Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara hii ya Maji pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi ambayo nimeweza kusimama hapa na kuweza kuchangia Hotuba ya Wizara ya Maji. Vilevile nichukue nafasi hii kuwapongeza sana, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii ya Maji pamoja na Mheshimiwa Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri wanazozifanya, mmekuwa ni Mawaziri ambao mpo busy site na majibu na matokeo yanaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile niweze kuwapongeza watendaji wote wa Wizara kuanzia Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu. Vilevile niwapongeze sana watendaji wa RUWASA ambao ni Mamlaka ya Maji Safi vijijini pamoja na usafi wa mazingira, niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnazofanya mkiongoza na Mkurugenzi wa RUWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazozifanya kuhakikisha anamtua mwanamama ndoo kichwani, kuhakikisha maji safi yanapatikana katika nchi yetu. Pamoja na kampeni hiyo ya kumtua mwanamama ndoo kichwani kwa Mkoa wetu wa Tabora, TUWASA wameamua kutuwekea maji ya Mradi wa Ziwa Victoria kwa wilaya zote saba na hivi sasa mkandarasi yupo site anapeleka maji Urambo, Kaliua na Sikonge na tumefika 36%. Ifikapo 2026 mradi huu unatakiwa ukamilike hivyo Wananchi wa Mkoa wetu wa Tabora waweze kuneemeka na maji safi ya Mradi wa Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri hayo yanayoendelea kufanyika nimpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameweza kutoa magari ya kuchimbia visima vya maji kwa kila mkoa na Mkoa wa Tabora ikiwa ni mojawapo ambapo tumepata gari hilo. Vilevile kila jimbo visima vitano kwa ajili ya upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jambo hilo ambalo Mheshimiwa Rais ameona na ametuwezesha Wananchi wote wa Tanzania hususani pia Mkoa wangu wa Tabora, lakini vilevile nipongeze RUWASA Mkoa wa Tabora kwa kazi nzuri wanazofanya, Meneja wa RUWASA na timu nzima ya RUWASA ya Mkoa wangu wa Tabora. Wao waliona waje na miradi ya mabwawa kwa ajili ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora. Pamoja na miradi hiyo ambayo imeshaenda tuna changamoto kubwa sana ya miradi hii kutokukamilika kwa ukosefu wa pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Wilaya ya Urambo tuna Mradi wa Bwawa la Kalemela ambapo pesa zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya bwawa lile kwenye bajeti inayoishia 2023/2024 hakuna pesa iliyoenda mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile watendaji hawa wa RUWASA Mkoa wa Tabora waliona watumie pesa za PforR kuanza ujenzi wa mradi ule wa Bwawa la Kalemela. Kwa hiyo niiombe Serikali iweze kuona namna gani watendaji wetu wanawaza nje ya boksi kuhakikisha maji yanapatikana, kwa sababu Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa ambayo ina changamoto sana ya upatikanaji wa maji chini ya ardhi hasa kwa kuchimba visima, lakini wao wameenda mbali wakawaza zaidi kwa kuja na miradi ya mabwawa lakini bado inashindwa kutekelezeka. Kwa hiyo tatizo la maji kwa Mkoa wa Tabora bado linaendelea kuwa ni tatizo sugu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna Mradi wa Bwawa la Ichemba ambapo mradi huu upo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020 na 2020/2025, lakini mpaka sasa hivi tunavyoongea kinachotekelezeka ni mkataba kusainiwa. Sasa tumebakiza mwaka mmoja au miezi nane kukamilisha awamu hii ya sita lakini bado Bwawa hili la Chemba halijakamilika. Niombe sana Serikali, pia niombe sana RUWASA, kwa magari haya ambayo Mheshimiwa Rais ametoa ambayo yanaenda kuchimba visima vitano kila jimbo hebu tuweze kuangalia majimbo ambayo hayana Miradi ya Maji ya Ziwa Victoria hasa kwa Mkoa wangu wa Tabora, mfano Jimbo la Ulyankulu, Jimbo la Urambo, Jimbo la Kaliua na Jimbo la Sikonge yaweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwaombe pia watoe maelekezo mkoani, gari linapoenda jimbo moja lihakikishe linachimba visima vyote vitano ndipo lihamie wilaya nyingine. Kwa kufanya hivyo itakuwa imerahisishia majimbo ambayo hayana mradi wa maji kuweza kupata maji na wakati wengine wanaendelea kupata maji na kuneemeka kwa maji Mradi wa Ziwa Victoria. ( Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umeisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema naomba niunge mkono hoja.