Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Gairo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye bajeti kuu. Mimi nitanyoosha maelezo, sitosifu sana kwa sababu sitoki Singida. Tutazungumza yale ambayo yana ukweli. Ili Waziri wa Fedha na Waziri wa Uwekezaji muonekane mnafanya kazi ni lazima kazi yenu ionekane kwa wananchi. Kwa hiyo, siyo kwa sababu tuko CCM pekee humu basi tunasifiana sifiana tu hata kama vitu haviendi vizuri. Kama vitu vinakwenda vizuri tusifiane ndio ubinadamu na kama vitu vinakwenda vibaya tutaambiana ukweli. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu penda sana watu wanaokwambia ukweli kama sisi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka leo nijikite kwanza kwenye barabara. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu naomba unisikilize vizuri sana. Mimi niko kwenye Kamati ya Miundombinu, kwenye Kamati ya Miundombinu barabara ambazo zimechoka Tanzania kongwe ni 71 ambazo muda wake umekwisha na sasa hivi ziko hoi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua mfano tu Barabara ya Shinyanga - Mwanza, Lindi – Dar es Salaam, Njombe – Songea, Morogoro – Dodoma. Pia, chukua barabara za mijini na nyingi nyingi tu, barabara ziko hoi tu. Ukiangalia bajeti ambayo mmeipangia Wizara ya Ujenzi ni shilingi1,700,000,000,000 lakini madeni ni shilingi 1,200,000,000,000. Kwa hiyo, ina maana wao watabakia na shilingi bilioni 500, shilingi bilioni 500 itafanya kazi gani? Hamna chochote tunachotengeneza kwenye hizi barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawalaumu hawa TARURA na TANROADS wao wanafanya kazi nzuri, na ni lazima tuwashukuru hawa ma-MD wa TARURA na TANROADS wanafanya kazi nzuri. Mheshimiwa Waziri, mimi hapa kama hii ndiyo bajeti na kama bajeti ya Ujenzi, bajeti ya TARURA hazitaongezewa pesa za barabara, mimi ndiyo nitakuwa wa kwanza kupinga bajeti. Chukua yale maoni tuliyokupa kutoka Kamati ya Miundombinu ya kuongeza vyanzo vya uhakika vya barabara, huo ndiyo ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki kuzungungumzia habari ya sukari, sijui ya nani na nani kwa sababu ukichimba kote, hawa na hawa tukiongea hapa itakuwa balaa, bora tunyamaze lakini tujikite kwenye hizi barabara zetu. Mheshimiwa tafuta vyanzo vya uhakika, chukua ushauri wetu wa Kamati ya Miundombinu agalau tupate shilingi trilioni 2.2 kwenye TANROADS na tupate shilingi bilioni kama 400 kwenye TARURA ili Wabunge tukienda kule tuonekane tumefanya kazi ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mwaka 2022 ulisema Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuagiza magari ya Serikali Tanzania lakini bado najiuliza swali moja, hii Serikali ni tajiri sana au kuna shida gani? Umekuja ukalalamika na ukaleta mpango kwamba sasa hivi kwa kuondoa gharama hizo kila mtumishi atanunua gari lake ili alionee uchungu atalimiliki. Mwaka huu sijalisikia, sasa inaonekana na sijajua imekuja mpya au ile imeshindikana au vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha msingi mimi najiuliza hivi twende Halmashauri zote za Serikali za Mitaa, Manispaa zote, majiji yote na twende Serikalini kwenye Wizara zote haya magari mabovu mpaka yanaoza na mengine hayauziwi na yakiuzwa, wanajiuzia wenyewe. Hivi hii nchi ina utajiri wa kiasi gani kwamba haipigi mnada yale magari? Nani alishawahi kusikia hapa kwamba kuna gari la Serikali linauzwa kwenye minada? Haijawahi kutokea. Kwa hiyo, magari yote mnajiuzia wenyewe tena kwa tender. Unakuta gari ambalo lingepigwa mnada kwa shilingi milioni 70, shilingi milioni 80 utakuta limenunuliwa kwa milioni tano, milioni sita. Halafu tunazungumzia habari ya kwenda kuwaminya watu wadogo wadogo hawa huku chini wakati huku kuna pesa nyingine zimelala lala tu, hicho kitu hakiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twendeni