari ya BRT yanakuja yako kwenye manunuzi siwezi kuelewa kwa sababu mradi ule, zile fedha ziko pale. Ile barabara imeisha ina mwaka, fedha za walipa kodi ziko pale zimelala hazina kazi na tumeanza kulipa. Mategemeo yetu ni kwamba sasa zingeanza ku-generate fedha pale ili kuanza kulipa lakini tunaanza kulipa au tutakuja kulipa wakati fedha zimelala pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi huo huo nauona kwenye SGR. Leo tumeshafika Morogoro na kesho tunaingia Dodoma lakini tumejipangaje kuhusu uendeshaji wa hiyo reli na kwa nini tunafika mahali ili tuweze kutekeleza mpango ambao tumeuanza miaka miwili iliyopita, sustainability yake ni mpaka tuje tubadilishe sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kitangulie? Tubadilishe sheria au tuanze mradi? Mwaka jana tu ndio tumebadilisha Sheria ya PPP, kwamba ndiyo tumegundua kwamba kumbe hii reli kuendesha kama Serikali hatutaweza tunahitaji watu wa kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali ambayo ndiyo yenye mradi wake mpaka leo mabehewa yako kwenye manunuzi, hawa PPP ambapo jana ndio tumeweka sheria ina maana wachukue muda na wao kuomba. Waombe, waingie mikataba, wakishapata hiyo mikataba ndipo waagize mabehewa itakuwa ni miaka miwili, mitatu au minne. Reli imeisha lakini watu wako kwenye manunuzi. Ina maana kwamba tulivyopanga hatukujua kwamba kama Serikali kazi yao ni kutengeneza njia ili wawekezaji waje watumie hiyo njia lakini mpaka juzi ndio tumekuja kubadilisha sheria hapa, ndio tunakumbuka kwamba kumbe ili hii reli iweze kwenda effectively lazima tuite PPP. Ndio tumebadilisha sheria tumekwenda na PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote ni kwa sababu tunakwenda na mipango ambayo haiko sawasawa. Mimi niwashauri Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Mimi nafikiri Waheshimiwa Wabunge tubadilike kidogo, Serikali inapokuja na mipango na sisi tujiridhishe. Kitendo cha Bunge kupokea mpango wa Serikali tukaupitisha juu juu bila kujua undani wake halafu unakuja unatuletea matatizo kama haya ya kubadilisha sheria nafikiri hatutakuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima mipango hii ya Serikalini inapokuja, sisi kama Wabunge tusimame tuiangalie sustainability yake, ufanisi wake, utekelezaji wake na miundombinu yake ya utekelezaji itakwendaje lakini kama sisi tutakuwa tunapitisha tu maadamu Serikali wameleta mipango yao na sisi tukakubaliana mwendelee. Matokeo yake ndio wanakuja kesho kutwa yake tubadilishe sheria ndiyo mipango iweze kutekelezeka ndiyo mipango iweze kutekelezeka, hii haiwezi kuwa sawa, atuisaidii nchi hii. Kwanza, tunapoteza fedha za walipakodi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine ni kwenye huu Mradi wa EPC+F...

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa, Taarifa, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga, Taarifa.

TAARIFA

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuunga mkono mchangiaji, anachangia vizuri sana lakini anavyosema kwamba Waheshimiwa Wabunge tupitishe bila kujua na sisi tuko hapa ndio tunatoa mawazo yetu, si utoe mawazo kwa namna ambayo unaona Serikali iende. Ndiyo tunachotakiwa kufanya. Kaka naomba usilishushe hivyo Bunge, changia unachotaka Serikali ifanye au iboreshe katika mipango.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kuchauka, unaipokea hiyo Taarifa?

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa yake. Nilichotaka kusema ni kwamba, EPC+F ilianzia kwenye Kamati ya Miundombinu. Kabla haijafika Bungeni inaanza kwenye Kamati na hata ile mipango ya BRT ilianza kwenye Kamati vilevile Mipango ya SGR ilianza kwenye Kamati. Leo tumesaini mikataba ya SGR, tumesaini mpaka vipande sita, imepitia kwenye Kamati lakini ukiuliza behewa tunazo? Unaenda kuambiwa kwamba bado ziko kwenye manunuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niliposema Bunge kwa maana ya Kamati zetu zinapoletewa hizi taarifa tuzisimamie vizuri. Leo tunazungumza hapa Bungeni na tunashauri lakini tunaposhauri jambo hili tayari limeshaharibika. Ili ionekane Bunge linafanya kazi vizuri, tuyasimamie haya kabla hayajaingia humu ndani ili yasiharibike. Leo hili likiharibika, linaharibika mikononi mwetu. Mbagala imekaa haina kazi, hamna magari na hii Barabara ya Kimara mpaka leo haina magari, barabara hizi zinaharibu matairi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za watu ziko pale, zimeshaharibika lakini zimekuja kuharibika mwishoni. Hili jambo haliwezi kuwa sawa. Lazima tunapoletewa mipango hii na sisi tujiridhishe kwamba mipango hii kama haitekelezeki basi tuikatae. Hicho ndicho ambacho nilikuwa nataka nikiseme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa mfano wa pili hapa huu wa EPC+F tuliaminishwa wapo matajiri wanakuja kujenga hizi barabara kwa muda mfupi. Badala ya sisi kutumia miaka 20 kujenga barabara saba, hawa watatumia miaka mitatu minne barabara zimeisha lakini kinachoonekana hapa, hawa watu wenyewe wametudanganya bado hawana uwezo ndiyo maana Serikali inasema bado tunaenda kwenye majadiliano. Tunajadiliana tuwawezeshe wapate fedha waje watujengee. Ndiyo majibu yaliyopatikana hapo kwenye hotuba ya kisekta lakini je, hawa watu hawakuja kwenye Kamati na hawajajiridhisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini sisi kama Waheshimiwa Wabunge hatukuwaambia hebu mtuletee hao matajiri tuwaone; tuwahoji tuone uwezo wao. Jambo hili lisingekuwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuna mambo mengine kama ya kisera, kama kuna sera ambazo tunaona hazitekelezeki Mheshimiwa Waziri wa Mipango tuzifute. Tuna sera ya kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami. Sera hii sasa inakwenda zaidi ya miaka 25 leo, bado hatuna uwezo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mkoa wa Lindi na Morogoro haijaunganishwa, jana Mheshimiwa Mbunge mwenzangu hapa amesema Kigoma nako hakujaunganishwa. Sasa kama hivyo vitu havitekelezeki kwa nini vibaki kwenye vitabu? Kwa hiyo, tuvifute. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona tulipohitaji kwamba kila kata iwe na kituo cha afya, tukaona kwamba haiwezekani kwamba kila kata iwe na kituo cha afya. Tukasema tunakuja na vituo vya kimkakati. Kwa hiyo, tukafuta ile ya kwamba kila kata iwe na kituo cha afya na hii nayo tufute. Kwa nini ibaki kwenye makaratasi na miaka inakwenda, mikoa hii haitaki kuunganishwa. Inafika mahali watu wengine wanaona kama wametengwa... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa muda. (Makofi)