Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Innocent Edward Kalogeris

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ya Wizara ya Maji, Wizara ambayo kwa uhakika imebeba maisha ya Watanzania. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kumtua mwanamke ndoo. Hii ilikuwa ni agenda yake toka alipoingia akiwa Makamu wa Rais lakini sasa hivi akiwa kama Rais, ameisimamia kwa dhati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, Naibu wake Mheshimiwa Engineer Kundo pamoja na watendaji wakiongozwa na Katibu Mkuu Engineer Mwajuma, kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati ya moyo wangu Engineer Mmasi, Meneja wa Bonde Ruvu, lakini Engineer wa Mkoa wa RUWASA pamoja na Engineer wa Wilaya yangu ya Morogoro Vijijini kwa kazi kubwa ambayo wameifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, nilienda ofisini kwake kwa suala la Mradi wa Kibana Group, mradi ambao una-cover kata nne lakini vijiji 13. Mwaka jana tuliweka token ya shilingi 200,000,000 pamoja na VAT, unahitaji shilingi 10,000,000,000. Tulishindwa kutangaza, lakini mwaka huu Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri na Engineer Mwajuma tulikuwa pamoja juzi, tumetenga shilingi bilioni 1.8. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, niombe, mmeniahidi kwamba tutatangaza, kwa hivyo nikuombe Engineer wangu wa maji wa mkoa yupo, naomba baada ya kupitisha bajeti kesho, naamini itapita, mwende mkakae, mradi hu utangazwe. Wananchi wa vijiji 13 na kata nne wapate mahitaji yao ya majisafi na salama. Hasa ukitilia maanani, Mkoa wa Morogoro, Jimbo la Morogoro Kusini ndilo linalotoa maji 76% kwa viwanda Dar es Salaam na Pwani. Kwa hivyo wana Morogoro wana haki ya kupata haki yao hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini natumia nafasi hii kumpongeza Ndugu yangu Mheshimiwa Aweso kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Mwaka jana, kuna Mradi wa Bwakila Juu Tower, kuna fedha ilitengwa lakini haikupatikana, nadhani bajeti bado haijakamilika. Kuna Mradi wa Mvuha Dala, lakini kuna Mradi wa Lundi. Wakati ulipokuja kuna ahadi ulitoa ya kutoa fedha ili maji yafike kwenye Kijiji cha Milango Miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba wakati bajeti bado inaendelea Mheshimiwa Waziri, angali kwa namna moja au nyingine, unafanyaje kusudi miradi hii ikamilike na wanachi wetu wa Morogoro Vijijini ambao ndiyo wahifadhi wa maji kama nilivyosema wa Dar es Salaam, wao nao waone wanafaidika vipi na maji. Nakupongeza kwa visima vitano ambavyo tumevipata ambavyo tutakwenda kuchimba Lukulunge, Nige, Kibangile, Vihengele na Ikulo. Ni imani yangu kwamba vitaenda kusaidia kuondoa kero kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hili, namwomba Mheshimiwa Waziri na watendaji wake hebu waangalie, sisi watu wa Morogoro kuendelea kupewa visima, siyo sawa. Sisi kama wahifadhi wa maji, tunahitaji tupate miradi ya maji ya mserereko, lakini nitumie nafasi hii kupongeza kwa ujenzi wa Bwawa la Kidunda umefikia 17.5%, lakini ziko changamoto ambazo ningependa nizi-address katika Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hoja, atamke kwamba Mradi wa Kidunda utaenda kutoa maji kwa Halmashauri ya Morogoro Vijijini kwa sababu ndani ya mpangilio wake, haioneshi. Ninajua ulinieleza kwamba tutapata maji lakini kwa kutamka ndani ya Bunge itakuwa ni kauli ya Serikali na sisi wananchi tutakuwa tunafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado kuna changamoto kwa ndugu zangu wa DAWASA katika kulipa makaburi. Mwaka jana tuliambiwa kuna shilingi bilioni 1.8 lakini hadi tunavyozungumza sasa hivi hakuna kitu hicho. Kwa hiyo tunahitaji wananchi wale wafidiwe makaburi yao ili kusudi mradi uendelee. Vilevile, kuna changamoto kwenye hili suala la Mradi wa Kidunda, wakati unatangazwa, mimi nilikuwepo katika Bunge la Kumi na ndiye nilikuwa mtu wa kwanza katika kuhakikisha kwamba mradi huu unafanikishwa kwa kuwashawishi wanachi wangu wahame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokumbuka wakati wanafanya tathmini ya mazingira, niliomba wananchi wote wa vijiji ambavyo viko kwenye Kata ya Selembala waondoke kwa sababu nilijua athari ambayo itakayowakuta. Vilevile, wananchi ambao wako kwenye Kata ya Mkulazi kwa mdogo wangu Mheshimiwa Tale Kijiji cha Kidunda nao tulisema waondoke. Walioondolewa waliondoka, waliobakia wamebakia. Hivi tunavyozungumza, mafuriko yamekuwa ni athari kubwa kwa wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakokwenda, tunaweza tukampeleka Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwenda kutoa pole wakati siyo sahihi. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, unapokuja kuhitimisha hoja, naomba unieleze, je, Wizara ina mpango gani wa kuwaondoa wananchi wa Kijiji cha Kiganila, Kijiji cha Bwila Juu na Kijiji cha Magogoni katika Jimbo la Morogoro Kusini lakini Kijiji cha Kidunda katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili tuondokane na adha hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa, wakiendelea kuwepo watu hao, tunaweza tukaleta hatari kubwa sana. Vilevile nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri, juzi wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anatoa taarifa za mafuriko, nilizungumzia jambo moja. Nini mpango wa Serikali katika kuvuna maji ambayo yanatokana na mafuriko, hata Mkoa wa Morogoro kila mwaka kuna mafuriko. Tuna mito mitano hiyo ambayo inakwenda katika kutengeneza Bwawa la Kidunda, kama tutaweza kuitengenezea mabwawa kwa juu, tutaweza kuondoa matatizo makubwa ya mafuriko kwa wananchi wetu lakini hili siyo tu kwa Jimbo langu la Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani Wizara itueleze kwa Mkoa wa Morogoro wana mpango gani wa kuchimba mabwawa ambayo yatapunguza mafuriko lakini vilevile yatahifadhi maji kwa mifugo na hata kwa matumizi ya wanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nataka kumuomba Mheshimiwa Waziri kwenye suala la …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Innocent muda wako umeisha.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)