Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, inakushukuru sana kwa nafasi hii adhimu, turuhani ya kuchangia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa makadara yake Mwenyezi Mungu jalia, natoa shukrani jelele, shukurani tumbitumbi kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais wake na Viongozi wote wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema viongozi mbalimbali nami nataka kusimama hapa kukiri mbele yako, mbele ya Watanzania na Mwenyezi Mungu kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa anafanya kazi kubwa ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuelewe kwamba maendeleo ni mchakato mpaka mwisho wa dunia. Tutaondoka duniani, tutafariki bado harakati za kimaendeleo zinaendelea. Leo Marekani wana miaka ziadi ya 200, mjadala wa Bima ya Afya haujaisha, sasa wasitokee watu wanaotaka sisi saa mbili asubuhi kila bomba litoe maziwa. Hilo halitawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yamkini kwamba, nataka kuomba maendeleo, lakini ni vizuri kushukuru na kusema kwa ufupi mambo machache ambayo tuliahidi katika Jimbo la Kilombero, Halmashauri ya Mji wa Ifakara na yote yameshakamilika katika miaka mitatu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wao wanafahamu tulikuwa na mambo makubwa pale hata kama hayapo TAMISEMI, suala la lami kilometa 67 imebaki kilometa mbili. Kuna kiwanda kipya cha sukari, tuna mradi wa umeme wa bilioni 23, tumejenga sekondari sita, zahanati nane, barabara za lami za mitaa na hospitali ya halmashauri tangu wilaya imeumbwa mwaka 1972 ndiyo tunajenga sasa hivi pamoja na vituo vya afya. Tunaanza barabara ya lami Ifakara - Mlimba, Mradi wa Maji wa Kiburubutu bilioni 43, tumepata Mahakama mpya ya Wilaya, tumepata Kituo cha Polisi kipya cha Wilaya na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi ni ajenda kubwa ambazo zilikuwa Kilombero, sisi tumezifanya, sisi siyo malaika lakini tuliyowaahidi, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imefanya. Sasa wale ambao wanaumiaumia tunavyomshukuru Mheshimiwa Rais wetu, wao wanapomshukuru Kiongozi wao mbona sisi hatuumii? Wanavyosema Kamanda tuvushe, hata kama kamanda anabadilisha Katiba anakaa miaka 20, wanasema tuvushe tu, sisi mbona hatuumii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumaliza hiyo shukrani leo hapa kwa kunukuu, maana yake inawezekana sisi tukinukuu hapa tunanukuu tu viongozi labda wastaafu wa CCM, tunanukuu tu viongozi wengine, tunaacha kunukuu viongozi wengine wakubwa katika siasa za nchi yetu kama vile Freeman Mbowe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kunukuu maneno ya Freeman Mbowe aliyoyatoa mwaka 2023 na hapa sasa naanza kunukuu akiwa Mwanza, Ndugu Freeman Mbowe alisema: “Leo niwaambieni kitu Watanzania tumetoka Serikali ya Awamu ya Tano, tumeona uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia, huyu mama ni kiongozi makini, Mheshimiwa Samia ni msikivu, Mheshimiwa Samia ni mvumilivu. Nawaambia ukweli hata kama mtasema nimelamba asali potelea mbali, anaongoza nchi yetu vizuri, anaupiga mwingi sana! Sisi kama Wapinzani lazima tuseme na tukosowe ila Samia ni jembe. Mkumbuke kwamba, mimi ni Mbowe siyo rahisi kupongeza Kiongozi wa CCM lakini kwa Samia napongeza.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu sana maneno haya yakatengenezewa bango, yakawekwa hata barabarani huko ili wananchi wetu waweze kujua kwamba kuna viongozi wanakiri kwamba Dkt. Samia ni Rais wa kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naanza kusema machache kuhusu Jimbo langu la Kilombero, Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Mheshimiwa Waziri na viongozi wa TAMISEMI waliopo hapa wakiniuliza, wanataka kunisaidia nini? Nafikiri wameona hali ya mafuriko, hakuna mtu amepanga mafuriko, hakuna binadamu amesema lete maji leo yakaathiri wananchi. Mafuriko yamekuja yametuathiri. Kwa hiyo, wakiniuliza mimi vitu vitatu vya kunisaidia vya haraka, kwa sababu mambo ni mengi. Nitamwambia cha kwanza ni dharura barabara, barabara, barabara za mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema kwamba kwa sisi ambao tupo Morogoro chini kule bondeni ili barabara zetu ziwe kupitika vizuri wakati wote, lazima uichonge, uijaze kifusi na uiwekee makalavati. Sasa inaonekana nchi nzima kuna uhitaji wa Barabara, lakini watazame maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa. Halmashauri ya Ifakara tumeathirika karibu Kata zote 19, hali ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa kule Msola Station - Kidatu, Sanje, Mkula, Mang’ula, Mwaya, Kisawasawa, Kiberege, Ziginali, Kibaoni, Mbasa, Viwanja Sitini, Katindiuka, Mlabani, Lipangalala, Ifakara, Lumemo na Michenga, Kata zote 19 hali ni mbaya kutokana na mvua nyingi tunazozipata zinazosababisha mafuriko. Yale Mafuriko na hali tunayoipata haigusi kwenye zile barabara ambazo zinawekwa changarawe, zinapitika na wananchi wanatumia. Changamoto ni kwamba, baadhi ya sehemu kuna mashimo makubwa, hivyo barabara za mitaa hazipitiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitoa