Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Naomba kujibu swali ambalo linazungumzwa kwenye mitandao kupitia Tarime Vijijini kwamba kwa nini Wabunge na Makada wa Chama Cha Mapinduzi wanampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama wa Taifa. Kwanza naomba kumpongeza kwa uteuzi mzuri sana wa Katibu Mkuu Dkt. Emmanuel Nchimbi, Balozi na kazi imeshaanza. Huko tunapoelekea mambo ni mazuri zaidi lakini vilevile imefanya mabadiliko ya uongozi kwenye Mkoa wa Mara. ametuletea Kanali mwingine, Kanali karibu sana katika Mkoa wa Mara, Mara tupo imara. Pia, kaleta Kanali mwingine pale Wilaya ya Tarime, tumempokea tumeanza naye kazi ni kada wa Chama Cha Mapinduzi anachapa kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Tarime Vijijini katika Halmashauri ya Tarime DC, elimu ya msingi, sekondari na afya tumeshapata shilingi bilioni 18.947 katika madarasa ya BOOST na maeneo mengine. Watu wa Tarime DC lazima waendelee kumpongeza Mama Samia kwa kazi nzuri. Tumejenga madarasa ya sekondari 216 mpaka sasa katika uongozi huu wa Awamu ya Sita tukianzia Awamu ya Tano, lazima Mama Samia aendelee kupongezwa. Tumejenga shule za msingi mpya 10 Tarime DC, tumejenga sekondari 18 mpaka ninavyozungumza hapa. Mama Samia lazima aendelee kusemwa, huyu ndio Mama mwenye nyumba, hakuna mwingine kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa umma 556 wamepandishwa madaraja 100%, mwaka huu watapandishwa 350 Tarime DC. Mama Samia lazima aendelee kusemwa usiku na mchana kama dozi ya malaria. Kule TARURA, mpaka sasa jimbo langu tumepata shilingi bilioni 18.044 kwa maana ya barabara. Madaraja ya Kebweye, Magoma Bulege na Rozana yamejengwa, changarawe kilometa 50.7 na barabara zingine zaidi ya kilometa 207 zimejengwa katika Jimbo la Tarime Vijijini. Mama Samia lazima aendelee kupongezwa kwa kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika RUWASA mpaka sasa jimboni kwangu tumepata fedha shilingi bilioni 11.469 za maji na miradi mikubwa. Ongeza Mradi wa Kimkakati wa Maji kutoka Rorya, Tarime mpaka Sirari shilingi bilioni 134 ambao utaenda mpaka Nyamwaga, utaenda mpaka Nyamongo. Mama Samia lazima aendelee kupongezwa katika kazi nzuri. Katika habari ya umeme tumeshapeleka umeme katika vijiji 52, sasa jimbo zima vijiji vyote 88 umeme unawaka. Sasa tunaelekea kumaliza umeme kwenye vitongoji vyote, jimbo lina vitongoji 500 na mpango umeshakamilika, mkandarasi yupo site, ameweka vigingi. Tarime Vijijini lazima wamseme Mama Samia kwa mambo mazuri, zaidi ya shilingi bilioni 12.8 zimepelekwa katika Jimbo la Tarime Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, nije kwa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI. Kwanza nampa hongera Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anafanya. Wabunge na Watanzania wana imani kubwa na Waziri kwa kazi aliyopewa, upele umepata mkunaji. Maombi na ushauri ni kwamba akisoma hotuba ya Kamati ya TAMISEMI ambayo mimi ni Mjumbe, apokee maoni yetu kwa niaba ya Wabunge wote ayatekeleze.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba na kumshauri, ni mbaya sana kwa kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais anaifanya, halafu Ripoti ya CAG inaonesha kwenye halmashauri kuna fedha zimeibiwa. Wanatupa changamoto kwa sababu wananchi wetu wanachangia gharama za maendeleo, halafu tunatoa ripoti ambayo fedha zimeliwa na watumishi ambao wamesoma, ni wataalamu na wanalipwa mishahara. Kipengele hicho Mheshimiwa Waziri asimamie, kama kuna mtu ambaye ni mwizi anakula fedha za halmashauri za Watanzania maskini, ashughulike naye na asikubali kumhamisha mtu kutoka kituo ‘A’ kwenda kituo ‘B’, kama mtu ameiba ampeleke jela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kuwashauri hapa wanyonge watu hawa ili wakome kuiba fedha za umma. Naona bado hawajanielewa, lakini jambo la pili asifunge masikio. Habari ya kikokotoo amwambie Mheshimiwa Rais, Wizara hii ina watumishi wa umma zaidi ya 60%. Mheshimiwa Waziri akae na Mheshimiwa Rais, watumishi wa Tanzania wanataka majibu namna ya kupeleka unafuu katika kikokotoo. Tumeshasema alipokee kama hoja ya Bunge, hoja ya watumishi wastaafu na watumishi waliopo kazini, hilo ni takwa lao alifanyie kazi. Kabla ya Bunge hili kwisha watumishi hawa wapate kauli ya Mama Samia, kauli ya Mama mwenye utu, Mama wa maadili ili wapate unafuu katika utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa