Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kupewa nafasi hii ya kufungua pazia kwenye Wizara hii muhimu sana kwa ajili ya Wizara ya Maji. Awali ya yote kabisa nimshukuru kwanza, ninaishukuru Serikali chini ya Mheshimiwa Rais, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli kwa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais, anaenda kufanya kwenye Wizara hii ya Maji nchi nzima lakini hususani Kasulu Vijijini.

Mheshimiwa Spika, Kasulu Vijijini tumepokea miradi mingi sana kwenye mwaka wa fedha uliyopita, kwa kutaja tu kidogo, tumepata mradi wa maji kwenye Kata ya Titye, Rusesa, Nyamnyusi, Kagera Nkanda na Mvugwe. Hii miradi inaenda kunufaisha watu zaidi ya 72,000 na gharama yake ni zaidi ya shilingi karibia bilioni tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapenda kusema Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya hasa ambayo yeye mwenyewe aliamua kuifanya kwa kuanza na kuasisi ile kauli mbiu kwamba ya kumtua mama ndoo kichwani, naamini kabisa Taifa hili litaendelea kumkumbuka Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kupitia sekta hii ya maji. Mheshimiwa Aweso ninakushukuru sana kwa namna ambavyo umekuwa unasaidia kutafasili maono ya Mheshimiwa Rais. umezunguka nchi nzima lakini na Kasulu Vijijini ulifika, nakumbuka ulifika pale mwaka jana na kwa kweli ukawatua wakina mama wa Kata ya Makele ndoo kichwani, tunakushukuru sana, wewe ni mtu mnyenyekevu, mfuatiliaji, mchapakazi lakini ni mtu ambaye unaweza kufanya maamuzi, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini hata ndugu yangu, kaka yangu Kundo, amepata mtu sahihi wa kuweza kumwelekeza kazi vizuri na atafanya kazi vizuri kwa sababu na yeye ni mchapakazi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitaanza na Mfuko wa Maji. Mfuko wa Maji ni nyenzo muhimu sana ambayo inapaswa kutumika kusaidia sana kutatua kero za shida ya maji lakini zipo changamoto. Mfuko wa Maji hauna fedha za kutosha lazima Serikali iumize kichwa, lazima Serikali itafute vyanzo mbadala au vyanzo vingine vya kuhakikisha kwamba mfuko wa maji unakuwa na pesa ya kutosha. Kwa sababu kama mfuko wa maji hauna fedha za kutosha maana yake nini? Maana yake tija yake inakuwa siyo kubwa sana, lazima tumekaa nao kama Kamati mara kadhaa, moja ya changamoto yao kubwa ni kukosekana kwa fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanayo miradi mingi ambayo wanapaswa ku-finance lakini hela ni kidogo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naamini umekuwa unapambana na Mheshimiwa Rais, amekutuma sehemu mbalimbali kwa ajili ya kutafuta fedha za maendeleo, wapeni mfuko wa maji hela za kutosha ili waweze kutekeleza miradi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo hapo kwenye Mfuko wa Maji. Kwenye mfuko wa maji wanadirisha la mikopo, kwa maana kwamba zile mamlaka kubwa za maji zinaweza kwenda kukopa pale kwenye mfuko wa maji, sasa tunaomba utaratibu wa utoaji wa mikopo usimamiwe vizuri na uimarishwe, maana yake zipo bado taasisi ambazo zinazo uwezo kabisa wa kwenda kukopa na kujiendesha kibiashara, bado wanaenda kuomba fedha za ruzuku kitu ambacho siyo kweli siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha za ruzuku zinapaswa kwenda vijijini, Kasulu Vijijini kule, Kibondo, Buhigwe, Pangani, siyo kwenda kufadhiri miradi ya taasisi kubwa kama DUWASA, DAWASA hawa wakubwa hawa, hawa nadhani wanapaswa waende kwa maana ya kwenda kukopa kwa utaratibu ambao umewekwa ili waweze kurudisha, hela za ruzuku ziende vijijini kwa ajili ya kusaidia kule kwa sababu taasisi za