Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia rehema, lakini pili nianze kwa kutumia nafasi hii kumpogeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni kwa nini? Ni kwa sababu kila Mbunge aliyesimama hapa anakiri kwamba Mheshimiwa Rais ametekeleza kwa vitendo nia yake ya kumtua mama ndoo kichwani. Kwa hiyo na mimi nina kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi tunatambua mwaka jana alivyoona kuna adha sana ya maji vijijini Mheshimiwa Rais alinunua mitambo akapeleka mikoani kwa ajili ya kuchimba visima na mabwawa. Tuliona kwamba kuna visima 283 vilichimbwa na mabwawa 12 na hiyo kazi inaendelea. Kwa hiyo naomba nimpongeze na Watanzania wote tuna kila sababu ya kumpongeza. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri wa Maji kaka yangu Aweso. Sasa kwa vile anajuaga mihemo ya wagonjwa sasa sijui atakuwa daktari, lakini pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye bajeti. Pamoja na kazi nzuri ya kaka yangu Mheshimiwa Waziri ukiangalia bajeti aliyoiwasilisha leo, ukifanya ulinganisho bajeti ya mwaka 2022/2023 aliomba bilioni 709.4, mwaka 2023/2024 bilioni 695.8 mwaka huu ametuletea maomba ya bilioni 627.7 ambayo kila Mbunge hapa ameona kuna upungufu wa bilioni 137.7
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najielekeza kwenye baadhi ya kazi alizoziainisha kwa mwaka huu wa fedha. Kwenye kazi alizoziainisha kwa mwaka 2024/2025 kwenye ukurasa wa 53 amesema Wizara pamoja na mambo mengine itafanya kazi ya kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea na ujenzi wa miradi mikubwa, lakini kazi nyingine ni kupeleka huduma ya maji kwenye vijiji. Sasa hapa ndipo ninapoona mzigo mzito alionao Mheshimiwa Waziri. Kwa nini? Kwa sababu pamoja na kwamba Wabunge wamesema hapa miradi imetekelezwa lakini kuna madeni ambayo yanapaswa kulipwa na Serikali ili Wizara iweze kutekeleza kazi ilizojipangia kwa mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda wala sitakuwa ninakwenda maeneo mengi, lakini niombe hili, kwamba Serikali iiwezeshe Wizara ya Maji kulipa madeni takribani bilioni 300, ama ninaweza kusema bilioni 300 na zaidi ambayo wakandarasi mbalimbali wamewasilisha hati ama kwa kizungu mnasema certificate sjui. Hizo ambazo zimeshawasilishwa ni vema zikalipwa kabla mwaka huu wa fedha uliopo sasa hatujaumaliza ili kuiwezesha Wizara kwa fedha milioni 627 ambayo imeombwa pungufu ya mwaka jana kutekeleza kazi zake ilizojipangia. Vinginevyo hizi fedha zitakwenda kulipa madeni haya ya nyuma na sjui watalipa kwa vifungu gani, kwa sababu madeni kama wana bilioni 300 na zaidi na hapa kuna miradi ameionyesha itatekelezwa atalipaje. Kwa hiyo mimi niiombe Serikali ilipe haya madeni ya nyuma ili kuiwezesha Wizara itekeleze kazi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala sipaswi kufanya rejea majimbo mengine ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kule kwetu Mtwara tulibahatika kupata miradi mikubwa. Mradi wa Makonde wenye thamani ya bilioni 84.7 una hati mbili umewasilisha, moja bilioni moja lakini mwingine bilioni mbili na hela, kadhaa jumla ni bilioni 3.5. Hizo hazijalipwa hata senti. Pia kuna miradi ya RUWASA, pamoja na utendaji mzuri wa Meneja wa RUWASA Mkoa na mameneja wa wilaya una-certificate takribani bilioni nne hazijalipwa hata senti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa pale Mtwara Mjini wa kuboresha miundombinu wenye thamani ya shilingi bilioni 19.7; umepelekwa hati lakini haujalipwa. Tuna mradi wa Mnyawi, Mtwara Vijijini bilioni 5.6, certificate imepelekwa miezi tisa iliyopita lakini haijalipwa hata advance payment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge, na kwa kweli nisipopata majibu ya kuridhisha, na hapa wala siamini kama Mheshimiwa Aweso anaweza akanijibu kwa sababu yeye ndiye anayeomba watu walipwe; kwa hiyo, yeye hana hela.
Naiomba Serikali na nilikuwa naangalia nadhani Wizara sahihi ya kutuletea hizi fedha ni Wizara ya Fedha, ilipe hizi fedha na mimi nitashika shilingi, nitaanza na Wizara ya Maji lakini nitaendelea na Wizara ya Fedha kama sitapata majibu ya kuridhisha kuhusiana na madeni mbalimbali ambayo Wizara ya Maji inadai ili tupate ahueni kwa utekelezaji wa miradi iliyopangwa kwa mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuanza kutekeleza mkakati wa Gridi ya Taifa ya Maji ambapo Kamati imekuwa ikilisema kila wakati lakini nimeona kwenye hotuba na nimesikiliza pia kwamba mmeanza kutekeleza huu mkakati. Tumeona maji ya kutoka Ziwa Victoria kuja huku ukanda wa kati lakini naomba sana Wizara iharakishe utekelezaji wa hii Gridi ya Taifa ya Maji kwa kuyapata maji kutoka Mto Ruvuma kwenda Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi wa shilingi bilioni 38 wa Mto Ruvuma kwenda Mangaka umeanza lakini ndiyo hizo certificate haziijalipwa, naomba mharakishe. Lakini pia kuyatoa maji kutoka Ziwa Nyasa kwenda Mkoa wa Lindi, Mtwara pamoja na Ruvuma yenyewe lakini kuyatoa maji Mto Rufiji na maeneo mengine ambayo mmeyaainisha kwenye hotuba. Hili kwa kweli tutaomba uharakishe ili kutekeleza hilo agizo la kamati na maoni ya Wabunge wengi ili tuwe na Gridi ya Taifa ya Maji, ni kengele ya pili?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba niombe niunge mkono hoja lakini niseme kabisa nia yangu ya kushika shilingi iwapo Serikali haitatueleza kwa kinaga ubaga kwamba italipaje madeni ya maji ili sasa Mheshimiwa Waziri wa Maji aweze kutekeleza miradi aliyoipanga. (Makofi)