Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata fursa hii. Pia napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ya jioni hii ya leo kupata nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika Wizara hii ni Mjumbe wa Kamati, kwa hiyo moja kwa moja ninaunga mkono hoja ya Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya hasa kwenye upatikanaji wa maji kwenye maeneo yetu. Mwaka 2022 Mheshimiwa Rais alikuja kuweka jiwe la msingi kwenye Halmashauri yetu ya Mji wa Bunda kwenye mradi mkubwa wa thamani ya shilingi bilioni 10.6 na leo mradi huu umeshakamilika kwa 100%. Kwa hiyo kilichobaki ni kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji, ndugu yangu Aweso kumwalika Mheshimiwa Rais aje kuzindua mradi ule kwa sababu umekamilika. Fedha zile ambazo tulipewa katika utekelezaji wa mradi ule zilitumika vizuri zikabaki tukanunua na gari yenye crane kwa ajili ya kusaidia kubeba mabomba katika mradi huo. Kwa hiyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya hasa katika Jimbo la Bunda Mjini kwenye suala la upatikanaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi mkubwa mwingine wa usambazaji wa maji Misisi Zanzibar ambao juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja kuweka jiwe la msingi na hiyo kazi inaendelea. Tuna mradi mkubwa pia wa usambazaji wa maji Manyamanyama na Mgaja na kazi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumshukuru wewe Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa ujumla kwa kazi kubwa ambayo mnaendelea kuifanya katika Halmashauri yetu ya Mji wa Bunda kwa suala la upatikanaji wa maji. Kwa hiyo kazi kubwa imefanyika kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mimi naingia kwenye nafasi yangu mwaka 2021 mwanzoni upatikanaji wa maji kwenye Halmashauri ya Mji wa Bunda ilikuwa ni kiasi cha chini sana, na maji yaliyokuwa yanapatikana pale yalikuwa ni maji ambayo hayakuwa katika kiwango ambacho kinatakiwa; lakini leo wananchi wa Bunda Mjini wanapata maji safi, salama na yenye uhakika. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana kila sababu ya kuja kuuzindua mradi ule kwa sababu umekamilika na wananchi wanapata maji vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati kwenye Wizara hii. Wizara ya Maji inashughulika na maji lakini Wizara ya Mifugo pia nayo katika bajeti unakuta kuna maji mle ndani kwa sababu inaweza ikatengeneza mabwawa kwa ajili ya wafugaji kunywesha mifugo yao. Wizara ya Kilimo pia nayo kwenye bajeti yake utakuta inatengeneza bajeti ikiwa inatarajia kuchimba Malambo kwa ajili ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mbunge nikasema kwamba wizara hizi tatu zikiunganisha bajeti hizi za mabwawa, bwawa lile ambalo wamelenga Kwenda kulichimba katika Halmashauri ya Mji wa Bunda. Wizara ya Maji inachimba, Wizara ya Kilimo inachimba, Wizara ya Mifugo inachimba kwenye eno hilohilo, likaunganishwa bwawa hilo likawa bwawa moja, bwawa kubwa toshelezi ambalo likichimbwa likawekwa vizuri litakidhi mahitaji yote ya Wizara hizo zote tatu, wafugaji watanywesha, wakulima watafanya kilimo cha umwagiliaji na wananchi watatumia maji kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mimi nakua nilikuta kuna lambo moja tu kubwa ambalo lipo kwenye Kijiji cha Bitalaburu ambalo lilikuwa linaweza kubeba maji kwa kiasi kikubwa na likuwa linatumika katika mahitaji haya yote matatu na wananchi wakawa wanatumia vizuri na kwa muda mrefu. Leo ukija kuangalia mabwawa yetu yanayochimbwa madogo halafu hayatoshelezi, wakati mwingine unakuta ndani ya muda mfupi yale mabwawa yamekauka. Niliona lile Bwawa la Bitalabulu lilikuwa linaweza kuchukua muda mrefu sana; na katika umri wangu mimi nilifikiri kwamba ni ziwa, kumbe ni lambo tu limechimbwa katika viwango ambavyo vinatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Maji kwa sababu inashughulika na maji, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo wakiunganisha jambo hili kwenye eneo moja watatatua changamoto zote za wananchi kwenye maeneo hayo. Wizara ya Maji katika kuhudumia wananchi wake inaweza kutatua maji kwa kupeleka usambazaji wa maji kwa mabomba, pale ambapo mabomba hayafiki Wizara inachimba visima na pale ambapo visima haviwezekani Wizara inachimba Malambo. Hiyo yote ni Wizara ya Maji inatatua changamoto za maji kwa wananchi wetu. Kwa hiyo mimi kama Mjumbe wa Kamati kwenye Kamati hii nilikuwa napenda kushauri hili, kwamba Wizara ilifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao kama Mawaziri kwenye Wizara hizi, na wote ni Mawaziri vijana wanaweza wakakaa, wakakubaliana kutengeneza kitu kimoja chenye mvuto mkubwa na manufaa makubwa kwa wananchi. Kwa sababu wakichimba lambo ambalo litakidhi mahitaji yote hayo kwa wakati mmoja wanachi watalifurahia kwa sababu ni vitu ambavyo vimekuwapo huko nyuma tukiviona vinafanyika na vinawasaidia wananchi kwa muda mrefu. Kwa hiyo nimuombe sana Waheshimiwa Mawaziri wa wizara hizi washirikiane ili wakubaliane nalo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nje na hapo tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya, kwa sababu hata kwenye mradi wetu ule wa Lubana, Mwizani wananchi wetu wa kwenda kule Mihale watapata maji kwa sababu shughuli inaendelea. Pia tuna mradi mkubwa pale wa maji taka na maji safi ambao bado unaendelea na kazi inafanyika. Kwa hiyo nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimuombe sana, kwamba yule Mkurugenzi wangu wa maji aliyeko pale asimtoe kwa sasa, amwache ili kwamba hiki alichokianzisha akikamilishe. Kwa taratibu ambazo mimi nimewahi kuziona wakati mwingine mtu mwingine akija akakuta mwenzake alikuwa ameshafanya vizuri akiingia pale yeye anaona apeleke njia nyingine, kwa hiyo inaweza kusababisha ile miradi mikubwa ambayo sasa hivi tunaitekeleza akaja mtu mwingine miradi hii ikaishia njiani kabla ya kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi jambo hili ili tufanye kazi na yule mama kwenye eneo lile ili tuendelee kutatua changamoto kubwa ya wananchi wetu wa Jimbo la Bunda Mjini kwenye changamoto zetu hizi za maji. Kwa kipindi hiki ambacho bado tupo naye, na Mheshimiwa Waziri mwenyewe akiwepo kwenye Wizara hii naamini kwamba tatizo kubwa la maji katika Halmashauri ya Mji wa Bunda litapungua kama ambavyo amekuja yeye mwenyewe akashuhudia kipindi kile ambacho amekuja kuzindua Mradi ule wa Misisi Zanzibar Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)