pale kwangu Gairo tu nina magari saba, ukienda hapa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma huwa napitapita magari yako kibao. Ukienda manispaa zote yanauzwa vipi? Yanatakiwa yauzwe kwa mnada, tunaomba usimamie vitu kama hivyo. Mimi ukitekeleza hivyo na ukinijibu hivyo nitaunga mkono hoja yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni habari ya hii pesa. Hizi taasisi zenu za Serikali mnakwenda mpaka huko mnazisifu kwamba fulani wameweka gawio bilioni tatu, Bandari wameleta shilingi bilioni nne, EWURA shilingi bilioni tatu halafu mnashangilia kweli sasa hivi taasisi zetu… Haya National Housing bilioni ngapi wakati ina madeni kibao? Sijui nani ana bilioni ngapi. Sasa mimi najiuliza swali hivi sasa hivi kila taasisi imekuwa TRA? Yaani sasa hivi hatuna TRA. Pamoja na kuwa Serikali inategemea TRA kukusanya kodi na kufanya maendeleo ya nchi lakini sasa hivi kila taasisi ya Serikali ikianzishwa inakuwa TRA. Ikianzisgwa sijui EWURA inakuwa TRA, ikianzishwa LATRA inakuwa TRA, ikianzishwa Bandari inakuwa TRA, OSHA nayo TRA yaani kila mtu anakuwa TRA. Ukienda kule TANAPA nayo imekuwa TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nafikiri ule mpango wa awamu ya tano ulikuwa siyo mbaya wa kuchukua zile pesa zote halafu wao waandike bajeti kwamba sisi ni taasisi fulani bajeti yetu ya mwaka ni hii. Ninyi BOT mnachotakiwa kufanya ni kuwafungulia akaunti tu iwe single treasury account. Wafungue single treasury account ili pesa zote wanazokusanya ziingie kwenye akaunti kuu ya Serikali halafu wao wanakuwa na bajeti na ninyi msiwache kuwapelekea. Halafu zinazobaki kwa mwaka ndiyo gawio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ikibaki labda kwenye taasisi fulani imekusanya shilingi bilioni 100 lakini bajeti yao ilikuwa ni shilingi bilioni 50 maana yake pale tayari kuna shilingi bilioni 50 zetu. Sasa mnawaachia wao wanapanga, wanatengeneza, wanatunga na wanatandika (wanazila) zile pesa halafu zikija huku mnashangilia vihela vidogovidogo. Mnapewa vihela vidogo, aah, hii taasisi inajiendesha na ina gawio shilingi bilioni tatu. Hivi kweli bilioni tatu kwenye taasisi zinazokusanya pesa namna hii, halafu tunakuja hapa tunakuwa washangiliaji. Mimi siwezi kuwa mtu wa kushangilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ukweli na ukiona Wabunge wametulia namna hii ujue wanasikiliza kwa makini, hii inawangia, ndiyo ukweli. Kwa hiyo, nilikuwa nakuomba Mheshimiwa na nakuona hata unavyopata taabu. Juzi hapa nilikuona unapata taabu sana ya kutafuta pesa lakini kuna baadhi ya taasisi zako zilikuwa zinakupinga, hiyo mimi ninaijua lakini ukiwa Waziri wa Fedha unatakiwa uwe ngangari. Kama umeshindwa kuwa ngangari unatakiwa uachie nafasi ili hata mimi nije nikae hapo. Mheshimiwa Waziri uwe ngangari, unafanya kazi nzuri lakini kuwa ngangarti kwenye hivi vitu. kila mtu akitaka achukue pesa na Mheshimiwa Waziri hapo ukitaka kuwa mzuri kwa kila taasisi hiyo kazi haiwezekani. Nchi imefikia mahali sasa hivi na lazima tuseme ukweli, wapigaji wamekuwa wengi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapigaji ni wengi na wengine utasikia tu Mama anaupiga mwingi. Siyo anaupiga mwingi kwamba anamsifia kwenye moyo, hapana anaupiga mwingi yeye anaiba hela. Anatandika pesa halafu akija huku anajifanya anasifia. Hata wewe Waziri wa Fedha na taasisi yako ya Mamlaka ya TRA nyie ndio mnaopata taabu. Ninyi lazima mkusanye kodi, mzilete kwenye mishahara, lazima ninyi huku ndiyo mzipeleke kwenye maendeleo wakati ukiangalia kuna taasisi nyingine mkizichanganya zinakusanya nusu ya TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo sitaki kuongea mambo mengi. Nafikiri amenielewa na ndiyo maana ameweka mikono hivi najua hapo amenielewa. Ahsante sana kwa kunielewa naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)