kule hazina uwezo wa kujiendesha kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nizungumze kuhusu suala la mradi wa maji wa Ziwa Tanganyika. Kwanza, Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana kwa sababu imekuwa ni kiu na wimbo wetu mkubwa wa siku zote, mradi huu unaenda kunufaisha Mkoa wa Kigoma, Katavi pamoja na Rukwa. Tumeusubiri kwa hamu sana, na tunashukuru hata kwa angalau sasa tumeambiwa mwaka huu wa fedha mnaenda kutafuta mshauri elekezi. Tunaomba sana kwa kweli mradi huu uharakishwe kwa sababu wananchi wanahitaji maji ya uhakika kwenye Mikoa hii mitatu. Mimi nasema huu mradi ukikamilika Mheshimiwa Aweso, Mikoa hii itamkumbuka sana Mheshimiwa Rais, kupitia mradi huu na wewe mwenyewe kama Waziri wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kuhusu suala la hati fungani (green bond). Kwetu Tanzania ni kama jambo jipya lakini ni jambo ambalo ni muhimu sana kama alternative source of financing ya miradi. Kwa sababu ukiangalia mahitaji ya maji katika nchi hii ni makubwa yaani miradi ipo mikubwa ambayo inahitaji pesa na wakati mwingine inazidi hata uwezo wa Serikali kuigharamikia yote kwa Pamoja, lakini kupitia hati fungani tumeona inawezekana kupitia Tanga UWASA.

Mheshimiwa Spika, Tanga UWASA wame-issue bond, mwaka jana walikuwa wana-target ya kukusanya shilingi bilioni 53 imeenda zaidi na sasa hivi wamekusanya shilingi bilioni 54, kwa hiyo sasa wanaweza wakafanya miradi yao vizuri, watu wamewekeza pale. Wapo watu wanahitaji kuwekeza, wapo watu ndani ya nchi na nje ya nchi wanahitaji kutoa fedha zao kwa ajili ya kuwekeza kupitia miradi ya maji na miradi ya maji ikisimamiwa vizuri, ikiwa designed vizuri na ikisimama vizuri ni uwekezaji mzuri ambao hauna shida yoyote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, kama Tanga UWASA imewezekana tunaamini hata taasisi zingine za maji hizi kubwakubwa ambazo vitabu vyao vya hesabu vipo vizuri wanao uwezo wa kwenda huko, kuliko kuanza kulialia kwamba wapewe ruzuku, wanaweza pia kuanzisha huu utaratibu wa hati fungani wakapata fedha watu wakawekeza. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Aweso hili ulifanyie kazi ni alternative way ya kupata fedha kwa ajili ya ku-finance miradi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali Mheshimiwa Aweso, tarehe 18 Julai, mwaka jana ulikuja kwangu Jimboni Kasulu Vijijini. Kwanza nakushukuru kwa sababu ya utendaji kazi mzuri uliyotukuka wa aliyekuwa Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kasulu ulimsimika pale pale kwamba awe full na kweli tunashukuru, kijana ulimpa morali kubwa ameshathibitishwa sasa ni Meneja kamili na kazi anachapa kweli kweli, pia niseme wazi tu Mheshimiwa Aweso, kwamba ile ahadi ambayo ulisema utatusaidia ya gari kwa ajili ya Meneja wa RUWASA ili aendelee kuchapa kazi vizuri bado naendelea kukumbusha kwamba haijafika. Nakuomba sana Kaka yangu najua wewe ni msikivu hilo halikushindi lipo ndani ya uwezo wako utusaidie gari ili Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kasulu aweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru kwenye hotuba yako umesema unaenda kutoa visima vitano kwenye kila Jimbo na naamini Kasulu Vijijini, tutapata na mimi kwa sababu huwa silazi damu ulivyosema tu hapa nilimpigia simu Meneja huyo huyo wa RUWASA tumepanga tayari, visima vitano tunachimba Kijiji cha Malalo, Kazage, Chekenya, Kabulanzwili na Mkiheta. Hapa nimesema wazi na wananchi wamesikia kwa hiyo tunasubiri visima vitano tukawachimbie wananchi wapate maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)