Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini pia namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi wa Singida Mjini tumepokea miradi mingi na fedha nyingi ambazo hazipungui takribani shilingi bilioni 70. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwanza hotuba yake imesomwa kwa ustadi, lakini hata bajeti yake imeandaliwa vizuri sana. Nampongeza sana yeye na timu yake yote ambayo imeandaa bajeti hii. Yako maeneo machache ambayo nachukua fursa hii kuishauri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuyaboresha ili bajeti hii iwe nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na eneo la ukurasa wa tisa na 45, ambalo linazungumzia suala la ugatuaji wa madaraka kwa umma. Nikifanya rejea ndogo ya ukurasa wa 72, tunatambua kwamba, miongoni mwa vipaumbele alivyoviweka ni pamoja na kusimamia utawala bora, kukuza demokrasia, kushirikisha wananchi na kurejesha madaraka kwa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona eneo hili bado Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hawajalifanyia kazi vizuri. Kwa nini hawajalifanyia kazi vizuri, bado halmashauri zetu zinategemea support ya Serikali kwa asilimia 100 katika kusimamia miradi. Lengo la kuanzishwa kwa D by D, ugatuaji wa madaraka, ni kuziwezesha halmashauri kujitegemea, halmashauri ziweze ku-graduate, lakini mpaka tunamaliza hatujaona mkakati wa Serikali kuziwezesha halmashauri hizi kuweza kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia Ripoti ya CAG, utaona kuna mikopo chechefu, kuna vurugu nyingi. Vurugu hizi zinasababishwa na hizi halmashauri kutokuwa na mandate ya kujisimamia, zinasubiri maelekezo kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Sasa, naiomba Serikali katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, tuweke mpango, tuweke mkakati, wa halmashauri hata kama ni chache, hata kama ni kidogo kidogo, tunapokuja mwakani tuweze kujua ni halmashauri ngapi zimeweza ku-graduate, zimeweza kujitegemea, zimeweza kusimamia miradi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata tunapotoa Hati Safi au Hati Chafu sijaona mantiki yake. Mantiki ya Hati safi ni kwamba halmashauri imeweza kujitegemea, hapo ndiyo tuipe Hati Safi, lakini siyo halmashauri imetengeneza hesabu vizuri ndiyo inapewa Hati Safi, hapana. Hili ni jambo langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nimetazama kwenye ukurasa wa 42. Ukurasa wa 42 unazungumzia mfumo wa kutoa elimu kwa masafa marefu au masafa ya mbali (E-Learning System). Ni kweli tunatambua ni mfumo mzuri sana ambao unatumiwa na Education Centre ya Kibaha, ni mfumo mzuri. Lengo hapa ni kwamba, sasa wanataka kutuelekeza kuwa mfumo huu wa kutoa elimu kwa masafa marefu katika shule zetu ni kuwezesha ku-cover gap la upungufu wa walimu. Hili jambo hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tukubaliane vizuri kwamba, tunapokuja na teknolojia kama hii tuje na teknolojia ya kuwawezesha walimu kuwa wabobezi kwenye shule zao ili waweze kufundisha vizuri, lakini tusije na teknolojia ya kufundisha moja kwa moja darasani. Darasani kuna zaidi ya ufundishaji, suala la ufundishaji ni malezi. Tunahitaji interaction ya mwalimu na mwanafunzi, interaction ya mwalimu na wazazi. Sasa, bado mazingira yetu hayaruhusu na wala siyo rafiki kwa mfumo kama huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiamua kuwa na mfumo kama huu maana yake ni kuaminisha kwamba, sasa tunataka teknolojia ku-replace human labour, jambo ambalo haliwezekani. Kitu ambacho nataka kushauri hapa ni kwanza, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waweke mpango wa kuhakikisha kila mkoa unakuwa na E-Learning System. La pili, E-Learning System isaidie ku-empower walimu. Wale walimu tulionao tuwafanye kuwa wabobezi, lakini jukumu la Serikali la kuajiri libaki pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirejea katika ukurasa wa 42, nimefanya uchambuzi kidogo nimeona kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii, ni nzuri sana, lakini tunazungumzia Chuo cha Hombolo. Chuo cha Hombolo sasa wanaanzisha Campus Shinyanga, siyo jambo baya ni jambo jema, lakini lengo la kuanzishwa Chuo hiki cha Hombolo lilikuwa ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo siyo kuzalisha tu wataalamu au maafisa, lilikuwa ni kutoa mafunzo kwa Madiwani, Watendaji wa Kata, Makatibu Tarafa na wengine wote ili wawe na uwezo wa kusimamia miradi na kuibua miradi. Wawe na uwezo wa kupunguza hoja za CAG, lakini lengo hili la kuanzishwa chuo hiki bado halijatimia, lakini tunaanzisha campus nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, campus hii inaenda kuzalisha wataalamu wengine wakati hakuna ajira. Nataka kuiomba Serikali, turudi kwenye lengo la msingi la Chuo hiki cha Hombolo kifanye majukumu yake yaliyokusudiwa, kitatusaidia kupunguza migogoro kwa watumishi au migogoro kwenye eneo letu hili la Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo wamefanya vizuri sana