Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Wizara ya Maji. Nikupongeze sana Mheshimiwa Aweso na timu yako kwa kazi kubwa mnazofanya. Kwa kweli mnafanya kazi kubwa. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamekupongza kwa usikivu wako na mimi nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu, Engineer Mwijuma, mnafanya kazi kubwa, Mheshimiwa Waziri kwa kweli tuna imani na timu yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee kwa sababu mimi nanufaika na miradi ya maji vijiji, nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, kaka yangu Clement, anafanya kazi kubwa sana kule vijiji na kuhakikisha kwamba maji yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa nimetunza pongezi za Mheshimiwa Rais, niziseme hapa sasa. Namshukuru sana na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi Wanamkoa wa Simiyu sasa hatuna deni naye, mwaka jana tarehe 10 Mwezi wa Tano, nilichangia hapa kwa uchungu sana; Mheshimiwa Aweso unakumbuka, mpaka nikataka nikata kushika shilingi yako. Mama yangu Mheshimiwa Esther alichangia hapa na Mheshimiwa Mpina alichangia hapa juu ya mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria. Sasa nitamke rasmi kwamba sasa ule mradi umeanza na mwezi wa pili ulikuwa na asilimia nne, kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali kusaini mkataba wa bilioni 444 kwa ajili ya Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria ambao unakwenda ku-solve matatizo yote ya Mkoa wa Simiyu, Busega, Itilima, Bariadi kwa kaka Kundo, Maswa pamoja na Meatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli peleka pongezi zetu kwa Mheshimiwa Rais, hatumdai kwenye mradi huu. Tunachokuomba Mheshimiwa Aweso, utakapokuwa unapeleka pongezi hizi na shukurani zetu kwa Mheshimiwa Rais, tunaomba sasa umuombe apande aje azingue rasmi mradi wetu, tumpe maua yake, aje Busega kwa sababu ndiyo kuna chanzo, ninajipendelea sana kwa sababu mimi ndiyo mchangiaji wa kwanza kwa Mkoa, basi aje Busega tuzindue ule mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria ambao utakuwa unapeleka maji kwenye Mkoa wetu wa Simiyu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tayari clearance za site pale Lwango kwa ajili ya kujenga tank kubwa la maji la ujazo wa lita milioni 5 umeshaanza na mimi nimeshuhudia pale. Nimeshaenda zaidi ya mara mbili, nimekutumia picha Mheshimiwa Aweso, umeona kazi inayofanyika pale ni Dhahiri tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, umesema hapa habari ya visima, sisi pale na Meneja wangu wa RUWASA wa wilaya tuna database ya vijiji vyetu. Tunavipa priority kulingana na matatizo yaliyopo, sisi tumeshamaliza kuweka kwenye orodha; tunaanza na Malili, tunaenda Ngunga, Mwamgoba, Ngasamo tunamalizia Nasanga. Sisi vijiji vyetu vitano ndiyo hivyo tulishamaliza, kwa sababu tuna data ya vijiji vyote ambavyo bado vina changamoto ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, meneja wangu wa wilaya ni mzuri, ananisaidia vizuri sana, nimeshaleta taarifa zake kwako, yeye ndiye anayejua, Mheshimiwa Aweso huwa unasema, anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mhemo wa mgonjwa. Kwa hiyo, mimi na meneja wangu wa RUWASA wa Wilaya ndiyo tunajua mihemo ya wananchi wetu. Kwa hiyo, hii tuliyokwambia ndiyo mihemo ya Wananchi wa Busega na ndiyo mahitaji ya kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi moja tu ambayo nimeshakuomba kijana wangu huyu Daniel Gagala, Meneja wetu wa wilaya amekaimu zaidi ya miaka miwili, mthibitishe, mimi binafsi nimeshamfanyia vetting, anatosha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni malipo kwa wakandarasi, Waheshimiwa Wabunge hapa wameshachangia juu ya malipo kwa wakandarasi. Kwa kweli kuna wakandarasi wanadai fedha nyingi, wengine wanadai miezi saba na wengine wanadai mwaka na bado hawajalipwa. Tunaomba sana sasa ukae na Wizara ya Fedha, tuwalipe wakandarasi hasa wakandarasi wazawa. Kwa kweli wanateseka na hawa ni wazalendo sana, wakandarasi wazawa hawatozi riba wakicheleweshewa malipo yao, wanakuwa wazalendo. Mheshimiwa Aweso, tunaomba sana mkae na Mheshimiwa Waziri wa Fedha tuweze kuwalipa hawa wakandarasi wazawa ili waweze kufanya kazi wakijua kwamba wana fedha zao. Kwa sababu wengine wana mikopo wanafirisiwa lakini mkiwalipa basi watapeleka mikopo yao na kurejesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule Usukumani tuna msemo mmoja unasema Ukiwa na wakulima wawili mazao yao yakaliwa, mkulima mmoja mazao yake yakaliwa na ng’ombe wa kwake na mkulima mwingine mazao yake yakaliwa na tembo, mwenye hasara zaidi ni yule ambaye mazao yake yameliwa na tembo. Kwa nini? Kwa sababu yeye hatafaidika popote pale lakini huyu ambaye mazao yake yameliwa na ng’ombe, jioni anaweza akakamua maziwa akapata compensation ya mazao yake waliyoliwa kwenye maziwa, namaanisha nini? Wasukuma hapa wanamaanisha kwamba mkandarasi mzawa tukimlipa fedha yake itazunguka hapa hapa Tanzania, ndiyo maana ya misemo hii ya Usukuma. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo, Mheshimiwa Waziri, tunaweza tukawalipa sasa hivi lakini ni lazima tutafute chanzo cha kudumu kwa ajili ya kupata fedha. Wenzangu wameshasema hapa juu ya chanzo, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha mzungumze, atakapokuwa analeta bajeti yake hapa mwezi wa sita basi aje na chanzo kitakachoiongezea fedha Wizara yetu ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna mfuko wa maji, huu mfuko wa maji unatakiwa uongezewe fedha ili kusudi ziende kwenye miradi yetu ya maji. Tunahitaji kuwa na maji na tunahitaji tupate maji kwenye vijiji vyetu hasa kwenye vijiji ambavyo bado havijapata maji. Wewe mwenyewe kwa kauli yako huwa unasema hamna mbadala wa maji na mimi naungana na wewe, hakuna mbadala wa maji, lazima leo tumalize tatizo la maji kwenye vijiji vyetu. Kwa hiyo, tutafute vyanzo tusiathiri wananchi,tuna vyanzo vya Serikali zingine, tunaweza kupunguza kidogo kidogo kwenye sekta zingine, tukaleta kwenye chanzo cha mfuko wa maji ili tuweze kupata fedha nyingi tuwapelekee Watanzania, wawe na maji kwa ajili ya matumizi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo...
(Hapa kengele ililia kiashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)