Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya maji, Wizara muhimu kabisa kwa maisha ya wananchi wetu. Mimi pia, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo anafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kwamba, azma yake ya kumtua mwanamke ndoo kichwani inatimia. Wote ni mashahidi, tumeona ni jinsi gani pesa zimemiminika kwenye majimbo yetu, ili kutekeleza azma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Muhambwe limepokea takriban shilingi bilioni 8.5 ili kutekeleza miradi ya maji mijini na vijijini. Hii imetusababisha kutoka kwenye upatikanaji wa maji vijijini kutoka 54% mpaka 77% na kwa upande wa maji mijini kutoka 37% mpaka 67%, hizi ni jitihada kubwa sana. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu, ameibeba ajenda hii akiwa bado ni Makamu wa Rais na ameenda kuitimiza kwa kishindo ambapo amekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pongezi nyingi zimuendee na waswahili wanasema tunampa maua na bustani yake kwa sababu, amefanya kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Jumaa Aweso, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii. Nampongeza Engineer Mwajuma kwa kazi nzuri anayoifanya, tumeona jinsi anavyofanya akiwa Naibu Katibu Mkuu na sasa anatekeleza kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza watendaji wa maji wa Mkoa wa Kigoma, Engineer Mwenda, Engineer Aida na Almas wa Kibondo kwa jinsi ambavyo wananifanya niweze kutekeleza kazi za Wizara hii ya Maji katika jimbo langu kwa urahisi. Hongereni sana watendaji wote wa Wizara ya Maji kwa jinsi mnavyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso kipekee nakushukuru kwa heshima uliyonipa ya kufika Jimboni kwangu Muhambwe. Umekuja ukajionea mambo yanavyokwenda, kwa kweli tunamshukuru sana, Wana-Muhambwe wanakushukuru sana. Nachukua nafasi hii kusema tunakushukuru kwa sababu, ahadi ulizoziahidi zimekwishatekelezeka. Tumepokea gari moja kama ulivyotuahidi, tumepokea pikipiki nane na tumepokea guta la tani tatu katika Jimbo letu la Muhambwe. Tunakupongeza sana na ninakushukuru kwa niaba ya Wananchi wa Muhambwe, Mwenyezi Mungu akubariki sana ndugu yangu Mheshimiwa Aweso. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba, tumepiga hatua kubwa sana kwenye miradi ya maji. Wote wameongelea, sina sababu ya kurejea, lakini hizi pongezi ambazo mpaka Kimataifa na kidunia mnakwenda kushika nafasi ya pili kwa miaka miwili mfululizo sasa ndizo ambazo zimefanya tuweze kutekeleza miradi ya maji. Tumeona kwa kufanya kwenu vizuri, badala ya kuwapelekea huduma ya maji watu milioni tatu, mmepeleka kwa watu milioni nne, mmesababisha muaminiwe na mpewe pesa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona miradi ya P4R sasa itakwenda kupokea Dola za Marekani milioni 654 kutoka milioni 350. Hizi ni jitihada kubwa na wananchi wa Muhambwe wamefaidika. Kile kiasi cha shilingi bilioni 1.3 uliyonipatia kutoka P4R basi wananchi wa Rukaya wanakunywa maji, wananchi wa Magarama wanakunywa maji na wananchi wa Mikoko wanakunywa maji. Kwa hiyo, ni jitihada kubwa, tunakupongeza na tunaamini tutaendelea kupata pesa zaidi, ili miradi katika majimbo yetu iweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi nzuri hizi ambazo tunaendelea kumpatia, bado zipo changamoto ndogo ndogo ambazo tunaamini Serikali yetu inaziweza. Kwanza kabisa Wananchi wa Mkoa wa Kigoma leo wamefurahi sana kusikia kwamba na sisi tunaenda kuingia kwenye historia ya kupata maji kutoka kwenye Ziwa Tanganyika. Hiki kilikuwa ni kilio chetu na leo tumekusikia kwamba, mshauri anaendelea kufanya kazi, tunaamini atakuja na matokeo chanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mimi jimbo langu lina Mto Malagarasi, kutoka Mto Malagarasi mpaka kata yangu ya kwanza ya Busunzu ni kilomita nane. Wananchi wa Nyalulanga na Busunzu hawana maji ilhali wako katika Mto Malagarasi, lakini sijakuona kuandika Mto Malagarasi kwenye grid yako. Mheshimiwa Waziri nakuomba uuingize Mto Malagarasi kwa sababu uko karibu sana na jimbo langu na utakwenda kutatua changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni Jimbo la Muhambwe tumefanya vizuri sana. Kwa sasa tunapata maji lita milioni tatu kwa siku, lakini mahitaji ni lita milioni 6.8 kwa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Neema ya Mwenyezi Mungu, kupitia mitambo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, moja ya kisima tulichochimba katika Kata ya Lusohoko kimetufanyia maajabu kwa sababu, kimeleta maji mengi sana. Wanasema inawezekana ni katika mkoa mzima kisima kile kinatoa lita laki tatu na nusu kwa saa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri Aweso kwa sababu, kisima hiki kimeleta hayo maji hatuna tena sababu ya kwenda kutoa maji Nduta kwa ajili ya maji ya mamlaka ya mji kwa maana ya Kata tatu za Kibondo Mjini, Biturana na Kumwambo. Tunachotakiwa kufanya, nakuomba Mheshimiwa Aweso, tumeshakuletea andiko ambalo linagharimu shilingi bilioni 4.5, hili tunakwenda kuweka tanki tu pale kwenye Mlima wetu wa Muyaga pale Kitahana na maji tunatoa Lusohoko badala ya kuhangaika na Mto Nduta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso nakuomba unavyokuja kuhitimisha unihakikishie umeuweka mradi wangu huu mpya wa maji kutoka katika kisima hiki cha maji ambacho kimeonyesha maajabu katika Mkoa wa Kigoma, ili Wananchi wa Jimbo la Muhambwe waweze kupata maji. Kwa kufanya hivi, nina uhakika tutakwenda kutimiza matakwa ya Ilani yetu ambayo yanatutaka tufike 85% kwa 95% ya maji mijini na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi mwingine wa Nyamkokoma ambapo ni Kata ya Kumwambu, wananchi hawa hawana maji kabisa. Mradi ule umeshaanza japo kwa kununua mabomba tulipopata shilingi milioni 300, lakini mradi huu unahitaji shilingi bilioni moja. Naomba Serikali inisaidie niweze kupata hii pesa kwa ajili ya kuweza kutekeleza huu mradi wa Nyamkokoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tuna vijiji sita ambavyo havijapata miradi. Mimi naishukuru Serikali kwa sababu, naamini vijiji hivi sasa vya Kumkuyu, Kasana, Nyarugusu, Kumhama, Nyarulanga na Kigina vitafaidika na hivi visima 900 ambavyo Mheshimiwa Rais ametoa. Kwa niaba ya Wananchi wa Muhambwe ninaishukuru sana Serikali kwa sababu, sasa tutakwenda kupata miradi ya maji katika vijiji vyote vya Jimbo la Muhambwe, ili Wananchi wa Muhambwe waweze kuendelea kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi niungane na wenzangu kuunga mkono hoja ya bajeti hii ya Wizara ya Maji kwa sababu, kwa kweli imetupa heshima katika majimbo yetu. Mwenyezi Mungu ambariki sana Rais wetu na Waziri wa Maji. Ahsante sana. (Makofi)