Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuku kwa nafasi hii na mimi kuchangia kwenye Wizara hii ya Maji. Pia nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima na kwamba tunaweza kuwatumikia wananchi hasa wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa adhma yake ya kumtua mama ndoo kichwani. Hii siyo kazi ndogo, tumeona ripoti sasa hivi tunafikia upatikanaji wa maji wa asilimia 79.6 kwa watu wa vijijini na asilimia zaidi ya 90 kwa watu wa mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kazi kubwa ambayo ameifanya, ninaamini kwa miradi mingi ambayo bado inaendelea iko kwenye hatua mbalimbali, baada ya kukamilika ni imani yangu kabisa kabla ya uchaguzi wa mwakani, mama atakuwa amefikisha ile asilimia ambayo imeahidiwa kwenye Ilani ya chama chetu, 85% vijijini na 95% mjini, hiyo ni imani yangu, miradi mingi mikubwa imetekelezwa tunampongeza sana Rais wetu kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi siwezi kuelezea miradi yote. Kila Mbunge kwenye Mikoa yao na Wilaya zao watakuwa wanaelezea miradi huko angalau mimi nitaje michache kwenye Mkoa wangu lakini hasa kwenye Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna miradi yetu mikubwa miwili, hii ilikuwa kichefuchefu muda mrefu, lakini tumshukuru Rais wetu wa Awamu ya Sita, kipindi chake ameweza kuikwamua miradi hii miwili mikubwa. Nikizungumzia mradi mkubwa ule wa Mwanga, Same na Korogwe lakini mradi wa miji 28. Miradi hii ilikuwa kero kubwa Watanzania walikuwa wakipigia kelele lakini tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kufanikisha kuleta fedha na miradi ile sasa hivi iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa hiyo, ninampongeza Rais wangu Mama Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia pia nitumie fursa hii niwapongeze ndugu zangu viongozi wa Wizara hii. Moja, Kaka yangu Jumaa Hamid Aweso kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Ndugu huyu ni msikivu, mchapakazi lakini ni mcha Mungu na anashirikiana kwa asilimia kubwa sana na Wabunge ndiyo maana anaendelea kufanikiwa siku hadi siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza aliyekuwa Naibu Waziri dada yetu Engineer MaryPrisca Mahundi kwa kazi kubwa ambayo ameifanya, nimshukuru na kumpongeza Engineer Kundo amepokea kijiti na anakimbia nacho kwa speed kubwa sana. Kwa hiyo, nimpongeze kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Kipekee kabisa nimpongeze Katibu Mkuu Eng. Mwajuma Waziri, wakati akiwa Naibu Katibu Mkuu kafanya kazi kubwa, sasa hivi ni Katibu Mkuu anaendelea kupambana kuhakikisha anaendelea kumsaidia Mama Samia Suluhu Hassan ili kumtua Mama ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Jimbo langu, wakati nachukua nafasi hii ya Ubunge upatikanaji wa maji kwenye Jimbo langu ulikuwa ni chini ya 43%, ilikuwa kila nikiongea Bungeni ilikuwa ni kulia kulalamika kumuomba Waziri Aweso aniokoe kwenye Jimbo la Korogwe Mjini, lakini namshukuru Mungu nimshukuru Rais pamoja na Waziri wangu Jumaa Hamid Aweso, Sasa hivi upatikanaji wa maji kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini ni zaidi ya 84%. Hebu chukulia kuanzia 43% sasa hivi ni 84% kwa hiyo ninakupongeza sana na ninakushukuru Kaka yangu kwa kunitendea mambo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nisiache kuwapongeza MD wetu wa Idara ya Maji kule Korogwe, Ndugu yangu Yohana Mgaza, Meneja wa HTM lakini na Wiliam Tupa Meneja wa RUWASA kwa namna wanavyoendelea kutupa ushirikiano kutusaidia kwenye kutatua changamoto ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kabisa kwa miradi ambayo inaendelea kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini baada ya mwaka huu upatikanaji wa maji utakuwa ni zaidi ya asilimia mia moja kwenye Jimbo la Korogwe Mjini kwa sababu tunao mradi wa miji 28 pia mradi wangu mkubwa unaitwa Mradi wa Ndemaa. Hii miradi ikikamilika nina uhakika kabisa upatikanaji wa maji kwenye Jimbo la Korogwe Mjini utakuwa ni zaidi ya asilimia mia moja. Hivyo namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maombi machache ninadhani muda wangu bado, ombi la kwanza, hatuna treatment plant kabisa kwenye Mji wetu wa Korogwe Mjini, wakati wa mvua maji yakichafuka kwenye vyanzo yanakuja nyumbani jinsi yalivyo. Tunashukuru umetutendea mambo makubwa sana. Upatikanaji wa maji umekuwa mkubwa sana, lakini tunaomba utusaidie tupate treatment plant ili maji yanayoingia majumbani yawe maji mazuri.
Mheshimiwa Waziri, kwenye Kata za pembezoni mwa Jimbo langu la Korogwe Mjini bado miundombinu, network za mabomba bado haijafika kwenye Kata za Mtonga, Kilole na baadhi ya Kata ambazo ziko pembezoni, miundombinu bado haijafika. Kwa hiyo tunaomba utusaidie kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tenki letu dogo kwenye Kata ya Mgombezi kwenye Kijiji cha Mgambo, tenki hilo limejengwa miaka mitatu iliyopita lakini hadi sasa hivi hatujapatiwa pump ya kuweza kuchukua maji kuyapeleka kwenye tenki hilo. Naamini meneja wetu wa HTM analimudu hili ni kumpigia tu simu apelike ile pump. Juzi nilikuwa kwenye ziara katika Kijiji hicho, wakatuomba sana, nimeona niliongee hili, ninaamini watalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitumie fursa hii kukushukuru sana na kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)