Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kuweza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu na kuweza kuchangia katika bajeti hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso pamoja na Naibu Waziri lakini na Watendaji wote wa Wizarani katika Wizara ya Maji. Ninakiri kwamba Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake nzima wanafanya kazi nzuri katika kuhakikisha kwamba Rais Dkt. Samia anatimiza ile azma yake ya kuweza kumtua mwanamke ndoo kichwani. Pongezi sana kwa Mheshimiwa Waziri na timu yako.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nawapongeza? Naipongeza Serikali kwa sababu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukiisikiliza ameonesha kabisa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ilivyoongezeka kutoka 77% Disemba, 2022 hadi kufika wastani wa 79.6% Disemba, 2023 kwa vijijini. Vilevile, tumeweza kuona ongezeko la hali ya upatikanaji wa maji mijini kutoka wastani wa asilimia 88 Disemba, 2022 hadi kufikia wastani wa 90% Disemba, 2023. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi kuamini kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana nia ya dhati ya kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa sababu hata kwenye hotuba ya Waziri pia imejidhihirisha, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ametoa zawadi ya visima 900 ambavyo vitakwenda kwenye Majimbo 180 na kila Jimbo litakwenda kupata visima vitano. Waziri hapa wakati anawasilisha hotuba yake ametueleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazozifanya za kuhakikisha kwamba anataka kumaliza kero ya maji nchini kwetu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sambamba na hilo niwashauri Wizara katika suala zima la geothermically investigation. Kipindi cha nyuma tuliona visima vilikuwa vinachimbwa lakini kipindi cha kiangazi havitoi maji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Aweso na timu yako nakuomba sana muwe waangalifu sana katika suala zima la geothermically investigation ili vile visima ambavyo mnaenda kuchimba kwenye yale maeneo mliyokusudia kuchimba, mchimbe sehemu sahihi ili maji yaweze kupatikana ili azma ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mwanamke ndoo kichwani iweze kukamilika kwa ufanisi na ilete tija kwa wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza kilio cha wananchi katika changamoto za bill za maji. Wananchi wengi walikuwa wanalalamika kwamba wanabambikiwa bill, lakini kwenye hotuba ya Waziri ameeleza kabisa kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara kuongeza kasi ya ufungaji wa hizo dira za malipo ya kabla ya matumizi ya maji hizo pre-paid meter za maji ili wananchi waweze kutatua kero hizo za kubambikiziwa maji. Vilevile kwa kuweka pre-paid meter itatusaidia mashirika na zile taasisi za Serikali ambazo zilikuwa na madeni sugu, madeni makubwa, tunaamini kwamba hii itakwenda kuwa suluhisho la changamoto hizi, changamoto za wananchi kubambikiziwa bill za maji lakini pamoja na wale ambao walikuwa hawalipi maji kwa maksudi itakwenda kuwa mwarobaini wa changamoto hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kwenye zuri hapakosi changamoto, napenda kuishauri Wizara muwe makini sana katika kuangalia ubora wa hizo meter ambazo zitakwenda kufungwa, kwa sababu kinyume cha hapo mtakuja kuiingizia Serikali hasara, na kama itakuwa na urahisi watu ku-temper nazo na kufanya ujanja ujanja mtu akatumia maji hata bila kulipa kabla ya matumizi ya maji. Tunajua Tanzania hii ina mambo mengi na wajanja ni wengi kwa hiyo muwe makini katika kuhakikisha kwamba mnapata meter au mna supply meter ambazo zina ubora na ambazo hazitaweza kuchezewa kwa urahisi na watu ambao hawana nia njema na nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nizungumzie changamoto za miradi ya maji Mkoa wa Njombe. Mkoa wa Njombe kuna mradi wa maji wa Mfumbi Wilaya ya Makete. Mradi huu wa Maji Mfumbi Wilaya ya Makete takribani sasa ni miaka miwili mradi huu haujaanza kufanya kazi. Wananchi wa Makete wanataka kujua nini tatizo? Na mkiangalia thamani ya mradi huu hauzidi hata milioni 700. Tunakuomba wananchi wa Makete uwamalizie kadhia hii ili nao waweze kufurahia matunda ya Chama Cha Mapinduzi kwa kupata maji bora, safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa maji Igando, Kijombe wenye thamani ya bilioni 10.8. Mradi huu wa maji wa Igando Kijombe uko ndani ya Jimbo la Wanging’ombe, mradi huu Mkandarasi amekabidhiwa kazi tangu Septemba, 2023 lakini mpaka ninavyozungumza hivi sasa bado Mkandarasi hajaanza kazi. Mheshimiwa Waziri tunaomba mzingatie pia Mkandarasi aanze kazi na wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine tena wa kujenga mtambo wa kusafisha maji chanzo cha Mbugwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iangalie namna ya mradi huu kuweza kuanza kufanya kazi kwa sababu Mkandarasi amepewa kazi tangu Oktoba, 2023.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)