Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza kwenye mambo manne. Kwenye gharama za umeme kwa mamlaka za maji nchini, kwenye mita za pre-paid, changamoto ya maji taka kwenye majiji pamoja na fursa ya mradi mkubwa tulio nao kwenye Jiji letu la Arusha.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia mamlaka zetu za maji nchini, mamlaka kama ya maji Jiji la Arusha (AUWSA) wana deni la umeme kama la bilioni 4.95 kutoka kwa wenzetu TANESCO, Mamlaka ya Maji Jiji la Dar es salaam (DAWASA) wana deni kama la bilioni 36 na mamlaka ya Maji ya KASHWASA wana deni la bilioni 2.97.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa data tulizo nazo, ukiangalia kwenye taarifa hii moja inaonesha kuwa Mamlaka ya Maji Jiji la Arusha wao wanakusanya 2,325,000,000 kwa mwezi lakini umeme pekee wanalipa kiasi cha bilioni 1,100,0000,000 ambayo ni sawa na asilimia 47 ya wanachokikusanya. Mamlaka ya Maji ya Jiji la Dodoma (DUWASA) wao wanakusanya 2,200,000,000 lakini wanalipa umeme milioni 843 sawa na asilimia 38. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Kahama (KUWASA) wao wanakusanya milioni 290 na umeme wanalipa milioni 140, sawa na asilimia 48. Nikimalizia na KASHWASA wao wanakusanya 1,325,000,000 wanalipa umeme milioni 666 sawa na asilimia 50.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye data za namna hiyo utagundua mengi. Kwa mfano kwenye taarifa niliyo nayo inaonesha kuwa DAWASA pamoja na kukusanya bilioni 2,600,000,000 lakini kwenye upande wa KVA (kilo-volt-amperes) pekee wanalipa kiasi cha shilingi milioni 288; na pia wanalipa pia VAT milioni 370.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka yetu ya Maji Safi na Maji Taka ya Jiji la Arusha wanalipia umeme kwa maana ya kwenye bili ya maji kwa mwezi kiasi cha shilingi bilioni 1,100,000,000 lakini kwa upande wa KVA ni milioni 94 na VAT ni milioni 150.
Mheshimiwa Spika, nimesema nisome data hizi ili tuone namna ambavyo wenzetu wa mamlaka za maji wanavyopata mzigo mkubwa wa kulipa bili za umeme ilhali mitambo yao inatumika kwa ajili ya kutoa huduma na wala si kwa kufanya biashara kama ya kupata faida kwa watu wengine. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba; na nilikuwa ninateta pia asubuhi na Mheshimiwa Waziri Mkuu; kwamba kwa sababu jambo hili linahusisha Wizara tatu, linahusisha Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Fedha; ni vizuri Wizara hizi zikakutanishwa ili wakatoa ahueni kwa Wizara ya Maji ili hatimaye mamlaka hizi ziendelee kupunguza mzigo kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ukiwaambia leo walipe VAT na wao hawachaji VAT kwa wananchi unawapa gharama kubwa za uendeshaji na baadaye wanalazimika kuongeza gharama zaidi kwa mwananchi; na hatimaye mabilioni haya yanayokwenda kwa Watanzania yatakuwa hayana tija sana. Kwa sababu wananchi watakuwa wanalalamika sana kubambikiwa bili, gharama kubwa za maji kutokana na mzigo mzito ambao wenzetu wa mamlaka za maji wanao. Kwa hiyo ombi langu la kwanza lilikuwa ni hilo. Kwamba tumwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Kiongozi Mkuu wa Serikali katika suala la utendaji aweze kuzikutanisha wizara hizi ili tuweze kuangalia namna nzuri zaidi ya kukumbana na changamoto hii.