Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia, aliyetujalia uhai na leo tuko hapa tunachangia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambazo anazifanya kwa Watanzania, kuanzia ujenzi wa vituo vya afya, shule na kila kitu. Kweli, ameonesha ni mama anayejali, kama jinsi mama anavyowajali watoto wake nyumbani na yeye anawajali Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa na Manaibu wake. Mwanangu Mheshimiwa Zainab Katimba, hongera sana, nafasi imekuenea mwanangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo napenda kutoa mchango wangu kwa mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni halmashauri pamoja na manispaa nchini Tanzania zimezua tabia ya kujenga shule zenye mkondo wa Kiingereza, kwa maana ya English Medium. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapitisha Bajeti ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, lakini linapopitisha hii ndani yake huwa kunakuwa na pesa ambayo inapaswa kwenda kuhudumia shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapopitisha bajeti hii ina maana linataka elimu bora kwa Watanzania wote, kwa watoto wote wa Kitanzania. Sasa uanzishwaji wa shule hizi zenye mkondo wa usomaji wa Kiingereza, tunaziita English Medium, wananchi wanaambiwa walipie, lakini siyo wananchi wote wenye uwezo wa kulipia hizo shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza, Sera ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu elimu ni Elimu Bila Malipo, sasa, je, Ofisi hii ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inataka kuniambia kwamba, sasa hivi Serikali inafanya biashara kwa kufungua shule zenye mkondo wa Kiingereza? Kwa sababu shule hizo zinalipiwa na siyo wananchi wote wenye uwezo wa kulipia, kama kuna haja ya kufundisha Kiingereza, ni kwa nini basi hiki Kiingereza kisifundishwe kwenye shule zote? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo, shule hizi zinatumia walimu ambao wanalipwa mshahara na Serikali. Sasa iweje walimu wale walipwe mshahara na Serikali halafu halmashauri au manispaa ziseme kwamba, zimetengeneza kitega uchumi wakati walimu wanaofundisha pale ni walimu ambao wanalipwa na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo wanachukua wale walimu bora, mawazo yangu ni kwamba, wale walimu wangetawanywa kwenye shule zote nchini ili waweze kuwafundisha wanafunzi wote. Naona shule hizi zinakwenda kujenga matabaka nchini Tanzania. Hapa tulipo tutajenga matabaka ya watoto wa walionacho na watoto wa wasiokuwanacho na ina maana haya matabaka tutakuwa tumeyatengeneza sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Sera ya Serikali ni Elimu Bila Malipo, basi sioni sababu ya halmashauri au manispaa kujenga shule ambazo zinahitaji kulipiwa ada. Mwaka jana nilimuuliza Waziri wa Elimu atoe ufafanuzi, akasema shule hizo hata kama zimejengwa watoto watasoma bure. Naomba Hansard irejewe, hayo yalikuwa ni majibu ya Waziri wa Elimu. Kwa suala hili, naomba halmashauri zilizoanzisha shule hizo ziweze kuzibinafsisha kwa watu binafsi ili waweze kuziendesha kwa sababu, Serikali huwa haifanyi biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naenda kwenye Wilaya ya Mpanda katika Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye Mkoa wangu wa Katavi nime-sample research ya shule zilizoko kwenye Wilaya ya Mpanda pale Mpanda Mjini. Shule hizi ni chakavu, nikianza na Shule ya Shanwe, shule hii ilianzishwa mwaka 1959, ina wanafunzi 1,588, lakini ina walimu 18 tu wanaowafundisha hao wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Shanwe ina madarasa 11 tu. Vilevile shule hii ina uhitaji wa matundu ya vyoo kwani yaliyopo kwa sasa ni matundu 11 tu kwa ajili ya wasichana na matundu mengine 11 yanayotumiwa na wavulana. Shule inahitaji madawati 316, watoto kuanzia darasa la tatu, la nne wanakaa chini. Ina maana watoto wanaokaa kwenye madawati ni watoto wanaoanza darasa la tano, la sita na la saba. Watoto hao wanakaa chini, hii ni Shule ya Shanwe inayopatikana pale Mpanda Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule nyingine, Shule ya Nsemulwa imeanzishwa mwaka 1974 ina wanafunzi 1,582, ina walimu 16 tu na madarasa nane. Shule ina upungufu wa madawati 568, shule ina matundu ya vyoo 12 tu, sita kwa wasichana, sita kwa wavulana. Huu ni upungufu wa hali ya juu na hizi shule zote zinapatikana pale Mpanda Mjini ambayo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule ambayo utashangaa ni shule ya Misukumilo. Shule hii ina wanafunzi 3,082, lakini ina walimu 19 tu ambao wanafundisha hao wanafunzi 3,082. Shule hii yenye wanafunzi 3,082 ina upungufu wa madawati 500, ina maana watoto wanakaa chini lakini ina matundu ya vyoo 13 kwa wavulana na 13 kwa wasichana, shule yenye watoto 3,082… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tunaomba utulivu ndani ya Bunge.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, shule hii yenye watoto 3,082 ina walimu 19 tu ambao wanafundisha hao watoto, huu ni upungufu wa hali ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule nyingine pale pale Mpanda Mjini, Shule ya Msakila ina wanafunzi 2,370, lakini ina upungufu wa vyoo, ina upungufu wa madawati na ina upungufu wa walimu. Kuna shule nyingine, Shule ya Nyerere ipo pale Mpanda Mjini ina wanafunzi elfu moja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango mzuri.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, lakini naomba Serikali iangalie kutupatia walimu pamoja na vitendea kazi. (Makofi)