Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Santiel Eric Kirumba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amepambana kwa kipindi chote tangu alipokuwa Makamu mpaka amekuwa Rais kwa agenda hii ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza na amewekeza kwenye Sekta ya Maji kwa kiasi kikubwa sana. Mpaka sasa tunavyoongea takribani wakazi milioni nne Tanzania nzima wanapata maji safi na salama. Hili halikuwezekana katika kipindi cha nyuma lakini chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, maji yameweza kufika kwa haraka na amekuwa akitia jitihada za haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wenyewe mnaelewa agenda ya kumtua mama ndoo kichwani ni kitu kikubwa sana na muhimu sana. Kwa sababu gani? Mwanamke anaweza akatumia masaa matatu hadi manne anakwenda kutafuta maji, shughuli za kiuchumi kwake zinakwama. Pia, hata wale watoto wetu wadogo wa kike waliokuwa wanakwenda kuchota maji walikuwa wanapitia ukatili wa kijinsia, wanabakwa na wengine kupelekea kupata mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii agenda ya kumtua mwanamke ndoo kichwani ni agenda kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais. Pia, anapokwenda kuitekeleza kwa namna moja au nyingine inakwenda hata kupunguza ukatili wa kijinsia kwenye Mkoa wetu wa Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nipende kumpongeza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, Dada Juliet. Mheshimiwa Waziri nakuomba unapokaa na unapofanya mambo yako huyu dada mtazame kwa jicho lingine. Huyu dada anaendana na kasi ya Mheshimiwa Rais. Kwenye bajeti iliyopita mlimuwekea hela takribani shilingi bilioni 28. Dada huyu aliweza kujenga visima, matenki na pesa zikaweza kubaki. Huyu ni mfano mmoja wa meneja ambaye anaendana na kasi ya Mheshimiwa Rais. Vilevile, kazi zake nyingi zimekuwa zikienda na kuisha kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipende kuwapongeza Wizara, Mheshimiwa Jumaa Aweso na timu nzima kwa kuweza kupata tuzo duniani kwa mara ya pili mfululizo kwa kuweza kufikisha maji vijijini. Pia, hiyo imewapelekea hata World Bank kuwaongezea pesa za PforR kutoka dola milioni 330 mpaka milioni 650. Hii kwa namna moja ama nyingine Serikali hii imekuwa ikitekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kishindo na imekuwa ikionekana kama mfano kwa nchi nyingine duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi 50 Nchi ya Tanzania ndiyo imeweza kupata tuzo kwa miaka miwili mfululizo na hii yote imekuwa ni chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna anavyoendelea kufanya kazi kwa kuweza kutuletea maji ya Ziwa Victoria. Maji ya Ziwa Victoria yalikuwa ni story kila siku na wapinzani ndiyo walikuwa wanaitumia kama agenda kwamba, tuna maziwa lakini maji hayafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa Mkoa wangu wa Shinyanga, tumeweza kupata maji ya Ziwa Victoria. Ule Mradi mkubwa wa Tinde ambao unapelekea maji Tabora – Shelui na mwisho yale maji yatakuja kufika Dodoma. Ule Mradi ni baadhi ya miradi mikubwa sana kwa East Africa ambao umetekelezwa kwa takribani shilingi bilioni 640. Sisi kwa Mkoa wa Shinyanga Kata ya Tinde ni wanufaika wa ule Mradi mkubwa wa Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ule Mradi kwa Tinde tu umeweza kukidhi vijiji 23. Licha ya hivyo, kwa mwaka wa fedha uliopita Mheshimiwa Aweso amejitahidi sana kututendea haki. Tumeweza kupata maji ya Ziwa Victoria kutoka Nduku – Busangi ambao umetekelezwa kwa shilingi bilioni tano. Vilevile tumeweza kupata katika Kijiji kingine cha Igaga – Lagana shilingi bilioni sita, Zongombela – Kahama tumepata shilingi bilioni 1.5, Tinde – Tabora – Shelui ambao huo ndio Mradi mkubwa wa shilingi bilioni 640. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ambayo mpaka sasa hivi tunaongelea na nina imani kwenye hii bajeti yako Mheshimiwa Aweso umetenga fedha ambayo bado inaendelea na inakuhitaji sana kwa sababu kwetu hii bado ni changamoto kubwa sana. Kuna Chona – Ubabwe ambayo umeiahidi kwenye bajeti hii utaikamilisha, Seseko, Masengwa na Kagongwa. Hizo ni sehemu ambazo ni kubwa na zina mkusanyiko mkubwa wa watu lakini zina changamoto ya maji. Mheshimiwa Aweso, nakuomba sana hii ukaitekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashukuru kwa ambavyo mmeweza kutupatia mabwawa ambayo yanapatikana Shinyanya na Ngofila- Kishapu. Mheshimiwa Aweso, nikupongeze kwa jinsi ambavyo unafanya kazi na timu yako nzima na yule Dada yangu Katibu Mkuu ambaye amechaguliwa binti mdogo. Hii yote inaonesha Mheshimiwa Rais ana imani na vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine cha mwisho, napenda tena kuwapongeza kwa kutuletea visima kwenye kila jimbo kwa Mkoa wa Shinyanga. Majimbo yetu sita yameweza kupata visima vitano vitano. Hii inaonesha Mheshimiwa Rais ana nia ya dhati ya kila Mbunge aweze kurudi. Ni wakati wetu sisi kujitoa na kwenda site ili kuhakikisha kuwa utekelezaji huu unawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu haya maneno ya pesa za UVIKO yalisemwa sana lakini sasa hivi unaona kwa jinsi gani zile fedha za UVIKO mpaka sasa zimeendelea kutumika na ndiyo zimeweza kuleta mitambo hii. Kwa hiyo, nipende kumpongeza Mheshimiwa Rais, Wizara nzima na kila mtu pamoja na timu nzima ya Wizara ya maji. Mheshimiwa Aweso unaonesha utulivu wa hali ya juu. Hiyo inaonesha wewe balozi mzuri wa afya ya akili. Ukianzia nyumbani umekuja na timu nzima ya familia yako. Wewe inaonesha kwamba umetulia kuanzia nyumbani, unapata utulivu hadi kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)