ushauri ambao kama Bunge tuliwahi kuutoa katika Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo, tukasema Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA waangalie modal ya kununua vifaa, miundo vifaa sijui wanaitaje yale grader, excavator, roller na tipper kwa baadhi ya Wilaya wakabidhi kwa TARURA. Tumepiga hesabu inaweza ikachukua miaka 10, barabara zote za Kata 19 kuwekwa changarawe tu kwa hizi fedha tunazozipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ifakara tuna kifusi kizuri ambako tunajenga barabara ya lami kwa kifusi chetu, kwa kokoto zetu. Wanaweza wakafanya special case Wilaya ya Kilombero wakatupa vifaa ambavyo ni vya bilioni 1.5. Grader, excavator, tipper na shindilia, wakaikabidhi TARURA, wakaweka na mtaalamu wa mitambo wa kusimamia pale, mbona sisi tuna V8, viongozi wa Serikali wana magari hayafi. Waziri akitaka kuleta hii modal watu wanamwambia kwamba, nani atatunza grader zitakufa, sijui nini na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hii modal ni nzuri, tueni mifano kwa mfano, Wilaya ya Kilombero watupatie hivi vifaa. Mfuko wa Jimbo, kiongozi yeyote mwenye pesa anaweza akaweka mafuta kwenye grader akachonga Barabara, akaweka mafuta kwenye tipper ya TARURA akachukua kifusi pale Kibaoni akaenda akajaza kwenye barabara hizi. Kwa hii bilioni 1.0 au bilioni 1.5 tunayopewa, itachukua miaka 10 kumaliza barabara zote 19. Tunasema hii ni modal nzuri sana, lakini wajaribu kuifikiria, vinginevyo watupe basi fedha za kutosha tumalize changamoto hii ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia Ofisi hii inasema kwamba watanunua magari, namwombea gari Mheshimiwa DC wangu Dunstan Kyobya, Wakili Msomi, anafanya kazi nzuri sana kushirikiana na viongozi wake, lakini hana gari. Wilaya ya Kilombero ni kubwa kuliko Mkoa wa Mtwara, DC mara yupo huku mara yupo huku na gari lake ni bovu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana TAMISEMI wametuletea Mkurugenzi mpya Bi. Zahara Michuzi, amekuja juzi ana miezi miwili, amekuta mapato 31%, ameshafikisha 68% sasa. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie mchangiaji nimpe taarifa. Mkoa wa Mtwara ni Mkoa mkubwa hauwezi kuulinganisha na Kijiji chake, kwa hiyo aombe gari kwa ajili yake asilinganishe na Mkoa wa Mtwara. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Haya. Mheshimiwa Abubakari.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sijasema Mkoa wa Mtwara ni mdogo kwa dharau, ila nasema kwa namba za kilometa za mraba. Wilaya ya Kilombero na Bonde la Kilombero ni kubwa zaidi, siyo Mkoa wa Mtwara pekee yake na mikoa mingine mingi tu. Kwa hiyo, Mkuu wa Wilaya yetu anatakiwa kufika maeneo yote hayo, lakini kiukweli gari lake lina matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimekuwa nashukuru hapa kuhusu Mkurugenzi Bi. Zahara ameanza vizuri, alikuta 31% ya mapato ya Halmashauri, amepeleka mpaka 68%, changamoto ni Barabara, hawezi kufika maeneo yote. Kwa mara ya kwanza naona Mkurugenzi wa Halmashauri amekuta milioni 180 za kwenda kununua gari ya Mkurugenzi, akazibadilisha zile pesa akaenda kununua pikipiki 19 za Watumishi wa Halmashauri, Watendaji wa Kata. Sijawahi kuona Mkurugenzi mwenye moyo kama huu. Kwa hiyo, wakati mwingine tunavyowalalamikia hawa watumishi, ni vizuri pia kuwapongeza wanapofanya vizuri kwa kufanya mambo kama haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka haraka nimeona kengele imegonga, nataka kuuliza kuhusu Miradi ya TACTIC, sisi tumo na tuliambiwa mwezi Julai itaanza, sasa Soko jipya la Ifakara Mjini linaanza lini? Watuambie hapa, Stendi mpya ya Halmashauri ambayo ipo kwenye Mradi wa TACTIC inaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu lingine ni kwamba, viongozi wanaopanga ratiba wakumbuke kuja Morogoro Chini kule Kilombero, Malinyi, Ulanga na Mlimba, wasiishie hapo Morogoro Mjini tu, wapange ziara zao kuja kule chini. Siku hizi kuna lami unateleza tu kutoka Mikumi - Morogoro - Mikumi unakuja Kilombero unafika Ifakara kwa lami. Matatizo yapo Ulanga na Mlimba huko, ndiyo kuna shida ya Barabara, lakini kwetu Ifakara pale unafika vizuri sana. Kwa hiyo, tunaomba sana wakipanga ratiba waweze kuja kule ili waweze kuwasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itusaidie gari la Usimamizi Shirikishi la Afya, DMO wangu hana gari. Halafu Ifakara ni Halmashauri lakini Jimbo ni Kilombero, hapa kuna mgongano unataokea sana. Ndiyo maana hata ambulance yetu imetolewa tena ikapelekwa kwenye Jimbo lingine. Naomba wakumbuke kwa kuandika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, DMO wangu hana gari Shirikishi la Halmashauri, halmashauri nyingine zimepata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali na TAMISEMI, wanisaidie kumalizia zahanati ambazo tumejenga na wananchi ya Ifakara, Zahanati ya Kikwawila, Sululu, Lung’ongowe na Msola Station. Wakipata watendaji watupatie, hakuna Watendaji wa Kata na Watendaji wa Mitaa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Muda wako umekwisha.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)