Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima. Napenda kutoa pole kwa ndugu zangu na jamii yangu ya Mkoa wa Lindi kwa athari za Kimbuga kile cha Hidaya lakini Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa vijana wake wanafanya kazi usiku na mchana na mawasiliano yanaenda kurejea muda si mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati kwa ajili ya kumtua mama ndoo kichwani, tunashukuru sana. Pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri Aweso, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Watendaji wote wa Wizara hii ya Maji na Mameneja wa RUWASA, Meneja wa RUWASA wa Mkoa wa Lindi na mameneja wote wa Wilaya zote za Mkoa wa Lindi, wanafanya kazi nzuri sana kwa ajili ya kuwaletea Wananchi wa Mkoa wa Lindi maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wana-Lindi tunashukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia miradi ya maji mikubwa. Mradi wa kutoa maji kutoa Nyangao kupeleka Ruangwa – Nachingwea bilioni 119.5, si jambo rahisi ni jambo kubwa sana tunashukuru sana, vijiji 54 vinaenda kupata maji. Pia kuna mradi wa maji kutoka Ngapa kwenda Mchinga na sasa hivi tayari pale Mchinga wanapata maji ya bomba, maji safi na salama haijawahi kutokea na mradi ule unaenda mpaka Kilola Mbwani mpaka Kijiweni kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso tunakushukuru sana kwa kutekeleza adhima ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia kuna maji ya kutoka Mto Mavuji bilioni 44 maji yanaenda kupelekwa Nangurukuru, Kivinje, Kilwa Masoko haijapata kutokea, huyo ndiye Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumepokea milioni 400 pale Liwale kwa ajili ya kutoa maji kutoka chanzo cha Turuki kuja Liwale Mjini pamoja na vijiji vyake nalo hilo halijawahi kutokea ndiyo tunayaona sasa hivi kwa Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tunamshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikienda kule Nachingwea naona kuna Mradi kule Naipanga wa bilioni 1.6 na ule pia nawahakikisha ndugu zangu wa Nachingwea kule Naipanga wanaenda kupata maji muda si mrefu, hata Juni, hii haitafika. Sisi Wana-Lindi tunafurahi sana tunashukuru sana kupata maji safi na salama. Naamini kabisa kwa bajeti hii mimi naiunga mkono kabisa ipite kwa asilimia zote ili kuhakikisha Nachingwea na Mkoa wa Lindi kwa ujumla tunapata. Mheshimiwa Aweso anakwenda kumalizia ile miradi ambayo ilikuwa bado haijaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa kupeleka maji Nachingwea, Meneja wa RUWASA ameomba shilingi milioni 670 ili Wananchi wa Ngunichile wapate maji safi ambayo wao tangu misingi ya ulimwengu iumbwe wao wanakunywa maji ya kuokota okota. Tunaenda kushuhudia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaenda kulimaliza hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia maji kutoka kwenye ardhi ya Mkoa wa Lindi hayana ubora ndiyo maana meneja wetu ameomba miradi ya mkakati ya kutoa maji kutoka Rufiji ili kuleta maji Kilwa, Lindi na Ruangwa na kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kuleta Nachingwea, Ruangwa pamoja na Liwale. Tunaomba mikakati ya mradi huo Mheshimiwa Aweso itekelezeke kwa kipindi hiki tunachopoitsha bajeti hii, vinginevyo Wana-Lindi wale wataendelea kunywa maji yenye chumvi. Zaidi ya hayo wananchi wale wa Mkoa wa Lindi wanashukuru kwa miradi kama hii ambayo haijawahi kutokea hata kwa wakati mmoja kupata maji safi na salama ambapo mradi mwingine utaenda kulisha kule Kitomanga na Kilangala ambapo sasa hivi tanki kubwa linajengwa pale maeneo ya Mkwajuni. Hizi zote ni juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru sana Mheshimiwa Aweso na timu yako yote, tunaomba mtuangalie bajeti hii tunaipitisha kwa asilimia zote ili miradi ile ikaendelee kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na Wana-Lindi wanaahidi kura zote kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nashukuru ahsante sana. (Makofi)