Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa fursa uliyonipa ili kuchangia kwenye Wizara hii ya TAMISEMI. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa namna ambavyo anatupa uhai. Naungana na Waheshimiwa Wabunge wote waliozungumza kwa kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwetu sisi Wanamwanza tunafurahia sana hasa katika utekelezaji wa ile miradi ya kimkakati ambapo hadi leo hakuna hata mmoja uliosimama, yote inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo meli kubwa kule inaendelea, uboreshaji wa viwanja vya ndege, standard gauge, Daraja la Busisi na mengine mengi. Pia ukija kitaifa Bwawa la Mwalimu Nyerere nalo kazi inaendelea na hata ukiangalia kwenye bomba la mafuta, hakuna kilichosimama. Anastahili kupewa maua yake kwa sababu tunajua miradi hiyo ikikamilika Watanzania tutapata fursa nyingi za kiuchumi na ajira zitaongezeka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuwapongeza Mkuu wetu wa Mkoa ambaye ni mgeni. Huyu aliyekuja na wale waliotoka wote ni wazuri na wanakuja kufanya kazi. Nampongeza sana DC wangu, Ndugu Hassan Masala, amewahi kuwa Mbunge hapa, naye kazi anayoifanya ni kubwa, kwa hiyo Mbunge nina amani. Vilevile timu nzima ya Manispaa ya Ilemela, madiwani, watendaji na mkurugenzi wote tunashirikiana. Kwa hiyo nawashukuru kwa namna wanavyowezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia masuala kadhaa hasa katika vile vipaumbele ambayo Mheshimiwa Waziri amevizungumza. Naanza na suala zima la miundombinu. Katika miundombinu nataka kuwaambia TAMISEMI, wananchi wamefanya kazi kubwa katika Jimbo la letu la Ilemela na hakuna mradi ambao umesimama katika suala zima la huduma za jamii. Kwa hiyo katika maboma ambayo yapo, tunayo maboma 220, yanahitaji pesa shilingi 3,708,000,000 na haya yote yana nguvu za wananchi na pamoja na Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukianza kuangalia kwenye sekta ya elimu tuna madarasa ya kutosha, maabara, nyumba za walimu na mabweni. Pia, ukija kwenye afya tunayo maboma ambayo yanasubiri kumaliziwa. Ukija kwenye Ofisi za Serikali za Mitaa, kila mtaa wanafanya kwa ushindani, wamejenga maboma ambayo yanasubiri kumaliziwa pamoja na kata na yote unayoangalia kuna nguvu za wananchi na nguvu za Ofisi ya Mbunge. Tunachosubiri ni Serikali kumalizia. Tunaomba sana ili tusiwavunje moyo hawa wananchi ambao wanajitolea katika kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije kwenye suala la miundombinu ya TARURA. Kwanza nimpongeze Mkurugenzi wa TARURA, Ndugu Seff, anafanya kazi kubwa na nzuri sana na tunaona namna inavyokwenda. Tunachohitaji tu ni kuwezeshwa katika mikoa yetu. Kwa Mkoa wa Mwanza mimi nina malalamiko kidogo. Meneja wa TARURA amekuwa akihamishwa mara kwa mara. Ndani ya muda mfupi tuna Mameneja wa TARURA kama watatu wanapita. Anakaa kidogo anaondoka, anakaa kidogo anaondoka. Hiyo, inafanya pia mtiririko wa kazi usiende vizuri, lakini tunaye Engineer Sobe, anafanya kazi yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa namna ilivyokuwa imejipanga kwa mujibu wa ilani ya utekelezaji. Walikusudia kujenga kilometa 24,493 lakini wakaenda kwenye kilometa 41 na hizi ni barabara za changarawe. Kwenye barabara za lami wakajikita kwenye 2,025 mpaka kufikia pengine 3,100. Sasa upande wa bajeti tunavyoweka tuna underestimate sana kwenye suala la lami. Ukiangalia barabara za mitaani kule vijijini, uki-base kwenye barabara za changarawe, tunapopata mvua ya namna hii, athari inakuwa ni kubwa sana. Ningeomba sana takwimu zetu zibadilike, tuelekeze zaidi katika barabara za lami. Hata kama tutapata kilometa chache lakini walau zinakuwa ni imara kuliko kujikita kwenye barabara za changarawe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimkumbushe Mheshimiwa Waziri ile ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilometa 12. Tunaisubiri sana na ilikuwa inatakiwa itengenezwe ndani ya mwaka huu wa fedha, lakini mpaka leo hakuna dalili yoyote. Naomba sana na hili tuliweke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye bajeti naomba sana tuangalie; Ilemela ni manispaa na Mwanza ni jiji, lakini bajeti zetu ni ndogo. Huwezi ukaweka bajeti ya bilioni 2.1 kwenye manispaa yenye mzunguko wa barabara za kilometa 1,920, lakini zilizoko TARURA ni kilometa 875. Hizo kilometa 1,045 zinatengenezwa kwa bajeti ipi? Naomba sana tuangaliwe katika bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, japo kuwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge tunapowatolea mifano kidogo wanakuwa hawajisikii vizuri, lakini ukiangalia Ilala ambako ni kwa Mheshimiwa Naibu Spika wanapewa bilioni 29, ukienda Tanga wana bilioni sita. Ukienda Dodoma wana bilioni 20 na haya ni majiji, ni manispaa. Inakuwaje bajeti inakuwa na variation kubwa zaidi. Kuipa Ilemela bilioni mbili na milioni mia moja si sawa, tunaoneana vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nizungumzie