Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwamba leo nachangia hotuba ya bajeti kwa mara ya nne na Ludewa ikiwa inashuhudia maendeleo makubwa sana, kwa hiyo ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ludewa kwa kuniamini, kunipa heshima hii na kuendelea kunishauri na kuniamini niweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha nyingi za maendeleo Ludewa, kwa kweli kila mmoja ameshuhudia kasi kubwa ya maendeleo ila kuna changamoto chache ambazo wananchi wanaomba zifanyiwe kazi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni miezi zaidi ya miwili sasa tokea meli ile inayofanya safari zake MV – Mbeya, kutoka Mbeya kwenda mpaka Nyasa haifanyikazi kutokana na mafuriko, maji yalijaa sana wakawa wanashindwa kuendelea kufanya safari zao kwa sababu abiria mpaka kuifikia meli ilikuwa tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ludewa kuna Kata nane za wananchi ambao wana changamoto kubwa za barabara wanategemea usafiri wa meli. Kwa hiyo, niombe sana Wizara husika ikiwezekana watumie bandari ya muda pale eneo la Matema ili huduma ziweze kuendelea kwa sababu Uchumi wa wananchi unaathirika sana kwa kukosekana kwa usafiri wa uhakika wa meli katika Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba matumizi ya Serikali yameongezeka sana kwa mika hii ya karibuni na idadi ya watu pia imeongezeka. Tukianza kuangalia kwa mfano, kuna zoezi la kupeleka umeme vijiji vyote nchini linahitaji mapato mengi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna zoezi la usambazaji wa maji nchini linahitaji fedha nyingi, kuna kujenga barabara za vijijini ili tuweze kusafirisha mazao ya wananchi kutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine, inahitaji mapato mengi sana ya Serikali. Ukiangalia tokea miaka hii ya 1990 kuja huku mbele misaada misaada imepungua sana, tafiti zinaonyesha kwamba misaada imepungua kwa zaidi ya asilimia 50, kwa hiyo ili Serikali iweze kupata fedha kugharamia shughuli zote hizi pamoja na shughuli za elimu, shughuli za afya ni sharti kwamba ikusanye kodi ya kutosha ama ichukue mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kodi ningeshauri sana Serikali ijitahidi sana kuongeza mapato ingawa Bunge lilifanya kazi yake kupitisha ile sheria, leo Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo yupo tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua, sasa sekta yake hii ya mipango inatakiwa iwe mbele iweze kumsaidia sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye kubuni vyanzo vipya vya mapato. Tukianza kuangalia kwa Watanzania Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema hapa kwamba walipa kodi ni wachache sana kwa hiyo wanakamuliwa hao hao kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali inawajibu mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba inaongeza idadi ya walipa kodi na inaongeza vyanzo vipya vya kukusanya kodi. Vilevile takwimu zinaonyesha kwamba sekta isiyo rasmi ni kubwa sana hapa nchini na kusababisha Serikali kukosa mapato mengi sana. Serikali inatakiwa iweke vivutio ambavyo vitawafanya wale watu ambao wapo kwenye sekta isiyo rasmi waweze kuingia kwenye sekta amabyo ni rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatusaidia sana kuongeza kiwango cha mapato ya ndani, kodi yetu inayokusanywa iendane na hali ya uchumi. Hata tunavyoangalia wastani wake, uwiano kati ya kodi na Pato la Taifa tukisimamia vizuri sekta isiyo rasmi na ikarasimishwa watu wakajisajili wakaingia kwenye sekta rasmi tutaongeza wigo kwa kiwango kikubwa sana cha walipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje kuweka sekta hii ambayo siyo rasmi iwe rasmi. Eneo la kwanza ambalo tunaweza tukaangalia ningependa kuishauri Serikali kwanza zile taratibu za usajili mtu akitaka sijui leseni ya biashara, akitaka kibali cha kujisajili biashara yake tupunguze urasimu, kipatikane kwa urahisi kama inawezekana ikapatikana