Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Wizara hii muhimu ya Maji. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso na Naibu wake na Watendaji wote wa Wizara hii ya Maji kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha Watanzania wanaenda kutatuliwa kero zao za maji kama siyo kuisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita itaacha historia ya aina yake katika utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii ikiwemo katika sekta hii ya maji. Wananchi wa Arusha hatuna budi kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaona ni jinsi gani Dkt. Samia anaendelea kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kweli Dkt. Samia yupo kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hii slogan ya kusema kuwa “Kumtua Mama Ndoo Kichwani” tukumbuke kuwa slogan hii haijaanza leo wala jana, aliianzisha Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa Makamu wa Rais na tumeona nia dhahiri ya Dkt. Samia, kuhakikisha anamtua mama ndoo kichwani na alisema mama kwa sababu kina mama wengi ndiyo wamekuwa wakipitia changamoto ya maji kutafuta maji katika mazingira ya hatari, kuamka usiku mama kwa ajili ya kwenda kutafuta maji. Kwa hiyo, tunaona lengo rasmi na nia ya Dkt. Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais katika kipindi kifupi cha utawala wake ameweza kutekeleza miradi 47 yenye thamani ya shilingi bilioni 20 na kuwezesha upatikanaji wa maji katika vijiji 35, amepandisha upatikanaji wa maji kutoka 69.4% hadi wastani wa 73.5%, idadi ya vijiji vinavyopata huduma imeongezeka kutoka vijiji 304 hadi vijiji 339 sawa na 87% ya vijiji kwa Mkoa wote wa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika Jiji la Arusha, nadhani wote mnaelewa jiji la Arusha tulipata mradi wenyethamani ya shilingi bilioni tano na 20 ambao ni karibu bajeti ya Wizara nzima, sisi ni nani tusiishukuru Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia. Mradi huu umekuwa chanzo kikubwa cha maji kwa Wilaya hata zilizo za Jirani zisizo na vyanzo vya uhakika vya maji ambapo Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa kimkakati kutoka mradi mkubwa wa Jiji la Arusha kwenda Monduli katika vijiji 13 katika Wilaya ya Monduli Mjini, gharama ambayo ni shilingi bilioni 20.3 ambapo itahudumia jumla ya watu 34,000.

Mheshimiwa Spika, sambamba na mradi huu Serikali imeendelea na mradi wa vijiji vinne ambavyo ni Makuyuni, Naiti, Mbuyuni na Loosimingor wa shilingi bilioni saba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na malalamiko ya wakazi wa Jiji la Arusha kuwa bili zinakuwa kubwa sana za maji lakini tatizo kubwa siyo katika Mamlaka ya Maji ya Jiji la Arusha, tatizo kubwa lipo katika Wizara ya Nishati. Kwa sababu maji yale yanasukumwa kwa pump, bili inayokuja katika Mamlaka ya Maji ya Jiji la Arusha inakuwa kubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali waangalie Wizara ya Nishati ni jinsi gani watawapunguzia gharama za umeme Mamlaka ya Jiji la Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitakuwa mchoyo wa shukrani nisipomshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Arusha (AUWSA) Ndugu Lujoba pamoja na Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Arusha Ndugu Makaidi, wamekuwa wakifanya kazi vizuri, wamekuwa wakishirikiana katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha wakazi wa mji wa Arusha wanapata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna ule mradi wa Mlangarini wa shilingi bilioni 3.7, mradi huu tuliambiwa unakamilika Disemba. Disemba imebaki miezi michache sana, Mheshimiwa Waziri naomba sana mradi huu ukamilike kwa wakati. Kuna mradi wa Enguik Monduli wa shilingi bilioni mbili, utekelezaji wake umefikia asilimia 67, Mheshimiwa Waziri mlisema unakamilika mwezi Juni, bado wiki tatu tu tufike mwezi Juni, ninaimani Mheshimiwa Waziri mwezi ujao wana-Monduli wanaenda kufurahia maji haya ambayo Mama Samia aliweka slogan yake ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina imani Mheshimiwa Waziri, mwezi ujao wana Monduli wanaenda kufurahia maji haya ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliweka slogan yake ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa Imbaseni upo Arumeru wa shilingi bilioni moja na mwenyewe waliahidi watakamilisha mwezi Juni, mwezi Juni bado wiki tatu. Mheshimiwa Waziri, najua kabla hatujaondoka kwenye Bunge hili atatukabidhi miradi yetu miwili ya Imbaseni, Arumeru na miradi ya Monduli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa Oldonyosambu wa shilingi bilioni sita, tuliambiwa unakamilika mwezi Juni, 2025; hapa bado una muda. Changamoto kubwa ya wakazi wa Oldonyosambu ni Fluoride ambayo kina mama wengi walikuwa wanapata shida wanapobeba ujauzito wanajifungua watoto wenye matatizo ya meno na mifupa.

Mheshimiwa Spika, kimekuwa kilio cha muda mrefu sana. Tunaishukuru sana Serikali hii sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuna wataalamu wapo pale, kwa ajili ya kuchunguza na kurekebisha hili tatizo. Tunategemea matokeo mazuri na sasa kina mama wataenda kubeba ujauzito, watajifungua watoto wazima kama ambavyo inatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa Mageri, Ngorongoro mradi wa shilingi bilioni sita. Utekelezaji wake umekamilika asilimia 52, wametuambia mpaka mwezi Juni, mwaka kesho mradi huu utakamilika. Mheshimiwa Waziri miradi hii nitaifuatilia kwa karibu sana kwenye Mkoa wa Arusha. Tunataka miradi hii ikamilike kwa wakati ili wananchi wa Arusha, waendelee kuwa na imani na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na ikifika 2025, wampe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kura za kishindo. Sasa miradi hii msipoikamilisha itakuwa hamna nia nzuri na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu kashatenga bajeti. Tunataka miradi ikamilike wananchi wa Arusha wakapate maji ya kutosha, maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa Seed Farm wa Nanja wa shilingi bilioni 27 ambao utatiririshwa maji yake kutoka katika huu mradi mkubwa Jiji la Arusha ambao utasafiri kutoka Seed Farm Ngaramtoni hadi Nanja. Watu wa Monduli Mjini, Engutoto, Monduli Juu, Lashaine hadi Nanja watafaidika na maji haya. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tukafanye kama ambavyo tumepanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipindi cha mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha tulipata hasara ya uharibifu wa miundombinu katika Bwawa la Nanja, lililopo Monduli linalohudumia zaidi ya Kata saba. Tunashukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tulipewa shilingi milioni 354, Bwawa likakarabatiwa na kudhibiti maji yaliyokuwa hatarini kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hii programu ya visima 900, ambayo wamesema kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa kila jimbo visima vitano. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaamini utendaji wake. Tunajua mama yupo kazini na mama halali amekuwa akihangaika usiku na mchana kuhakikisha kero zetu Watanzania wote zinatatuliwa. Hakuna kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba visima hivi vikachimbwe kwa wakati. Waheshimiwa Wabunge wa majimbo wakitoka humu ndani, waende moja kwa moja kwenye majimbo yao wakaanze kuchimba visima kwa ajili ya wananchi ili wananchi wapokee zawadi hii iliyotoka kwa mpendwa wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba niishie hapa kwa leo na ninaunga mkono hoja asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)