Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. Kwanza na mimi naanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa uhai na leo kupata nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Hotuba ya Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya kwenye kutatua changamoto hii ya maji na upatikanaji wake nchini. Pia, nampongeza sana mdogo wangu, rafiki yangu, Mheshimiwa Waziri Aweso pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Kundo, Katibu Mkuu wetu, dada yangu, Mwajuma Waziri pamoja na viongozi wote kwa maana mnaisimamia taasisi yenu na idara zake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siachi kuwapongeza sana watu wangu ninaofanya nao kazi kwa karibu kwa maana ya DAWASA, kaka yangu Kiula Kingu, Mkurugenzi Mtendaji wa DAWASA, na dada yangu Everlasting Lyaro ambaye ni Afisa Mahusiano wa DAWASA. Kwa kweli, umeweza kutuunganisha Wabunge wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu nyingi sana ni kwa Mheshimiwa Rais, nilisema juzi wakati nachangia kwa Waziri Mkuu, kwa sababu ya mambo makubwa ambayo ameyafanya, lakini kwa sababu ya muda nitasema tu kwa haraka kwa kutaja. Ndani ya muda huu wa miaka yake mitatu tayari tumeona ma-tank karibu mawili na jingine jipya linajengwa Tegeta A, lenye ujazo wa lita 6,000,000 ambalo linasaidia Goba yote na maeneo machache ya Mbezi, Mshikamano na Mbezi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, lipo tank la Kitopeni maeneo ya Mbezi, Makabe na sehemu ndogo ya Msumi A. Sasahivi linajengwa tank kubwa la ujazo wa lita 9,000,000 kule Bangulo, Ilala, ambalo litasaidia Kusini yote ya Dar es Salaam kwa hiyo, mimi napongeza sana juhudi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, niseme kidogo juu ya eneo la bajeti. Eneo hili limesemwa na wachangiaji wengi na mimi kwa fani yangu siwezi kupita bila kueleza jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masikitiko sana, sijui kama miradi itakuja kutimia huko mbele, miradi ambayo imeainishwa humu ya zaidi ya trilioni 1.8 hadi mbili dhidi ya bajeti ya shilingi milioni 627 ambayo imepitishwa kwa Mwaka 2024/2025 tofauti na bajeti iliyopita ya Mwaka 2023/2024 ya shilingi bilioni 756.2. Tofauti yake ni shilingi bilioni 128.4 ambayo ni chini kwa asilimia 17, hii siyo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziada sitaki kusema mapungufu hayo kwenye fedha za OC (Other Charges), nizungumzie za maendeleo. Kwa Mwaka 2023/2024 zilitengwa shilingi bilioni 695.83, lakini sasa hivi kwa Mwaka 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 558.1 tofauti ya shilingi bilioni 137.7, amesema Mwenyekiti wakati anaizungumzia Taarifa ya Kamati. Ipo chini kwa asilimia 18, hii ni hatari sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati kwa kukubaliana nayo imetoa mapendekezo na lugha yake imekuwa ngumu kidogo. Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukajikuta tunashindwa kwenda kukubalina na hii bajeti katika kumsaidia Waziri wa Maji, ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, lakini mimi nataka niseme au kuchangia na kuchochea juu ya taarifa ya Kamati. Kupungua huku kwa shilingi bilioni 137 tunashangaa ni kwa nini dhidi ya mpango uliopo ambao ni mzuri kufikia ile asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haiendi bure, tunajua mpango huo pia, umeathiriwa sasa hivi na El-Nino na mvua nyingi. Tunashangaa, hapa palikuwa na maboresho makubwa ya miundombinu dhidi ya kupungua kwa fedha. Je, hiyo miundombinu itarudije? Siyo hivyo tu, ni vizuri tujue kuna faida au ushauri tupate wapi hizi fedha zilizoondoka shilingi bilioni 137?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema Kamati, ni vizuri, moja tunaweza tukaenda kwenye Hati Fungani, wala siyo jambo baya. Tunaweza tukajikuta Watanzania wengi wana fedha wakawekeza na kutapata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limeshauriwa na kamati ni shilingi 50 ya Mfuko wa Maji ikaongezwa au ikabaki palepale, lakini kupunguza gharama nyingine kutoka kwenye zile ambazo tunazitoza sasa hivi, lakini ushauri wa ziada kwenye eneo hilo ni lazima ikumbukwe tuna madeni ya zaidi ya shilingi bilioni 300 ambayo yana-exist hadi sasa hivi na ni lazima yalipwe. Kwa hiyo, kwa kila hali tunatamani Waziri wa Fedha kesho uje na mawazo ya kutafuta fedha nyingine, ili tuzirudishe pale zile shilingi bilioni 137 zilizoondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulizungumza hilo niseme kidogo katika uchimbaji wa visima. Nimefurahi, tungeweza kujiuliza ni kwa nini visima? Swali gumu lingekuwa tunaondoka kwenye majisafi na salama sasa tunarudi kwenye maji ya chumvi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni visima kwa sababu, kama nchi kuna wakati tunaingia kwenye vipindi vigumu vya ukame. Vile visima vinaweza vikatusaidia zile nyakati ambazo hatuna majisafi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwangu nimefurahia sana. Sasa hivi navitaka hivyo visima haraka hata kesho asubuhi vikachimbwe kule Msumi Centre, Msumi Darajani, Mpiji maeneo ya kwa Mvungi, maeneo ya CCM ya zamani na maeneo ya Torino. Vilevile maeneo ya Msingwa Mpakani Kata ya Saranga, maeneo ya Msigani pale Manzese na kwa Mama Nipe ni muhimu sana. Sisi tunavitaka sasahivi visima hivi pamoja na hiyo miradi mizuri ambayo inakuja baada ya mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la kumalizia ombi letu kwa sasa ambalo tuliliomba sana ni mabomba, distribution ya mabomba. Miradi hii tayari ina vifaa vya maji nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ukija kujumuisha hapo naomba useme, nimeona kwenye bajeti yako fedha za ndani shilingi milioni 214 na za nje shilingi bilioni 6 kwenye eneo la kuendeleza miradi ya Dar es Salaam, utoe commitment hapa ili mabomba yapatikane ya aina zote wananchi wapate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Mradi wa Msumi ulieleza hapa swali langu la msingi juzi lilijibiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri bilioni 13.9 zipo, nimeingia kwenye bajeti nakuta bilioni moja kuunganisha chanzo cha Ruvu Juu na Ruvu Chini ukija uniambie 13.9 zinapatikana wapi kwenye bajeti yako?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho ushauri nikuombe ukija hapa uniambie huu mradi unaondelea wa uuzwaji maji kwenye magari ambao nimeeleza humu ndani ni changamoto na ndiyo maana labda wananchi wanafikiri mabomba hatuletewi kukamilisha miradi aliyowekeza bilioni nyingi Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Awamu ya Sita...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja ya taarifa hii au Hotuba wa Wizara ya Maji, ahsante sana. (Makofi)