ni aibu kwa rasilimali tulizonazo na kazi nzuri inayofanyika, Wabunge kusimama Bungeni kuuliza maswali eti matundu ya vyoo, watoto wanakaa chini, sijui madarasa, viti na meza. Waweke mkakati katika Wizara ili ifike mwisho Wabunge kuja kwenye Bunge hili na kuuliza masuala ya matundu ya vyoo, kuja kuzungumza habari ya madarasa au nyumba za walimu. Tunaweza kukamilisha na hii shida ikaisha. Mheshimiwa Waziri atoe maelekezo kwa wakurugenzi kwenye bajeti zetu, kila mkurugenzi atuoneshe ana upungufu wa matundu ya vyoo mangapi na ndani ya muda gani yataisha, wanahitaji madarasa mangapi na ndani ya muda gani yataisha. Tuwe na mpango kazi wa muda mfupi, wa muda wa kati na muda mrefu ili hii shida iishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Watanzania, kwa miaka yote ya uhuru, kuzungumzia matundu ya vyoo, hili jambo siyo sawasawa. Kwa hiyo naomba hili Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi na alisimamie. Tunahitaji tupate majibu katika eneo hilo. Nataka nijue pia kwenye bajeti hii ya TAMISEMI, lakini pia na Waziri wa Fedha anapokuja ku-present bajeti yake hapa, madiwani na wenyeviti wa vijiji mara ya mwisho kupitia posho yao ilikuwa mwaka 2012. Ni wazi kwamba kuna mabadiliko makubwa, maisha yamekuwa ni magumu, wanafanya kazi nzuri. Ukisoma kwenye Katiba, Ibara ya 145(1) ndiyo imetamka kuanzisha Serikali za Mitaa. Vilevile Ibara 146(1) inasema madaraka yapo kwa wananchi na wananchi hao watakaa na uongozi wao kujipelekea maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hao wanaosimamia Serikali za Mitaa ni wenyeviti wa vijiji, vitongoji, wajumbe, madiwani, Wabunge na Watanzania kwa ujumla. Ni muhimu kwenye bajeti ya Serikali ioneshe namna ambavyo wamepokea maombi yao ya kuboresha posho au kuwapa mishahara ili waweze kufanya kazi yao. Kama maisha yanapanda kwa Watanzania hata kwa madiwani na wenyeviti wa vijiji pia yamepanda hayo. Naomba pia na eneo hilo watoe kauli, kwa sababu Wabunge wanapata lawama kwamba hawawasemei, naomba watoe kauli ili tuongee lugha moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia maneno pia huko mtaani kwamba uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za Mitaa 2024, Ofisi ya Rais, TAMISEMI isisimamie. Ibara ya 145(1) kama nilivyosema inataja kuanzishwa kwa mamlaka za mtaa, lakini Ibara ya 146(1) inataja madaraka ya Serikali za Mitaa. Maana yake kama unazungumzia Serikali za Mitaa utaenda kwenye Katiba, wizara ambayo inahusika na Serikali za Mitaa ni Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Mheshimiwa Mchengerwa aendelee na maandalizi ya Serikali za Mitaa, yupo Kikatiba, anatajwa kwenye ibara niliyoitaja, tunasubiri mchakato ukamilike, uchaguzi wa mwaka huu ni salamu kwao kuelekea mwakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo niliyotaja ya Tarime Vijijini sitarajii kwamba kuna kitongoji au kuna kijiji kitaenda kule kwingine, vyote vimebaki Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo tumejipanga kumpa ushirikiano Mheshimiwa Waziri, asiogope, anachapa kazi na wenzake wote hapo mbele wanatambua nafasi hiyo. Nataka nimwambie Mheshimiwa Mchengerwa, Watanzania wanamwamini, kote alipopita ameacha alama, ameenda Wizara ya Michezo akaacha alama, alikwenda Maliasili, watu wa Tarime wanamkumbuka sana kule Nyanungu, Kwihancha na Gorong’a. Sasa TAMISEMI ndiyo nchi, afanye kazi usiku na mchana, tutampa ushirikiano, apokee maoni ya Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kila baada ya bajeti tuhame kutoka ajenda ya kudumu kwenda ajenda nyingine. Mama Samia ataendelea kusemwa, ndiye mama mwenye nyumba, ndiye Rais mwenye nidhamu kubwa, amefanya maendeleo makubwa. Tusipomsema Mama Samia unataka tumseme nani? Tusipomsema Rais, unataka tumseme nani? Yaani tukuseme wewe kwa lipi? Tunamsema Rais kwa kazi nzuri aliyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kila kijiji, kila kitongoji, kila jimbo, nenda TARURA utamkuta Mama Samia, nenda kwenye maji utamkuta Mama Samia, kwenye barabara kuna Mama Samia, kwenye shule za msingi kuna Mama Samia, kwenye vyuo vikuu kuna Mama Samia, uende baharini kuna Mama Samia. Sasa unataka tuseme nini, Mama Samia anatosha na chenchi inabaki, wajipange makada wa Chama Cha Mapinduzi, tunaenda naye 2025 – 2030, hakuna lingine kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana na Mungu awabariki. (Kicheko/Makofi)