Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja ambayo ipo Mezani kwetu kuhusu Makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambayo kimsingi naweza kusema ndiyo ya vijiji vyote, vitongoji na mitaa yote nchini. Ni Wizara kubwa, Wizara ambayo inagusa maisha ya wananchi kule ndani kabisa vijijini. Kwa hiyo, nataka niseme Wizara hii ni muhimu na ninaona leo nisimame kwa ajili ya kuweza kuchangia hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nachukua nafasi hii kwa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwemo kutoa maelekezo mbalimbali ya kuhakikisha kwamba fedha zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo ambayo ipo kwenye vijiji vyetu, mitaa yetu pamoja na vitongoji vyetu. Kwa hakika, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana, amefanya kwenye Wizara nyingi, lakini pia kwenye Wizara hii amepeleka fedha nyingi sana, nasi ambao tunatoka Wilaya ya Ikungi, Jimbo la Singida Mashariki ni mashahidi na nitasema kwa uchache wake hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mohamed Mchengerwa kwa kazi nzuri anayofanya. Kwa hakika kwenye maeneo yetu anatajwa kwa wema sana na hata mafuriko yanayotokea pale Rufiji wanandelea kumwomba Mungu yapite salama ili uweze kurudi tena mwaka 2025 kwa sababu, unamsaidia sana Mheshimiwa Rais katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika ile kauli yake aliyoitoa juzi wakati anaongea ofisini, alisema; “watu wenye brains huwa wanapigwa vita kwenye maeneo.” Wengi wamekupa big up kwamba unajua wajibu wako na imekuwa ni eneo la kuonesha uwajibikaji kwa vitendo. Kwa hiyo, maana yake ni wale wenye brains walindwe ili waweze kuiongoza nchi hii vizuri. Tunakupongeza sana kwa kauli hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana mdogo wangu Mheshimiwa Zainab Katimba kwa uteuzi wake kuwa Naibu Waziri, anafanya kazi vizuri. Juzi amejibu vizuri swali langu la barabara, sitasema maneno mengi, lakini naamini amemwambia Mheshimiwa Waziri yale madaraja yangu yajengwe ili kuhakikisha kwamba Barabara za Jimbo la Singida Mashariki zinakaa vizuri. Nahitaji kiasi cha fedha kama shilingi bilioni tatu tu ili tujenge yale madaraja na barabara zipitike ili mwakani wakati wa kwenda kumwombea kura Mheshimiwa Rais iwe tunapita mbele kwa mbele bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nampongeza sana ndugu yangu, Mheshimiwa Dugange kwa kazi nzuri anayoifanya. Amekuwa na Mheshimiwa Waziri kwa muda wote na kwa kweli wanafanya kazi nzuri pamoja na uongozi mzima; Katibu Mkuu na wenzake wote. Kwa hakika ili ukamilishe Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni lazima uwataje Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi, hawa ndio wanafanya kazi ya kusimamia maelekezo yote yanayotolewa na Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kwa dhati kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Mkuu wa Mkoa bora, Mheshimiwa Halima Dendego, mama mlezi wa wana. Hakika mama yule toka amekuja ametuunganisha kwa pamoja Wanasingida na alipofika Waheshimiwa Wabunge tumekaa naye, tumezungumza mambo ya maendeleo kwa maslahi ya Mkoa wa Singida. Tunasema mama ahsante, tunasema Mheshimiwa Waziri ahsante nasi tutaendela kumuunga mkono Mheshimiwa Halima Dendego tufanyenaye kazi kwa sababu ameanza na mguu mzuri kwa Mkoa wetu wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Thomas Apson, naye ni kada mpiganaji mzuri kabisa, anasimamia vizuri maendeleo ya Wilaya ya Ikungi. Vilevile kipekee nampongeza Ndg. Justice Kijazi ambaye ni Mkurugenzi wetu, anafanya kazi nzuri sana akishirikiana na watendaji wenzake. Ndiyo maana mnaona Ikungi ya leo siyo Ikungi ya jana kwa sababu fedha zikija zinakwenda zilikolengwa, maendeleo yanaonekana na wananchi wanashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya, nashukuru sana kwa fedha tulizopata. Mwaka wa fedha uliopita, huu unaokwenda kumalizika, tumepokea takribani shilingi bilioni 15 katika Wilaya yetu ya Ikungi katika Jimbo la Singida Mashariki, haijapata kutokea. Sisi tunaposema tunamshukuru Mheshimiwa Rais, tunasema kwa vitendo kwa sababu, tunayaona. Hatukuwahi kuzidi shilingi bilioni tatu huko nyuma, leo tunapata shilingi bilioni 15, kwetu ni jambo kubwa sana, ndiyo maana tunasema hatuna sababu