ni la Tume ya Utumishi wa Walimu, ukurasa wa 69, wamefanya vizuri sana na nawapongeza. Tume ya Utumishi wa Walimu (TACC) sasa hivi wamekuja na mpango mzuri wa Teachers Management Information System. Teachers Management Information System ya TACC inatusaidia kuweka sawa data za watumishi. Huko nyuma tulikuwa na tatizo kubwa sana, tatizo ambalo linamfanya mwalimu anatoka Nanyumbu, Mtwara anakuja Dodoma, anafika anaambiwa bwana wewe tunaomba barua yako ya ajira, tunaomba barua yako ya mwisho ya kupanda daraja. Yeye anaitoa wapi amekaa kazini miaka 35? Wewe uliyemwajiri huna hiyo barua, uliyempandisha daraja huna hiyo barua, umeweza kumpa mshahara wa mwisho hata document ile wewe huna, unataka yeye akupe anaitoa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzishwa kwa Teachers Management Information System kumeenda ku-accommodate matatizo makubwa yanayojitokeza kwenye jamii hii. Hapa, nataka kuishauri Serikali jambo la msingi, kwa sababu tunaanzisha mfumo huu, basi tuuweke wazi ili mwalimu kwenye simu janja yake awe anapata taarifa zake moja kwa moja. Akiingia kwenye hiyo portal kila kitu anakiona, ili anapokuja kustaafu lisiwe tatizo tena. Vilevile mfumo huu tu u-link na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili mwalimu anapokwenda isiwe jambo tena la kuanza kumuuliza yeye ni nani? Tayari document itakuwa inaonesha kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushauri eneo hili; hawa Maafisa wa TACC wamekuwa ni Desk Officers. Wako pale kusubiri mashtaka yanayoletwa na mkurugenzi kwamba, mtumishi huyu au mwalimu huyu moja, mbili, tatu. Kazi ya TACC siyo kuja kuonesha ina mashtaka mengi, kazi kubwa ni kupunguza. Sasa inapunguzaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, iende kule site, waende wakatoe elimu ya maadili shuleni ili kuwasaidia walimu kuweza kujua majukumu yao na kuepukana na hizi changamoto. Maana yangu ni kwamba, wawezeshwe, itengwe bajeti ya walimu hawa kwenda. Kwa nini leo Wadhibiti Ubora wana magari na wanaweza kwenda shuleni wakafanya kazi yao? Kwa nini TACC wakae ofisini? Itengenezwe bajeti, watoke waweze kwenda na wao wakatoe elimu ambayo itaweza kuwasaidia walimu tuondokane na suala hili la utovu wa maadili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo pia nimelitazama na ni vizuri sana na Serikali ikaliangalia ni mabadiliko ya tabianchi. Ukurasa wa 64 tumezungumzia habari ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi. Tunazo halmashauri 184, Hotuba ya Waziri imezungumzia halmashauri 15. Katika Halmashauri 15, saba zimeshaingia mkataba wa hewa ya ukaa, lakini nane ziko kwenye mchakato, the rest bado. Sasa kama halmashauri hizi zote zinatakiwa, nakumbuka Makamu wa Rais akiwa Mama Samia alitoa maelekezo ya kila halmashauri, kupanda miti milioni moja, hii miti milioni moja mpaka leo haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakuja na biashara ya carbon wakati hatuna mkakati wa kuhakikisha kwamba, halmashauri hizi zinapanda miti ya kutosha ili tuepukane na mabadiliko ya tabianchi. Naiomba Serikali kwenye bajeti hii isisubiri Ofisi ya Makamu wa Rais waje na miradi, wao wanayo nafasi ya kuzisimamia halmashauri zikapanda miti ya kutosha na wote wakaingia kwenye suala la biashara ya carbon, eneo hili haliwezi likawa limebaki tu hewani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii. Kazi yake kubwa ni kufanya monitoring and evaluation. Sasa, jambo hili halijafanyika vizuri, sisi wa Singida Mjini tunawapongeza, tunayo hospitali ya manispaa, ni hospitali nzuri lakini, tumepewa fedha kwa ajili ya majengo na tunaendelea nayo. Tunahitaji kupata fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, tunajenga jengo letu la OPD liwe la kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Hotuba ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imezungumza kwamba, ziko hospitali za wilaya ambazo ni za zamani zimechakaa watazipa fedha kwa ajili ya kukamilisha au kufanya ukarabati. Naomba hospitali ya manispaa iwe ni mojawapo kwa sababu, ndiyo uso wa Mkoa mzima wa Singida. Tunahitaji tupate fedha hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata fedha za vituo vya afya na sasa nina Kituo cha Afya cha Kisake, hiki ndiyo kituo cha kimkakati, barabara kubwa inapita pale na ndiyo tunatengeneza bypass nyingine na ziko kata kama tatu au nne ambazo zinategemea hapo. Mimi na wananchi wangu tumejenga, tumefikia hatua ambayo tunahitaji Serikali itusaidie ili kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kisake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, Serikali inatoa pikipiki na pia inatoa magari, hebu turudi kule tukaangalie, yale magari tuliyoyatoa kwenye halmashauri zetu pamoja na vifaa tulivyopeleka kwenye halmashauri zetu hali ikoje? Tusije kuwatwisha mzigo mwingine ambao utakuwa hauwezi kutimia. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Sima, kengele ya pili hiyo.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)