Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia bajeti hii. Mimi nianze kuipongeza Serikali yetu, Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan na watendaji wote wakuu wa Serikali hii inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan. Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri ambao hoja yao iko mbele yetu (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma mpango na ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa vipaumbele ambavyo ameviweka. Nimeangalia vitatu vya mwanzo ambavyo kimsingi ni vipaumbele vya kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele namba moja anaongelea kuchochea uchumi shindani, shirikishi na kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki kwenye uchumi wao. Nadhani kipaumbele hiki kama tutakifanya vizuri, ndiyo kipaumbele ambacho kitashirikisha Watanzania kimiliki uchumi lakini pamoja na kushiriki kwenye kumiliki uchumi hata kuongeza wigo wa walipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili wanaongelea kuimarisha uwezo wa uzalishaji na cha tatu kukuza biashara na uwekezaji. Kwenye hiki cha tatu, kwenye Jimbo langu la Muleba pale tuna wafanyabiashara ambao wanaongeza mnyororo wa biashara kwenye zao la kahawa. Tuna viwanda kama vitatu pale, naomba nivitaje, tuna Johansen Company Limited, Atadals Groups na Hakika Cofee. Naiomba Serikali iwaangalie watu ambao wamewekeza kwenye kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo. Hawa watu wanahangaika kutafuta mikopo, kuimarisha na kuboresha kilimo chetu lakini hawapati usaidizi wa haraka haraka na wa moja kwa moja hasa inapokuja kwenye suala la mikopo. Hawa ndio tunaweza kuwatarajia kesho na kesho kutwa kulipa kodi na kuzalisha na kuwafanya wawe kampuni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kutengeneza mabilionea kama Serikali haishiriki moja kwa moja katika kuwatengeneza hawa mabilionea. Serikali ina wajibu mkubwa kuwawezesha hawa wafanyabiashara na wajasiriamali kuhakikisha kwamba wanakua kutoka kwenye hatua za mwanzo na kwenda kutengeneza kampuni kubwa ambayo mwisho yatakuja kulipa kodi kubwa kwa ajili ya kuongeza Pato la Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwenye hotuba yake aliyoitoa juzi, kwenye paragraph yake ya 58 ya hotuba yake aliongelea suala la kikokotoo. Naishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi ambao wamestaafu na wale wanaotarajia kustaafu. Kweli kilikuwa ni tatizo kubwa na niishukuru Serikali imeangalia kundi kubwa la wafanyakazi hasa wale polisi, kwenye idara ya afya, magereza na uhamiaji; ni taasisi au mashirika ambayo yanaajiri watu wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona sasa kutoka kwenye 33% kwenda 40% ni mwanzo mzuri lakini naomba niishauri Serikali yangu tusiishie pale. Naomba mwaka ujao turudi kule tulikotoka kwenye 50% ili kuwawezesha Watanzania wanaolitumikia Taifa lao kwa jasho usiku na mchana, wanapostaafu wapate mafao yao yanayotosheleza kukimu maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye paragraph ya 83 ya Hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliongelea suala la ajali za barabarani. Mheshimiwa Waziri alitaja takwimu kwamba kwa kipindi cha miaka mitano (2019 – 2024) zilitokea ajali za barabarani 10,093 lakini hizo ajali zilisababisha vifo 7,639 na majeruhi 12,663. Hili ni janga la kitaifa. Ukiangalia takwimu za dunia kila mwaka ajali zinaondoa takriban watu milioni 1.2 duniani kote na nusu za hizo ajali zinatokea kwenye nchi zinazoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia takwimu kwa ajali zilizotokea Tanzania zina athari kubwa kwenye bajeti ya Wizara yetu hii ambayo tunaijadili leo. Ingawa Mheshimiwa Waziri hakutuambia zina athari gani lakini ukiangalia takwimu hasa sisi ambao tumetoka kwenye usafirishaji, kwenye bajeti za nchi zinazoendelea hizi ajali zinakula asilimia tatu ya bajeti nzima ya mataifa yanayoendelea. Kwa maana hiyo kwenye bajeti tunayoijadili hapa kama kama trend ya ajali itaendelea hivi kama ilivyo, tutatumia zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kuwatibia watu au wahanga wa ajali kwenye hospitali zetu na kwenye nyumba zetu. Kwa hiyo, tunalo jukumu kama Taifa kuhakikisha kwamba tunazuia kutokea kwa ajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru leo asubuhi niliona makamanda wetu wa Kikosi cha Usalama Barabarani na Kamati ya Usalama Barabarani. Tunalo jukumu na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nakuona uko hapa, kuhakikisha kwamba tunatafuta mwarobaini wa hizi ajali ili kuokoa pesa ambayo tunaitumia kuwatibia wahanga wa ajali pamoja na ulemavu unaotokana na ajali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu kwenye hili, watu wengi wanakufa na wanakufa siyo kwa sababu wamepata ajali, wanakufa kwa sababu mfumo wa kisheria tulionao ni mbovu. Mtu anapopata ajali ili shirika la bima limhudumie lazima jambo liende Mahakamani na mnajua mlolongo wa Mahakama zetu na watu wengi wanashindwa kutibiwa kwa sababu wengine hawana bima na Serikali haina mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu kwenye hili, ianzishe mfuko wa kuwahudumia wahanga wa ajali ili ajali inapotokea tusisubiri mtu aende Mahakamani ili apate huduma. Mtu anapopata ajali watu wengine kutokana na umaskini, ukoo unaanza kuchangishana ili wampeleke mtu hospitalini. Tunawapoteza watu wakati mwingine kwa sababu ya umaskini wa familia wanazotoka au kwa sababu ya mipango yetu ambayo haiakisi uharaka wa hizi ajali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali yangu tuanzishe mfuko wa kuwahudumia wahanga wa ajali pindi inapotokea tusisubiri Mahakama itoe hukumu, tuwahudumie mara moja hata wale ambao hawana bima na wale wanaotoka kwenye familia maskini. Mfuko huo uchangiwe na mashirika yote ya bima ili mtu akipata tiba, shirika la bima likimlipa zile pesa tulizozitumia kumtibia kutoka kwenye mfuko wa kuwahudumia wahanga wa ajali zikatwe kwenye mafao yako ya bima zirudi kwenye huo mfuko na huo mfuko uweze kuwa endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna malalamiko makubwa sana kwenye viwanda vya maji, Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba unisikilize. Watoa huduma au wawekezaji kwenye sekta ya maji wanayo malalamiko makubwa kwamba wanachajiwa excise duty kwenye working capital na hii wanasema inawaletea umaskini kwa sababu pale ambapo hawakutengeneza faida bado Serikali inaendelea kumtoza kodi kutoka kwenye mtaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii naomba tuliangalie kwa umakini vinginevyo viwanda vyetu vya uzalishaji maji vinaweza vikafilisika na tuangalie trend ya kufunga biashara kwenye sekta hii ya maji, wanasema ni mzigo mkubwa kwao nashauri tuliangalie na tulifanyie kazi kama lina athari kubwa kwenye viwanda hivi badala ya kuvifunga viendelee kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo machache naunga mkono hoja ya bajeti yetu. (Makofi)