suala la utawala. Kwenye suala la utawala baada ya sensa ya mwaka uliopita, Ilemela sasa ina watu 509,687, ina tarafa moja, mitaa 171 na kata 19. Afisa tarafa ndiye huyo huyo hana tofauti na DC katika kufanya kazi. Tunaomba sana katika suala zima la kugawa maeneo ya utawala tuangalie eneo letu la Ilemela na tuangalie Nyamagana ambayo nayo ina kata 18 na tarafa moja. Utawala unakuwa ni mgumu na namna ya kusogeza huduma inakuwa ni ngumu maana kata moja unakuta ina watu 45,000 sawa na wilaya zingine ambazo hatuwezi kuzitaja, lakini unakuta ina watu wasiozidi 50, wana tarafa kama tatu hadi nne. Sasa wilaya yenye watu 500,000 inakuwa na tarafa moja. Kidogo siyo sawa katika suala zima la utawala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine naomba nizungumzie suala la afya. Tunamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumepata vituo vya afya vipya viwili. Hata hivyo, tuna vituo vya afya vitatu na kimoja kilijengwa mwaka 1973 mpaka leo hakina miundombinu ya kutosha. Kituo hicho cha afya mpaka leo hakina wodi ya wanaume, wana-share na wanawake. Kituo hicho cha afya hakina maabara, nyumba ya mtumishi, fence na hakina mortuary. Sasa namna ya uendeshaji ni ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kituo kingine ambacho pia ni kipya, lina OPD peke yake, lakini hakina miundombinu mingine. Ukienda Kituo cha Kayenze ni kipya nacho hakijakamilika. Naomba sana Serikali ikamilishe vituo hivi ili tuweze kupata huduma sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la matumizi ya ardhi. Tunajenga majengo mazuri sana kiasi kwamba kila ukiyaangalia yanapendeza, lakini tunatumia vibaya ardhi. Naomba sana ramani zetu za majengo ya hospitali, zahanati, vituo vya afya na ya shule yaangaliwe upya. Basi tuone namna ya kwenda juu zaidi badala ya kuweka ya mtawanyiko kwa sababu ardhi haiongezeki na sisi tunaitumia vibaya, naomba tuitumie vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hilo hilo la ardhi, wakati tuko Mwanza siku ile Mheshimiwa Rais amekuja kule tulizungumzia suala la changamoto ya fidia. Kuna shule nyingi za kata zilizojengwa katika kata zetu zote, katika ujenzi huo maeneo ya wananchi yalitwaliwa, kwa hiyo kuna madeni ambayo wananchi wanadai. Sasa inakuwa ni ngumu sana kwa sababu ni muda mrefu wanadai hasa katika zile shule za kata na katika maeneo mengine ya miundombinu ambayo tumeweka tunakuta wananchi wanadai. Naomba sana tuone namna bora ya kuweza kuwalipa fidia zao ili angalau wawe na moyo wa kutoa maeneo yao wakati mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la upungufu wa watumishi. Kwenye mchango wa maandishi nimeainisha suala la upungufu wa watumishi kiidara, lakini pia na kwenye miundombinu nimeainisha namna ambavyo maboma yamejengwa. Sasa nataka nizungumzie tu suala la watumishi, tuna upungufu wa watumishi 28%. Tulitakiwa kuwa na watumishi 4,460, lakini tunao 3,189, kwa hiyo tuna upungufu wa watumishi 1,271.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia tumepata hospitali ya wilaya lakini haina daktari bingwa hata mmoja, ndiyo upungufu wenyewe wa watumishi huo. Watu wa pharmacy tunatakiwa kuwa nao 26, lakini tunao saba kwa wilaya nzima na wasaidizi 46, lakini tunaye mmoja. Kwa hiyo unakuta kazi pia inakuwa ni ngumu sana. Kwa hiyo, naomba sana, katika suala zima la upungufu wa watumishi nimeainisha kiidara na yote yako katika mchango wa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima ambalo tunataka kuzungumzia ni suala la mapato. Tumetoa maelekezo kwa baadhi ya halmashauri ambazo zinapata mapato ya kutosha, pengine kuanzia bilioni tano kwenda juu. Hata hivyo, tukumbuke pia katika halmashauri hizo hizo zina matumizi ambayo yanahitajika kufanyika pale katika halmashauri zao. Sasa unapokuta wana madeni makubwa na wao wameambiwa hawawezi kupata ruzuku ya utawala kutoka Serikali Kuu, inawawia vigumu kulipa madeni yaliyopo. Tunaomba hili liangaliwe upya, kwa sababu katika utendaji tunazipa kazi halmashauri ambazo zina madeni makubwa wanayotakiwa kulipa kutoka kwenye pesa zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa suala la 10% ambayo ni ya akina mama. Naomba sana katika huu utaratibu mpya unaokwenda kufanyika elimu kwanza itangulie kwa wananchi wetu ili waweze kuelewa huu mfumo mpya wa 10% unavyokwenda kutumika, namna tunavyo-link na benki na namna ya registration inavyofanyika kwa wafanyabiashara. Wengi inawachanganya, wengi inawachanganya na kile kipande cha shilingi 20,000 kilichokuwepo cha mwaka mmoja na hiki cha sasa cha miaka mitatu kwa 20,000. Wanatakiwa wapate tafsiri nzuri ili hata wanapoingia katika ile mikopo wajue kabisa nini masharti yake na hata akiwa kwenye kikundi anatakiwa afanyaje... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Dkt...
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru kwa kunipa fursa na naunga mkono hoja. (Makofi)