Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza jioni ya leo. Kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa afya njema na kusimama ndani ya Bunge kwa mara nyingine kujadili na kutoa maoni yangu kwenye Wizara hii, Wizara ya Maji, ambayo ndiyo uhai wa wananchi wetu wa maeneo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa nzuri ambayo ameendelea kuifanya. Kipekee kabisa nachukua nafasi hii kukuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji tufikishie salamu sisi Wananchi wa Rorya, Tarime, tunamshukuru sana kwa Mradi mkubwa wa Maji wa Miji 28 unaoanzia Rorya kwenda Tarime.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka wakati tunaanza mradi huu haukuwemo kwenye bajeti, lakini Mheshimiwa Waziri nilikufuata na ukaniahidi kwamba, acha nizungumze na Mheshimiwa Rais nimuombe miradi minne ambayo itaongezeka kupitia miradi 28, ili angalau na wewe mradi wako Mheshimiwa Mbunge uwepo. Nakushukuru sana kwa sababu, ulitimiza ahadi hiyo na ulivyomuona Mheshimiwa Rais, leo tunajivunia sisi wananchi wa Rorya, Tarime. Mradi wa shilingi bilioni zaidi ya 134 unakwenda kutekelezwa kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee tufikishie salamu hizo, tunamshukuru sana Meshimiwa Rais kwa hiyo kazi kubwa nzuri unayoifanya. Pia, nachukua nafasi hii kukushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa, nzuri, unayoifanya brother. Wewe ni mtu mmoja ambaye kwa namna yoyote tukisema tuseme sifa zako ndani ya Bunge yawezekana tukajikuta tunamaliza dakika hizi zote saba tunakuelezea wewe, lakini tuendelee kukuomba endelea kuwa hivyohivyo, mnyenyekevu na namna ambavyo unashirikiana na Wabunge kutatua changamoto zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachua nafasi hii kukushukuru sana, Mheshimiwa Waziri, na kukupongeza kwa namna unavyoishi na kufanya kazi na watendaji wako wote wa Wizara. Kuanzia Katibu Mkuu, dada yangu Eng. Mwajuma, Mkurugenzi wa RUWASA na wengine wote kwa namna ya ushirikiano na unavyowaweka pamoja katika kutimiza lengo, dhamira na maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakika wewe umedhamiria kubeba maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunakupongeza sana kwa kazi kubwa na nzuri unayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda mimi nina mambo mawili tu ya kushauri leo. Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako ipo miradi ambayo umeitaja na hii ni miradi mikubwa. Pamoja na kwamba, haujaipa jina la miradi ya kimkakati, lakini kwa mtazamo wangu naiona kama ni miradi ya kimkakati. Mradi mmoja wapo ni huu niliousema wa Miji 28 kwa maana ya Rorya, Tarime, ni mradi mkubwa ambao una-involve zaidi ya shilingi bilioni 134, lakini, umesema kuna mradi mkubwa utakaotoa maji Ziwa Viktoria kuleta Dodoma. Kwa sasa wanafanya feasibility study na maana yake ni kwamba, na wenyewe unakwenda kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi umeuzungumzia ambao utatoa maji ziwa Tanganyika na kuyapeleka kwenye Mikoa ya pande hizo kwa maana ya Rukwa na Mikoa mingine. Vilevile kuna mradi wa Busega ambao ameuzungumza Mheshimiwa Mbunge aliyetoka kuchangia hapa asubuhi, lakini kuna Mradi wa Bwawa la Kidunda pamoja na miradi mingi mikubwa ambayo umeitaja kwenye bajeti yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ni mikubwa ukijumlisha fedha zake inawezekana ikagharimu sio chini ya shilingi trilioni moja mpaka shilingi trilioni mbili kuhakikisha kwamba, miradi hii inatekelezwa. Hofu yangu na hapa, ningetamani sana tumsaidie Mheshimiwa Waziri pale ambapo anakuwa na miradi mikubwa, anabeba dhamira na maono ya Mheshimiwa Rais, lakini fedha anayopewa ni ndogo sana. Sasa wasiwasi wangu ni namna ambavyo, kama anakuwa na miradi mikubwa ya zaidi ya trilioni mbili, lakini ana bajeti ya shilingi bilioni 600, tunajiuliza anakwenda kutekelezaje miradi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natamani kushauri mambo yafuatayo; la kwanza...

MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Almas Maige, Taarifa.

MHE. BALOZI DKT. BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongezea hapohapo, sekunde chache tu. Hata ukomo wa bajeti ya mwaka jana iliyopitishwa hapa, ya mwaka huu imeshuka kuliko ya mwaka jana. (Makofi)

MWENYEKITI: Samahani, nilimtamka Mheshimiwa Almas Maige, ni Mheshimiwa Kakurwa.

Naomba Mheshimiwa uendelee. Kwanza unaipokea hiyo Taarifa?

