Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa muda na mimi niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa pongezi kwako Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara ya Maji. Naiona dhamira yenu kama Wizara na Watendaji wa Wizara hii kuhakikisha miradi yote mliyonayo na watanzania wote waweze kupata maji safi na salama ya kunywa.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana sote kwamba changamoto uliyonayo Mheshimiwa Aweso pamoja na dhamira hiyo uliyonayo hela hazipo, kwa kudhihirisha hilo ni kwamba safari hii badala ya Wizara kupanda ili tuende tukapate maji kwa watanzania na miradi mingi iweze kutekelezeka Wizara imepunguziwa bajeti na sasa hapa napata kizungumkuti, hii miradi iliyopo ambayo haikukamilika na miradi inayokuja tunakwenda kuikamilisha kwa namna gani kama bajeti inashuka? Serikali watanisaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, naomba nizungumzie suala la uhaba wa maji kwenye Mkoa wa Dodoma. Tumekuwa tukizungumza Ofisini, Bungeni, Katibu Mkuu na Watendaji wako. Mheshimiwa Waziri, tunaomba Dodoma muiangalie kwa jicho la kipekee, pamoja na ukame wake lakini bado tuna maji chini ya ardhi. Leo kati ya Mikoa ambayo ipo chini kwenye suala zima la maji ni Mkoa wa Dodoma na kwa Mkoa wa Dodoma, watu ambao wako chini kwenye suala la upatikanaji wa maji ambao na wewe ulifika ni Wilaya ya Chemba. Mheshimiwa Waziri umeenda kwenye vijiji viwili wamama wakakulilia wakakwambia Mheshimiwa Waziri tusaidieni maji, tunaombeni maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi na wanawake ambao ni mama zetu, dada zetu, shangazi zetu na bibi zetu wa Wilaya ya Chemba tunafukua maji kwenye mito ya mchanga, leo mvua ikiisha mwezi wa tisa wa kumi yale maji yamekauka pale ardhini kwenye mito hawa watu hawapati maji. Mmekuwa mkitupa miradi ambayo haitekelezeki Mheshimiwa Waziri. Kuna visima kumi mlitupa 2022 imepita kavu, 2023 imepita kavu. Tunashukuru tumeona sasa hivi umetuingiza P4R - pay for results. Tunashukuru mmetupa, lakini umetupa miradi saba tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba utuangalie Wilaya ya Chemba hali ya ukame ni ngumu. Mheshimiwa Waziri, nikuombe kutoka hiyo miradi saba uliyotupa tunakushukuru na wewe una msemo kwamba asiyeshukuru kwa kidogo hata kikubwa hawezi kushukuru. Sisi hicho kidogo tunakushukuru, ahsante lakini tunaomba utuongezee miradi hali ni ngumu. Tegemeo letu ilikuwa ni mradi wa Farkwa. Mradi wa Farkwa haueleweki Mheshimiwa Waziri hata wewe mwenyewe kwenye hotuba yako umesema maneno mengi, lakini hitimisho lako Mkandarasi atakapopatikana, lini? Lini tunampata Mheshimiwa Waziri? Kwa hiyo, nikuombe miradi ya P4R ambayo tunaamini inaweza kutuokoa tusaidie tuongezee miradi angalau tufike hata 20, tunakuomba angalau ifike 20 na ukija hapa uwaambie wananchi wa Chemba angalau tutawapa hiyo miradi kutoka hiyo saba ifike 20. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunashukuru mradi wa miji 28 sisi pia ni wanufaika na ulisema. Pia kumekuwa na changamoto kidogo, walikuwa wanasuasua tunashukuru sasa hivi mkandarasi yuko site na kazi anafanya. Nina ushauri kwenye huu mradi, kulikuwa na uchimbaji wa visima kwenye maeno mbalimbali ili tuweze kuchimba kisima kujenga tenki na kusambaza kwenye eneo husika, lakini wameenda pale Chambalo wamechimba kisima kimedumbukia, lakini wameenda pale Paranga mpaka sasa wameshachimba visima viwili ambavyo vina maji mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachotamani kushauri kwenye mradi huu, niombe yule mkandarasi waendelee kuchimba maji pale kama yanaweza kupatikana, tupate hata visima vinne tujenge tenki kubwa pale Chemba Mjini ili sasa maji yale yasambazwe kwenda Chambalo, yasambazwe na kwenda Gwandi badala ya kwenda kuchimba hivyo visima kwenye kila Kijiji. Kwa hiyo, ninaomba muone ni namna gani mkandarasi mnampa maelekezo ili aweze kufanya hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa natamani kulisema ni suala zima la mitambo ambayo tuko nayo. Tunaomba ile mitambo mitano iliyokuja ya uchimbaji wa mabwawa lakini na mitambo ya kuchimba visima, RUWASA Mkoa wa Dodoma, tunaomba hilo gari lianze kwa Wilaya ya Chemba hali ni mbaya, maisha ya wanawake wa Wilaya ya Chemba, wakina mama ikifika mwezi wa tisa wanafukuzana kwenye milima kwenda kutafuta maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri ni suala zima la wakandarasi wetu. Wakandarasi wetu wa ndani wanafanya kazi kubwa sana na ndiyo wasaidizi na waokozi ndani ya Taifa letu, lakini kumekuwa na changamoto ya malipo yao. Kwa nini hao watu wanafanya kazi hamtaki kuwalipa? Serikali kuna shida gani? Awali mlisema fedha zinatumiwa vibaya kwa hiyo mkandarasi afanye a-raise certificate ipelekwe, wamepeleka certificate, watu wana miezi sita, watu wana miaka miwili, wengine wanauziwa nyumba, watu wanakufa, watu wanafanyaje, tunaomba hela za wakandarasi zilipwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi hawa watu hawadai hata ile fedha ya kucheleweshewa miradi yao, wakidai mnawaambia sio wazalendo na wakiomba miradi mnawanyima eti kwa sababu wamedai fee charge ya ucheleweshaji wa kulipwa fedha, lakini tukiangalia wakandarasi wa nje mnawalipa, sasa kwa nini watu hawa tunawafanyia namna hiyo? Hawa ni wa kwetu hawa watu fedha yao, na ukiangalia Mheshimiwa Waziri wakandarasi wa nje wanaokuja kufanya kazi hapa nchini kwetu tunawapenda na tunatamani watufanyie kazi, wakija kwenye mikataba yetu tunasaini mikataba mafundi wao kila kitu ni cha kwao mpaka mabomba na kila kitu wanaleta wao, wanachochukua kwetu ni vibarua tu ambao wanawalipa shilingi elfu tatu kwa siku, lakini huyu mkandarasi wa hapa kila kitu atanunua hapa ndani, tutakusanya kodi kwa wakandarasi wetu lakini kwa nini tunawafanyia haya yote? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba uwasaidie wakandarasi wetu ambao wame-raise certificate ziko Wizarani kwenu ama ziko Wizara ya Fedha, tunaomba muwasaidie wapate hizo fedha ili waweze kukamilisha miradi wananchi wetu wapate maji safi na salama, pili kodi iweze kulipwa kwa wakati nchi yetu iweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. (Makofi)