ya kuelekezwa, tunasimama na Mheshimiwa Samia mpaka kieleweke kuhakikisha kwamba tunampa kura za kutosha. Wapiga kelele hawana nafasi tena kwa sababu, vitendo vinaongea kuliko maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejengewa madarasa 128 mapya katika shule za msingi, katika shule zetu za sekondari tumeongezewa madarasa 20, lakini kama haitoshi, tumejengewa shule mpya mbili, Matongo na pale Nkuhi zaidi ya shilingi milioni 500 zimelala pale, na shilingi bilioni moja tumejengewa shule mbili mpya. Tukisema shule mpya, maana yake hatukuwa na jengo lolote kutoka ardhi mpaka shule. Hatuwezi kuacha kumsemea Mheshimiwa Rais kwa kazi aliyotufanyia. Leo watoto wanakwenda umbali mfupi kufuata masomo, kitu ambacho ndiyo lengo la kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu iliyo bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumepata shilingi milioni 590 tumejenga shule mpya ya msingi ambayo iko pale Ikungi kutoka Shule Mama ya Ikungi mchanganyiko. Shule ile imekuwa kama ni chuo na siyo shule ya msingi. Ni jambo kubwa ambalo sisi tunashukuru na kwa hakika tutakuwa wachoyo wa fadhila bila kumshukuru Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ni mingi, kwenye eneo la barabara tulikuwa hatuna lami, lakini sasa tuna lami pale mjini. Juzi tumepata kilometa moja ya lami, mkandarasi yuko site anaendelea na kazi. Taa za barabarani zimewekwa pale, Mji wa Ikungi leo una alama, ukifika unaiona Ikungi kwa sababu ya namna ambavyo Mheshimiwa Rais ameamua kutuletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelekezwa na Vitabu vya Mungu, Biblia inasema kwamba, “moyo usiokuwa na shukrani, unakausha mema yote,” lakini pia kushukuru ni kupata thawabu kwa sababu, unatambua kazi ya mwenzako. Pia, inasemwa hakika, kama huwezi kumshukuru unayemwona, je, Mwenyezi Mungu ambaye humwoni, utamshukuru vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maana yake ni kwamba kushukuru ni uungwana, ni jambo la kawaida kabisa. Ninaamimi huo ndiyo utaratibu wa Kitanzania. Hatuwezi kufundishwa utaratibu mpya, huo ndiyo utamaduni wetu na ndiyo uungwana wetu, lakini wanasema kushukuru ni kuomba tena, alisema Mzee Mkapa. Pamoja na haya mafanikio tuliyoyapata, lakini tuna mambo machache ya kushauri ili tuhakikishe tunaisaidia Wizara na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitashauri kwenye eneo la watumishi ambapo tumekuwa na upungufu, nitaongelea habari ya vitendea kazi kwa maana ya magari, nitaongelea kidogo ukaguzi wa fedha kwa maana ya internal auditor kwenye halmashauri zetu na nikipata wasaa nitaongelea barabara vijijini na mwisho nitaongelea kidogo maslahi ya Madiwani pamoja na Wenyeviti wetu wa Mitaa na Vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwenye eneo la watumishi. Mheshimiwa Waziri eneo la watumishi; rasilimali watu ni nyenzo muhimu katika kazi. Tukiwa na rasilimali ya kutosha ya watu itatusaidia kusukuma shughuli za maendeleo. Katika Halmashauri yetu ya Ikungi tunahitaji kuwa na watumishi 4,664, lakini watumishi tulionao ni 2,369 hatuna watumishi 2,292 maana yake ni asilimia 50 ya watumishi wanaohitajika, hatuna. Maana yake ni kwamba, kuna watumishi wachache ambao wanabeba mzigo kwa niaba ya watumishi wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka kupata maendeleo ya haraka kule vijijini, kwenye mitaa yetu, tuongeze watumishi. Ninaamini kazi nzuri inafanywa, tangu Mheshimiwa Rais ameingia katoa vibali vingi. Ninaamini tukipata watumishi tutakuwa na mgawanyo kwenye halmashauri zetu. Naomba Halmashauri ya Ikungi ili twende vizuri tuongezewe watumishi wa kutosha ili kuhakikisha kwamba fedha zinazokwenda kule na zinasimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo ni kwenye eneo la Idara ya Sheria, tunahitaji watumishi wanne, lakini tunaye mtumishi mmoja. Je, mambo ya Kisheria kwenye vijiji vyetu huyu mtumishi mmoja atafanyaje kazi? Kwa hiyo, naomba sana tuangalie kwa jicho hilo kuhakikisha kwamba tunapata watumishi wanaotakiwa na ikama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, Idara ya Fedha, ambayo leo tunasema ndiyo inaenda kusaidia mambo mbalimbali… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa. Ni kengele ya pili hiyo.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)