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa hiyo. Nakushukuru sana Dokta kwa kunikumbusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichotamani kumshauri Mheshimiwa Waziri ni nini, ili twende sote kama Bunge na twende kwa maana ya kumshauri kwa dhamira hiyo ya kubeba maono ya Serikali, la kwanza ni, Mheshimiwa Waziri ipambanue hii miradi yote. Ni lazima ukubali kuanzisha kitu kinachoitwa Mpango wa Maji wa Taifa. Mpango huu, Mheshimiwa Waziri, nenda kaainishe miradi yote mikubwa ambayo ndiyo maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais ambayo umeitaja kwenye bajeti yako iingie kama sehemu ya Mpango wa Maji wa Taifa, iainishwe, uisajili, uitengenezee urasimishaji, ili kama Taifa sisi Wabunge wote na wananchi kwa ujumla wake, kama Watanzania, tuwe tuna mipango tunayojua kwenye Sekta ya Maji ni miradi ipi mikubwa inayokwenda kutekelezwa kutatua changamoto yote ya maji nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii mikubwa hatuwezi kuiacha ikabaki kwenye bajeti ile ya shilingi bilioni 600 wakati miradi yenyewe ukiijumlisha inakwenda zaidi ya trilioni mbili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri la kwanza kabisa tengeneza mpango kabambe wa maji wa Taifa, ili angalau wananchi wote, na sisi kama Wabunge, tutakuunga mkono kwa sababu, dhamira uliyonayo ni ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tumuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha aone namna ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri kwa kutafuta vyanzo vya mapato, ili kukidhi na kuratibu miradi hii mikubwa ya kimkakati ambayo Mheshimiwa Waziri ameiainisha. Mimi natamani niende moja kwa moja kupendekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ambalo ninapendekeza ni ningetamani kupitia tozo hii tunayokatwa kwenye mafuta Mheshimiwa Waziri wa Fedha aone namna ya kupunguza baadhi ya maeneo ampelekee Waziri wa Maji fedha hizi, ili aweze kuratibu na kukamilisha miradi hii mikubwa ya kimkakati. Tusisubiri tozo nyingine zaidi ya hii inayokatwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwa kuwa, tayari alikuwa amekata fedha zaidi ya shilingi bilioni 137 kutoka kwenye bajeti ya mwaka jana ameipunguza kuja kwenye bajeti ya mwaka huu, naomba Waziri wa Fedha na Serikali kwa ujumla tumrudishie fedha huyu Waziri, ili aweze kutimiza haya maono na vipaumbele vya Mheshimiwa Rais. Ukipunguza fedha hizi huyu hawezi kutimiza haya malengo. Mwisho matokeo yake tutakuwa tuna miradi mikubwa ya maji ambayo itachukua miaka nenda rudi, wakati miradi hii inatakiwa itekelezwe ndani ya Mwaka 2025/2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa harakaharaka ninayo miradi ambayo Mheshimiwa Waziri ningetamani uishughulikie ndani ya Jimbo langu la Rorya. Tunao Mradi wa Bukura ambao unahudumia kata zaidi ya nne. Tulikwenda mimi na wewe Mheshimiwa Waziri tukaanzisha mradi huu, umesimama haufanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Mradi wa Gabimoli, tunao Mradi wa Komuge, tunao Mradi wa Nyarombo, tunao Mradi wa Bugendi, tunao Mradi wa Ikoma na tunao Mradi wa Sakawa, juzi Jumapili, nilikuwepo pale nafanya mkutano na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri miradi hii unaijua. Mimi mwenyewe kwa upendo kabisa wa Wananchi wa Rorya nilikuchukua ukaenda ukaianzisha kwa kutoa fedha na miradi imeanza, lakini kwa sasa imesimama. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, wananchi hawa wapate fedha, ili miradi iweze kukamilika na kukimbia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni mimi sikitiko langu ni lilelile ambalo naona hawa watu wamepunguziwa zaidi ya shilingi bilioni 137 na wakati hapa walipo Wizara hii inadaiwa na Wakandarasi zaidi ya shilingi bilioni mia mbili plus. Yani leo ukienda kwa Mkurugenzi wa RUWASA ana certificate za malipo za Wakandarasi ambao ni wazawa wa nchi hii zaidi ya shilingi bilioni mia mbili plus. Sasa ukimpunguzia shilingi bilioni 137 bado anatakiwa alipe Wakandarasi ambao wamefanya kazi za wananchi huko chini. Wanatakiwa wakamilishe miradi, ili iweze kutoa maji. Tunakuwa hatumsaidii Waziri na tunakuwa hatuendani na maono ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana fedha hizi ambazo zimekatwa, hizi shilingi bilioni 137 zirudi, ili angalau hawa watu waweze kuwalipa wakandarasi waliotoa huduma kwenye maeneo mengine. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)