Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani kwa kupata nafasi hii ya kuchangia Wizara hii ya Maji. Niungane na wenzangu kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Rais mpendwa wa Tanzania lakini Rais ambaye amekuja kuleta matokeo ya Watanzania nini kinafanyika kwenye kumtua mama ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nirejee kumpongeza Waziri wetu wa Maji na Naibu wake lakini Katibu Mkuu wa Maji na watumishi wote wa Wizara ya Maji. Wakati tunaingia 2020 hasa nikizungumzia kwenye jimbo langu nilikuta tunakinga maji kwenye mabomba yenye rangi ya njano. Tulipata kura Jimbo la Mtwara Mjini watu walikuwa wanatoa kura lakini kwa masikitiko. Hawaelewi kwamba kura wanazokipa Chama cha Mapinduzi faida yake ni nini? Hususan kwenye suala la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilivyokutana na Mheshimiwa Aweso nikamweleza juu ya halihalisi ya maji ya Mtwara akanambia kaka usipige kelele suala hili nalibeba nakwenda kumweleza Rais. Nakushukuru sana Mheshimiwa Aweso ulitupatia fedha shilingi bilioni tatu na kujenga chujio ambalo kwa sasa hivi linasaidia kwa 80%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuishia hapo tu, baada ya chujio lile kukamilika bado maji yalikuwa yana rangi. Nikarudi tena kwa Waziri wa Maji nikamweleza bwana tayari tiba tumeipata lakini kuna matatizo madogo madogo ya maji, akanambia kaka Rais wetu ni msikivu sana ngoja nilibebe Mheshimiwa Aweso nakushukuru sana mlituletea fedha shilingi bilioni 19 ambazo tumeanza sasa kuyaondoa mabomba yaliyowekwa mwaka 51 ambayo yana kutu na yalikuwa yanapitisha maji pale chini; Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunae Engineer wetu wa maji, Engineer Reja; kwa kweli huyu mtu mzima na kama itakapofika muda wa kustaafu Mheshimiwa Waziri muongezee tena kwenye mkataba aendelee kuwatumikia watu wa Mtwara kwa sababu ndiyo suluhisho la watu wa Mtwara kufika mahala sisi tukajivunia kwamba tuna mtendaji ambaye anawajibika kwa malengo ya kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tena kuipongeza Serikali na kumpongeza Rais, eneo la Mtawanya Mheshimiwa Waziri wamepita Marais zaidi ya wanne lakini eneo lile lilikuwa bado halijalipwa fidia ulivyokuja Mtwara nikakueleza wananchi wanavyopata shida ambapo wanadai fidia takriban ya shilingi milioni 700. Mheshimiwa Aweso uliniahidi kwamba unakwenda kwa Rais, peleka salamu zetu kwa Rais kwamba watu wale tayari wamelipwa shilingi milioni 700 za fidia ya takriban miaka 20 iliyopita, kwa hiyo, tunatanguliza shukran kwake na hatuna cha kumpa lakini atatuona mwaka 2025 kura zitakavyojaa kwenye sanduku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso leo sitaki kuzungumza sana lakini nina jambo moja nataka nikueleze kaka yangu. Tuna mradi wa Mto Ruvuma, suluhisho la Mtwara ni kuleta maji ya Mto Ruvuma na brother nilikuwa nakusudia nije hapa leo nikamate mshahara wako lakini kila nikikuangalia na sura yako na jinsi ulivyo siku ya leo unanigeukia mara mbilimbili njoo na majibu utueleze kwamba mradi ule package yake inaanza lini ya kutuletea maji ya Mto Ruvuma kuja pale Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nichukue fursa hii kukuomba kaka yangu na ndugu yangu umenisaidia sana kwenye Jimbo la Mtwara Mjini usichoke kutusaidia, hili nina imani unaliweza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuunga mkono hoja na Mungu akubariki sana.