Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara yetu hii ya Maji.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika sekta zote na hasa katika sekta hii muhimu amefanya makubwa sana nchini na katika Jimbo langu la Namtumbo kwa kuwatoa akina mama kutoka kwenda mwendo mrefu kufuata maji na kuleta majumbani na kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia ninaomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Aweso, Waziri wa Maji, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, wataalamu wote na wakuu wa taasisi walio chini ya wizara hii. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi mzuri sana na ushirikiano mkubwa anaotupa sisi Waheshimiwa Wabunge pamoja na watumishi wote katika wizara yake, wa juu mpaka wa chini. Ninakmwombea kila la kheri katika kazi hii anayoifanya, Mwenyezi Mungu aendelee kumpa hiyo busara na hekima katika kazi yake ya kulitumikia taifa hili. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika wilaya yangu Mheshimiwa Waziri amefanya mambo makubwa sana. Nilipomwendea mara ya kwanza kumwambia kwamba nina maeneo ambayo yana shida ya maji aliniambia, rudi nenda kakae na DM na RM wako wa mkoa, kaorodheshe maeneo yote yaandaeni tuleteeni tutaanza kuweka kwenye bajeti. Kwa hiyo ninaomba nimshukuru leo mbele ya Bunge hili Tukufu. Tupeleka miradi mikubwa isiyopungua 15 na yote imefanyiwa kazi. Ninamshukru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna mradi wa maji ambao ulikuwa kama donda ndugu, ulikuwa kizungumkuti mradi wa Walitora-kumbala. Mradi huu ulisimama kwa muda wa miaka isiyopungua saba bila kufanya kazi. Tulipeleka taarifa za mradi ule na sasa leo hii watu wanakunywa maji katika Kata ya Litora na Kumbala. Pia tuna mradi wa maji Lingusanguse. Lingusanguse ni kijiji ambacho hakikuwa na maji kabisa, hawakuwahi kupata maji ya mtiririko lakini leo wanakunywa maji ya mtiririko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi wa tatu ni Mradi wa Ilumbahiro na Ikesi, nao ulilala ni wa miaka isiyopungua nane; lakini tulipompelekea taarifa za mradi huu walianza kutuwekea bajeti na unaendelea, ambapo sasa hivi wamefikia asilimia 80, na wanakunywa maji. Tuna Mradi wa Maji Mgombasi, kule Mgombasi hatujawahi kupata maji ya mtiririko; kulikuwa na maji ya visima na akina mama walikuwa wanakwenda kuchota maji mabondeni, wanakwenda kwa mwendo mrefu. Leo wametupatia mradi huu wa 2,700,000,000. Mradi huu umejengwa lakini umebakia eneo kidogo tu ambalo ni kwa ajili ya mabomba ya nchi nane. Changamoto ambayo imebaki ni kwenye kupatikana kwa mabomba ya nchi nane ambayo inaonekana mkandarasi hajalipwa ili PLASCO waweze kutusambazia hayo maji kutoka kwenye tenki.
Mheshimiwa Spika, chanzo cha maji kimejengwa, tenki limejengwa, visambazio na mabomba madogo mpaka kwenye vituo vya maji vyote vimejengwa. Bomba la nchi nane kutoka kwenye tenki la maji kuleta chini kwenye visambazio na vituo vya maji kwa ajili watu waweze kuteka maji hayo ndiyo bado. Kwa hiyo tunaomba sana mradi huu ukamilike. Hilo bomba la inchi nane linunuliwe na kuletwa pale. Sio mita nyingi sana na si kilomita nyingi sana, ni chache, lakini ni hapo ndipo tulipokwama; hatuna bomba la inchi nane. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna mradi mwingine wa maji wa Msisima ambao unaendelea katika Kata ya Msisima na Vijiji vya Mnalawi. Utekelezaji wake unaendelea, upo vizuri, ujenzi wa kichotea maji kile umeshakamilika, ujenzi wa tenki lita 200 umekamilika na kazi inaendelea. Kwa hiyo tunamshukuru sana na wananchi wa kule wanamshukuru sana. Mradi wa maji Mchomolo nao unaendelea vizuri sana, ujenzi wa chanzo cha maji umekamilika, ujenzi wa lita 300 nao umekamilika. Kwa hiyo tunaendelea vizuri na usambazaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Misufini, kazi ya kwanza ya kuchimba visima ilifanyika kwa kutumia gari zile walizotuletea; tunashukuru sana. Sasa hivi tumeshatangaza ili kupata mkandarasi wa kuweka mabomba na kujenga matenki kwa ajili ya kusambaza maji. Kwa hiyo tunamshukuru sana kwa kazi hii nzuri ambayo ameifanya katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna Mradi wa Limamu ambao tumeshapitia, umekamilika na sasa hivi tunaomba kibali kwa ajili ya Mradi huo. Pia Mradi wa Maji Rumecha Mtakanini wa milioni 200, tulishachimba kisima na sasa hivi tupo katika hatua hizi za usambazaji wa maji. Pia kuna Mradi wa Maji Hanga, mradi huu nao ni miongoni mwa ile miradi ambayo ni donda ndugu. Huu ninaomba waufanyie kazi. Kati ya ile miradi miwili iliyokuwa donda ndugu mmoja aliufanyia kazi na umekamilika lakini Mradi huu wa Hanga ambao sasa hivi upembuzi yakinifu ulishafanyika, sasa watu wamesubiri zaidi ya miaka nane lakini bado mradi huu haujaanza. Tunaomba sana tupate kibali cha kuanza mradi huu ili mradi uweze kuanza. Juzi nilikuwepo Kata ya Msindo na Kata ya Hanga. Kule malalamiko yao makubwa ni kwamba mradi huu umechukuwa miaka mingi na haujaanza; na wanaona maeneo mengine miradi inaendelea lakini katika Kata hii ya Msindo na Hanga mradi huu haufanyika. Kwa hiyo tunaomba sana mtusaidie.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusu kuboresha maji Namtumbo Mjini; tunashukuru sana leo asubuhi Naibu Waziri amenijibu vizuri sana hapa. Pale Namtumbo Mjini mradi ule ulijengwa miaka ya 80, wakati huo kabla haujawa mji na wala haujawa Makao Makuu ya Wilaya, kilikuwa ni kijiji tu; kwa hiyo ni mradi wa siku nyingi. Miaka miwili ya nyuma walitusaidia, walitupatia bilioni 1.5…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.
Mhe. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba mtusaidie. (Makofi)