Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo kuwa mchangiaji wa kwanza katika hoja hii iliyopo mezani. Nianze kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuunga mkono hoja, nami nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa miradi mingi katika Jimbo langu la Kalenga ambayo imetekelezwa na TAMISEMI katika maeneo mbalimbali zikiwemo barabara, shule, zahanati na vituo vya afya. Kwa kweli kazi kubwa imefanyika, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Mawaziri wanaomsaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kwenye shukrani, pia namshukuru Rais kwa mabadiliko aliyoyafanya ya uongozi. Tulikuwa na RC mzuri sana pale, Mheshimiwa Halima Dendego lakini sasa ametuletea makomredi wengine wawili wazuri, tayari tumeshakaa mezani na kupanga mipango yetu ya namna tutavyoendesha mkoa wetu. Naona nuru kubwa ipo mbeleni na mambo yaliyopo mbele ni mazuri zaidi. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kumleta comrade Serukamba pamoja na Ndugu Kheri James katika mkoa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda upande wa TARURA, kazi nyingi zimefanyika, nasi kwa kweli katika CEO ambao ni maarufu sana katika Bunge hili, nafikiri Seff ni CEO maarufu sana. Ni maarufu siyo kwa sababu anatekeleza miradi yote tunayomwambia, lakini ana sifa moja ya open door policy kwa Wabunge. Ukienda pale ofisini kwa Engineer Seff ataacha anachofanya na atakusikiliza very much attentively hata kama hatekelezi sisi tunapata tu matumaini. Kwa kweli ndiyo maana tunaomba sana Engineer Seff tumalizane naye 2025 halafu tuanze naye tena 2026, haitakuwa mbaya, hata kama kwa mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambayo tulikuwa tumeahidiwa wakati tunasaini mkataba wa kujenga barabara ya kutoka Uwenda kwenda Mgama. Naishukuru sana Serikali kwa kujenga barabara hiyo ya vijijini kwa kiwango cha lami, ilikuwa ndoto ya siku nyingi, lakini tuliahidiwa pia kujengewa kipande kidogo cha barabara kinachokwenda kwenye Makumbusho ya Mkwawa. Tukiangalia heshima ya Mkwawa katika nchi hii na wageni wanaokuja pale, kipande cha kilometa moja mpaka leo kutokujengwa kwa kweli siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo hili liliahidiwa na Waziri aliyekuwepo wakati huo Mheshimiwa Angella Kairuki mbele ya Katibu Mkuu Ndugu Ndunguru, Engineer Seff na mbele ya Engineer Mativila, mpeleke fedha mkatengeneze kile kipande, ni kidogo sana. Mkikaa pale ofisini mnaweza mkafanya maamuzi haraka haraka mkaenda kurekebisha na haya mambo yakaisha na tukawa na kipande kizuri ambacho watalii wakienda kuangalia lile fuvu pakiwa panang’aa na tutaonekana watu tuko serious, si ndiyo! Kwa hiyo, hili naomba lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna daraja moja muhimu sana ambalo litakuwa ni daraja la mkato linalounganisha Kata mbili, lakini kimsingi linaunganisha majimbo mawili. Ukitoka kwenye hizi Kata za Mahuninga, Ruaha National Park unakwenda Pawaga kulima mpunga, lazima uzunguke mjini, lakini hapa katikati ukifika Nzihi, unakatisha Kijiji kinachoitwa Kipera, unatokea Kiwele unaingia Pawaga na biashara kubwa ya mashamba ambayo iko kule kwenye mifereji ya karibu shilingi bilioni 54 ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya pale. Kwa hiyo, kama tukitengeneza hili daraja itakuwa ni rahisi sana kwa hawa wakulima wanaotoka maeneo ya Idodi, Mahuninga na Mlowo kukatisha Nzihi, Kipera na kuingia Pawaga. Hili nalo naomba japo tulishaongea na ndugu yangu Engineer Seff, halipo kwenye bajeti ya mwaka huu, lakini naomba alifikirie katika zile dharura, akipeleka pale halitakuwa jambo baya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upande wa shule, unajua tumepeleka umeme kwenye shule zote, hivyo unakuta kila shule inahitaji printer na photocopy. Kwa hiyo, unakuta mara nyingi Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukinunua hizi printer na photocopy ili kupeleka kwenye hizi shule. Tunaomba Serikali sasa kwa kuwa miundombinu ya umeme imeimarika, waweke mpango wa shule zote kupeleka hizi printer na photocopy na kusaidia kuchapisha