Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Agnes Elias Hokororo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mezani. Kwanza nianze kuunga mkono hoja nisije nikasahau. Pili, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na hasa Mheshimiwa Naibu Waziri mdogo wangu Mheshimiwa Zainab Katimba, sisi tunamwombea. Amepewa hiyo dhamana, atuwakilishe vyema kama wanawake na kama Mawaziri wengine wanawake wanavyofanya kazi. Tunawaamini sana na tunawatakia kila la heri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kwenye Bajeti ya TAMISEMI. Kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu daktari bingwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa nini? Kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wote humu wamesema kwamba utekelezaji wa Ilani kwa kipindi hiki umefanyika kwa asilimia nyingi, lakini sote tunatambua kwamba fedha zilizokwenda kwa ajili ya utekelezaji wa miradi vijijini ile miradi inayogusa wananchi zimekwenda nyingi na miradi inatekelezwa katika kila sekta hivyo imewapunguzia wananchi ile mikikimikiki ya kuchangia kwenye miradi ya maendeleo kwenye maeneo yetu katika mikoa yote kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara sisi pia ni mashuhuda, kuna Mradi Wa Kiwanja cha Ndege umetekelezwa kwa fedha nyingi, Mradi wa Bandari umeboreshwa kwa fedha nyingi, Mradi wa Barabara ya Mnivata – Tandahimba – Newala - Masasi mkandarasi ameshajenga kambi na hivyo tuna uhakika barabara ile inakwenda kujengwa. Ujenzi wa bandari chafu pale Mgao utaanza mwezi Mei, lakini shule maalum walizopata katika majimbo yote Wabunge wa Majimbo na kwetu Mtwara napo ipo kule Nanyumbu. Mradi wa Makonde ambao ulikuwa umeachwa tangu miaka ya 70 safari hii fedha zilienda na mradi unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ramani kubwa ya kutupatia maji wananchi wa Mkoa wa Mtwara kutoka Mto Ruvuma ilikuwa ni ahadi ya miaka nenda rudi. Safari hii umeanza, maji ya Mto Ruvuma watu wa Nanyumbu wataanza kuyanywa na Wilaya nyingine zilizobaki tano katika Mkoa wa Mtwara tunaamini tutayapata. Kwa hiyo naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Watanzania ambao tunaendelea kuwa na imani naye sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti hii Waheshimiwa Wabunge humu kila mmoja akisimama anasema kuhusu uharibifu wa miundombinu na hasa Barabara, naomba nishauri kwenye eneo hilo hilo. Naomba tuangalie kwenye Hotuba ya Waziri ukurasa wa 11 katika utekelezaji wa bajeti ya 2023/2024. Naomba ninukuu kile kipengele cha kumi anasema; “Kuchochea na kuhimiza ukuaji wa uchumi shindani kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla kwa kuwezesha mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuweka mazingira mazuri ya uanzishaji wa viwanda, biashara na uwekezaji hasa katika kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na kadhalika.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunganishe huu utekelezaji wa kazi za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na mpango wetu wa Taifa ambapo Waziri husika alitusomea katika hili Bunge lako Tukufu, kwa namna gani? Lengo la Mpango wa 2024/2025 kama ambavyo umewasilishwa ni kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji uchumi ambao ni jumuishi, unaopunguza umaskini na unaochochea mauzo ya bidhaa zilizoongezewa thamani nje ya nchi. Ili kufikia hili, msukumo utawekwa katika kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini naomba tuunganishe hapa? Ni kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sasa naomba ijielekeze katika urejeshaji wa miundombinu ya Barabara, kwa sababu kama kilimo kiliweza kuchangia katika uchumi kwa 24.7% na kama hatutaunganisha kilimo na barabara, ni kwamba tunaenda kupata seti tupu katika shughuli zetu za kila siku hasa kwa sababu TAMISEMI ndiyo tunaotarajia wafanye uchechemuzi wa shughuli zote za uzalishaji katika Serikali za mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatutafungamanisha barabara na kilimo ni kwamba tunatarajia shughuli za uzalishaji wa kilimo zitapanda kwa sababu upatikanaji wa pembejeo utakuwa ghali lakini bei ya chakula itapanda, mfumuko wa bei utaongezeka. Kwa msingi huo, hivi vitakuwa na athari katika ukuaji wa uchumi ambao kwa kipindi hiki tumeona ulikuwa unaendelea kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba, kwa sababu kwa bajeti iliyopita TARURA ilitengewa zaidi ya shilingi trilioni moja lakini walipokea kwa asilimia 45.7 tu. Sasa kwa sasa hivi tukianza tena kuweka na mambo mengine, tusipojikita kwenye urejeshaji naungana na Waheshimiwa Wabunge wote waliosema fedha za dharura. Naomba bajeti hii ingejikita kwenye urejeshaji wa barabara ili tuweze kufungamanisha na Mpango wa Maendeleo wa Taifa ili tuweze pia kuhakikisha kwamba Sekta ya Kilimo inachangia katika ukuaji wa uchumi kama ambavyo imekuwa ikifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusipofanya hivyo, hatujui vijijini watabakiwa na chakula kidogo kwa sababu pia mashamba yamejaa maji lakini hata hicho kidogo kukisafirisha sijui watu wa mjini watafanyaje. Hivyo vyote ili viweze kufungamana lazima turejeshe barabara. Sasa sisi kule kwetu na maeneo yote ambayo yanafanya uzalishaji barabara zimeharibika, lakini niki-cite kule kwetu hata kutoka Chiwale kwenda Masasi na maeneo mengine, Morogoro, Njombe, Ruvuma na kote kule ambako kuna barabara za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kila Mbunge anavyosema hapa ni muhimu tukafanya urejeshaji ili TARURA ikafanya hiyo kazi yake na tukaweza kufungamanisha kilimo, kwa sababu tumeona sekta nyingine kama ujenzi ilichangia kwa 13.6%, lakini ukiona kilimo 24.8 ina maana tutakuwa tunafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo naomba kuchangia ni umaliziaji wa maboma. Wananchi walihamasika na walitumia nguvu kubwa katika kuhakikisha maboma hayo yanajengwa. Ni vyema Wizara badala ya kuanza vitu vipya ikajikita pia sehemu ya fedha baada ya kupeleka kwenye urejeshaji wa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa Wizara badala ya kuanza vitu vipya ikajikita pia baada ya kupeleka kwenye urejeshaji wa miundombinu ya barabara, sehemu ya fedha ikaenda kwenye umaliziaji wa maboma ya shule, zahanati na vituo vya afya. Kama kule Mtwara tungepata fedha kwa ajili ya kumaliza Vituo vya Afya vya kule Nyundo, Nanyamba, Nandwahi, Newala na Magomeni pale Mtwara. Pia Masasi kule Lukuledi na maeneo mengine ambayo sijayataja. Hiyo ifanyike kwa nchi nzima badala ya kuanza miradi mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la umaliziaji wa maboma ni shule pamoja na nyumba za watumishi, kwa sababu tunajua rasilimali watu ndiyo tunaitegemea katika kusukuma shughuli za kimaendeleo katika maeneo ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo naishauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa sababu ndiyo ina dhamana kubwa ya kushughulika na wananchi kule, ni kutekeleza ahadi za viongozi. Katika awamu mbalimbali kumekuwa na ahadi za Viongozi Wakuu wa Nchi katika maeneo mbalimbali. Sasa hizi ahadi zikibaki za Awamu ya Kwanza, ya Pili, ya Tatu, ya Nne, ya Tano na ya Sita, ni muhimu sasa TAMISEMI ikahakikisha hizo ahadi zinatekelezwa. Kwa hiyo, TAMISEMI wana kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba shughuli za maendeleo zinaendelea kufanyika kwa mujibu wa kazi ambazo wamepangiwa, lakini hili nalo la kuhakikisha ahadi za viongozi zinatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo zahanati, vituo vya afya, ujenzi wa shule na barabara katika maeneo korofi. Badala ya kusubiria lami kilometa moja, tukatumia pengine cement, tukaweka ule mtindo wa zege; hiyo inaweza ikafanywa na TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni vitu ambavyo kimsingi wanaweza kuvifanya katika kipindi hiki badala ya kuanza vitu vipya. Ni muhimu tutakapofika 2025, basi ahadi zote za viongozi ambazo zimeratibiwa katika Serikali za Mitaa, halmashauri, vijiji, wilaya na mikoa zikawa zimekamilika na hivyo kuwafanya viongozi wetu wakuu kutokuwa na madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, natambua tunakwenda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kwa hiyo ni imani yangu kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea kabisa kuhakikisha inaratibu vyema zoezi hilo, pamoja na kwamba sheria iliyotungwa hapa inaipa Tume ya Uchaguzi huo wajibu na hasa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi na wao wanajitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili tuweze kuchechemua maendeleo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.