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusiana na mita za pre-paid. Nilimsikia Mheshimiwa Rais akitoa maelekezo kwa Wizara ya Maji kuhakikisha kwamba wanafunga mita za pre-paid ili kuendelea kupunguza malalamiko ya wananchi ya kubambikiwa bili za maji na kuwa na bili kubwa za maji. Tunafahamu kuwa Wizara ya Maji wameshaanza kufanya kazi hiyo kwenye maeneo mbalimbali. Sisi watu wa Arusha ambao tuna wateja 123,204 mpaka sasa wameshaunganishiwa wateja 325 ambao ni sawa na asilimia 0.26. Hii ni ishara ya kwamba bado kazi kubwa inatakiwa ifanyike. Ninajua jambo hili Mheshimiwa Waziri analifahamu, na ninafahamu kuwa amefanya kazi kubwa ya kuhamasisha na kuelekeza lakini bado kazi ya ziada inatakiwa ifanyike ili wananchi wenzetu waweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ni kuhusiana na maji taka. Ukiangalia Taarifa ya Kamati ya Bunge ambayo waliisoma hapa Bungeni, ninakumbuka ilikuwa ni tarehe 9 Februari, 2024; Kamati ya Bunge ilisema kwamba “kwa kuwa miundombinu ya maji taka katika miji na majiji bado hairidhishi kwa kiwango kinachostahili; na kwa kuwa hali hii inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa kwa wananchi hali ambayo inaweza kuathiri shughuli za uzalishaji;” kwa hiyo inaonekana kabisa hii changamoto ya maji taka ni kubwa. Sisi Jiji la Arusha tumepata mradi mkubwa sana wa maji wa bilioni 520, na kabla ya mradi huo mtandao wa maji taka uliopatikana ulikuwa ni wa 7.66%.
Mheshimiwa Spika, uwepo wa mradi huu mkubwa umeweza kuitoa hiyo 7.6% kwenda hadi asilimia 30. Kwa hiyo unaweza ukaona kabisa kwamba asilimia 70 ya wananchi wa Jimbo la Arusha bado hawana uwezo wa kupata huduma za maji taka kutokana na uwezo mdogo wa fedha zilizopo. Kwa hiyo ningependa kumwomba Mheshimiwa Waziri, ninajua ametusaidia sana Jiji la Arusha tuna kiwanda chetu cha A to Z ambacho kimeajiri watu zaidi ya 10,000, kwa kile cha mjini na cha kule Olmoti; lakini kuna mtaro wa maji taka ambao una changamoto kubwa sana kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, ninajua Mheshimiwa Waziri alishafika hapo na tayari kuna fedha zimekwishatolewa kama 1,152,000,000 na bado kuna mahitaji ya 1,362,000,000. Kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri atumalizie fedha hizi ili tuondoe changamoto baina ya kiwanda, kwa maana ya mwekezaji na wananchi, hasa wa mitaa ya olmoti na Mtaa wa Olteves.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, ukienda Masklia kwenye Kata ya Telati tumejenga bwawa kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 22 za maji taka kwa siku. Changamoto iliyopo, wananchi wanaozunguka pale, wa Mtaa wa Masklia wanataka wafanye shughuli za kilimo na masuala mengine kwa kutumia maji yale, lakini hawajapelekewa miundombinu ya kufika kwenye mashamba yao.
Mheshimiwa Spika, ninakumbuka jana tulizungumza kwa pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Maji. Ninaomba jambo hili tulipe uzito unaostahili ili wananchi wenzetu waweze kutumia fursa ile ya maji taka kama mbolea na kwa hivyo waweze kufanya shughuli za kilimo vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya changamoto ya muda tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwa usimamizi wa Waziri Aweso na Naibu wake, Katibu Mkuu na timu nzima kwa namna ambavyo wametupatia mradi mkubwa wa maji wa bilioni 520.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia; kuna maeneo ambayo bado hayana maji, hasa kwenye maeneo ya pembezoni kama kwenye Kata ya Telati, kuna mitaa ya Bondeni, Olekolesi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)