Halmashauri basi kipatikane Halmashauri. Zile leseni za biashara kungekuwa na uwezekano ikitolewa mara moja ndiyo basi kuwe na njia nyingine ya uhakiki kama huyu bwana anaendelea na biashara au amefunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kama inatoa kila mwaka kewa lengo la kumkamata yule ili alipe mapato basi ilitakiwa tuweke utaratibu mwingine ambao ni mwepesi, hata kama kuna mifumo nayo itakuwa nzuri sana. Vilevile yale malipo zile tozo tozo, ada, malipo kwa mtu anayetaka kusajili biashara yake mimi ningeshauri vingeondolewa na zile gharama kwa mtu anayeanza biashara kwa mara ya kwanza kumwambia nenda TRA kachukue tin number kabla hajaanza biashara anaambiwa akalipe kodi ya makadirio vitu kama hivi vinakwamisha watu wengi sana katika kuingia kwenye mfumo rasmi wa biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungetafuta namna fulani ikiwezekana hivi vitu, mtu akitaka kuanza biashara mara ya kwanza asilazimike kuanza kulipa mapato, aruhusiwe aanze, aingizwe kwenye mfumo na baadaye jinsi anavyozidi kufanya biashara tutajikuta tumesajili watu wengi sana kwenye mfumo wa kulipa kodi, kwa hiyo tutapunguza watu kwenye sekta isiyo rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna maeneo mengine ambayo tunaweza tukayaangalia, kwa mfano watu kama TBS, watu kama BRELA wangeongeza ofisi zao mpaka huko Mikoani, sijui wale kwa ajili ya kusajili jina la biashara, unakuta watu wengi wanafanya biashara zisizo rasmi. Maeneo haya tukiyaangalia tukarasimisha biashara, tukapima ardhi ya nchi hii vya kutosha na kusajili kwenye mifumo, tunaongeza sana wigo wa walipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika ile kodi ya majengo watu wa Vyuo Vikuu vya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi na Halmashauri wana teknolojia ile wanaweza wakaenda kwa kutumia mfumo ya GIS wakasajili nyumba zote kwenye mifumo na wakazifanyia uthamini watu wakalipa kodi kulingana na thamani ya jengo ile itasimamia hata haki na itawewezesha watu wengi zaidi kulipa kodi bila usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ulipaji uwe rahisi kuwa kuna kodi nyingi huko ambazo zinaweza zikaongeza mapato ya Serikali, tukifanya haya naamini tutaongeza wigo wa kodi kwa kiwango kikubwa sana, hata mimi Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa nikija nikasema barabara zangu zimeharibika sana na mvua itakuwa ni rahisi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuweza kutoa fedha kwa ajili ya matengezo ya dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Ludewa kwenda Ibumi kule kumeathirika sana, daraja la Mto ketewaka lilikatika pale, Mlima Kimelembe ardhi iliporomoka sana, hata tunavyoomba fedha sisi Wabunge wakati mwingine unakutana na mtihani. Mkandarasi wa kutoka pale Itoni kwenda Lusitu ninavyomwambia Mheshimiwa Bashungwa kwamba ameondoka site wa sababu ya changamoto ya malipo inakuwa ni rahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Njombe muda wa kufanya kazi ni mfupi sana kutokana na kuwa na kipindi kirefu cha mvua, sasa wananchi wanaomba msimu huu ambapo mvua zimekata zitarejea mwezi Oktoba wakandarasi wasikutane na vikwazo vya malipo. Huu ndiyo muda wao ambao wanaweza wakafanya kazi vizuri na kukamilisha ile miradi ya ujenzi ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana eneo hili liweze kutatuliwa ili lisiathiri shughuli za wananchi. Kuna muda kama mwezi mkandarasi haonekani barabarani na anazungumzia ana changamoto ya malipo. Hali kadhalika zile barabara za TARURA na zenyewe tunaomba ziweze kupewa fedha haraka ili msimu huu ambapo wanaweza wakafanya kazi wafanye kazi ili kukuza uchumi wa wananchi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, ni kengele ya kwanza?
MWENYEKITI: Kengele ya pili.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ok kama ni kengele ya pili niseme naunga mkono hoja kwa asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)