Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji. Kwanza, niunge mkono hoja, pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Aweso na timu yote ya Wizara Naibu, Katibu Mkuu pamoja na Meneja wa Maji Mkoa wa Rukwa Ndg. Boaz pamoja na Wilaya ya Nkasi kwa sababu wanatupa ushirikiano mkubwa sana; nasema hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya uboreshaji wa miundombinu ya maji nchini ikiwa ni pamoja na Jimbo la Nkasi kusini. Kwanza, nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wa Jimbo la Nkasi Kusini kwa kupatwa na mafuriko Kata nne; Kata ya Wampembe, Kata ya Ninde, Kata ya Kizumbi na Kata ya Kala, timu ya wataalam ukijumlisha Mkuu wa Wilaya na viongozi wote wa wilaya wanaenda kutathmini tuone namna ya kuwasaidia walioathirika na mafuriko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe nafasi hii kuwatoa hofu wavuvi wa Jimbo la Nkasi Kusini na Mkoa wa Rukwa hasa suala la kupumzisha ziwa, wenyewe wanajua mtu yeyote haruhusiwi kuingia. Hata mvuvi yule wa ndoano wanaona kama hata kitoweo cha familia watakikosa lakini uvuvi wa ndoano kitoweo cha kwenda kula na familia unaruhusiwa, hii ni Serikali Sikivu ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Nkasi Kusini lina changamoto kubwa sana ya maji hasa baadhi ya miradi iliyokuwepo imesuasua kwa muda mrefu. Ukianza na mradi wa Isale ambao una miaka 11 toka uanze lakini mpaka sasa hivi haujaisha. Mheshimiwa Waziri nikuombe utakapokuja kuhitimisha Hotuba yako ya Bajeti ya Wizara ya Maji uwahakikishie wananchi wa Jimbo la Nkasi Kusini huu mradi wa Isale ambao utanufaisha Kijiji cha Mkata, Nkukwe, Temba, China, Kitosi, Ifundwa, Ntuchi na Chenje unakwisha lini? Huu mradi wameusubiri kwa muda mrefu. Vijiji vimeteseka sana kwa kukosa maji. Mabomba yamewekwa pale lakini matumaini ya maji hawayaoni kwa sababu kulikuwa na changamoto ya mkandarasi nadhani kesi imeshaisha., tumeshapata taarifa na tumekufata ofisini na mimi mwenyewe nimekufata ofisini umenihakikishia mradi huu wa maji unaenda kwisha. Kutokana na umahiri wako na usikivu wako kama ulivyofanya katika Kijiji cha Kasu ulikuja nikakuomba shilingi milioni 400, wananchi wa Kijiji wameshapata maji na wanakushukuru sana, tupelekee salamu kwa Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi alikpokuwa niliwasilisha changamoto ya maji Wilaya ya Nkasi. Ulipigiwa simu palepale ukatupatia shilingi milioni 400, zimeshafika na ukarabati wa mabwawa Wilaya ya Nkasi kutatua changamoto ya maji kama dharura umeshaanza; tunakushukuru sana wananchi wa Wilaya ya Nkasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya hapo Wilaya ya Nkasi ina changamoto kubwa, suluhu ya kutatua hii changamoto ya maji ni kutoa maji Ziwa Tanganyika, tumemfata Mheshimiwa Waziri ofisini ametuhakikishia upembuzi yakinifu umeshaanza. Nikushukuru sana Naibu Waziri ameshafika Wampembe kwa sababu mradi huu wa maji kutoa Ziwa Tanganyika unaanzia Jimbo la Nkasi Kusini Kata ya Kizumbi Tarafa ya Wampembe, tenki kubwa linajengwa Kijiji cha Kantawa, baada ya Kantawa maji yanaenda wilayani; tunasema ahsanteni sana, mradi huu ukamilika mapema ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vijiji vinavyopita katika mradi huu viweze kupata maji na wananchi pamoja na vijana wengi wa Jimbo la Nkasi Kusini wapate ajira kupitia mradi huu mkubwa wa maji. Pia, upo mradi wa Kizumbi kwenda Wampembe, tarafa nzima hii haina mradi wa maji. Nikuombe mradi huu ni wa muda mrefu, Kata ya Kizumbi kwenda Wampembe kuna changamoto tarafa nzima haina mradi wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshmiwa Waziri, utakapokuja kuhitimisha hotuba yako uje na majibu ya namna ya kutatua changamoto ya mafundi wa pampu kwa sababu pampu ikiharibika wanasema inakaa muda mrefu, wananchi wanasubiria. Tuandae mafundi mahalia kama ni wilayani na kama ni kijijini tuwa-train ili pampu ya maji inapoharibika awepo fundi mara moja anaenda anatengeneza na wananchi wanaendelea kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bili za maji zimeongelewa humu, hizi bili za maji ziendane na vipato vya wananchi. Kuna wananchi wa TASSAF wengine hali duni vipato viko chini. Kwa hiyo, bili walau tukae chini muone namna ya wananchi watavyolipa kulingana na vipato vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha naunga mkono hoja. Ahsante sana.