mitihani wakiwa hapo hapo shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kidogo pale kwenye TARURA. Pamoja na kazi nzuri ambayo TARURA wamekuwa wakiifanya, kumekuwa na changamoto wakati mwingine kwenye hizi barabara hususan wakati wa mvua nyingi, kuweka kifusi ambacho kinateleza. Kwa mfano, tuna barabara moja ambayo inatoka Ifunda – Mibikimitali, kuna barabara nyingine Masaka kati ya Saadani kwenda Makota, tunatengeneza vizuri lakini kwa sababu ni maeneo yenye utelezi, ikifika wakati wa mvua barabara hazipitiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, naomba wakati mwingine ni vizuri kama barabara ina kilometa tano, basi fanya angalau tatu kwa kiwango kizuri cha kokoto halafu baadaye uje umalizie, kuliko kuweka yote matope halafu baadaye tunawazuia watu wasipite inakuwa siyo jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye zahanati kumekuwa na juhudi kubwa sana, vijiji vingi vimekuwa vikijenga zahanati, na mwongozo unasema mpaka tuezeke. Kwa sababu ya hali ya kiuchumi napenda kushauri kwamba, Serikali ipokee pale wananchi wanapofika kwenye boma. Tunayo maboma mengi ambayo yamejengwa, lakini hayajamalizika kwa sababu hali ya kiuchumi siyo nzuri. Kwa hiyo, Serikali ione sababu ya kutusaidia pale tunapofika tu kwenye boma wao waendelee mpaka kumalizia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu siyo sera ya Serikali kujenga mabweni kwenye shule za kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne, lakini kwa sababu wanafunzi wetu wamekuwa wakitoka kwenye maeneo ya mbali sana, wananchi waliamua kujenga mabweni katika shule mbalimbali. Asubuhi dada yangu, Mheshimiwa Tendega alizungumzia habari ya Shule ya Lumuli kwamba walijenga mabweni mawili pale na sasa ni miaka 12, mimi nimepeleka mabati 450 pale, wenzangu wa NMB walinisaidia mabati 300 na mengine 150 nilipeleka kutoka kwenye Mfuko wa Jimbo. Sasa Serikali ione ni namna gani inaweza kutusaidia tukamaliza pale ili kuunga mkono juhudi za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua pengine Serikali inaweza ikawa inakwepa kujenga mabweni mengine kwa sababu itaji-commit kuanza kulisha, sisi tumejiwekea utaratibu wetu wa kukusanya chakula, ninyi mkitumalizia, sisi tutaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa kwenye Mfumo wa NeST. Hivi karibuni kuna supplier mmoja alikuwa ananiambia kwamba mimi nitashindwa kulisha hizo shule zenu kwa sababu nina siku tatu nashindwa kuingia kwenye mifumo. Sasa hii mifumo ningependa sana twende nayo polepole. Kwa hawa suppliers wetu ambao wako vijijini, hawajui namna ya kutumia hii mifumo. Wakati wanazoea mifumo na mitandao yetu inaendelea kuimarika, turuhusu ule utaratibu wa zamani uendelee kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ku-transform manual kwenda kwenye digital, nafikiri tunachelewa sana. Kwa hiyo, naomba twende na hii mifumo polepole, turuhusu hawa suppliers mahali ambapo mifumo haifanyi kazi hasa huko vijijini kuwe na njia nyingine mbadala ambayo watu wanaweza wakaendelea ku-supply. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la vituo vya afya, tunaishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya. Hata mimi katika Jimbo la Kalenga nimepata vituo vya afya vitatu na sasa nina vituo vya afya sita, maana yake ni asilimia 100. Kwa hiyo, Serikali imefanya kazi kubwa, lakini bado tuna maeneo ya pembezoni na tulikuwa tumeiomba Serikali ione namna gani inaweza kutusaidia. Tumejaza fomu na Serikali ikatuahidi kwamba itatuletea. Sasa, vile vituo ambavyo tuliomba, basi tuendelee kupata fedha ili tuzogeze huduma karibu zaidi na wananchi hasa katika yale maeneo ya pembezoni. Tukifanya hivyo, mambo yetu mwaka 2025 yatakuwa mazuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata sasa mambo yetu ni mazuri, lakini tukiongeza kwa mfano, niliomba kituo cha Kihanga kiko pembeni kabisa, lakini tuna ahadi nyingine ya Katibu Mkuu wa Chama katika Kata ya Lyamgungwe, kama tukiletewa itakuwa ni jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mwenyekiti wa Mazingira, pia TAMISEMI ni sekta mtambuka, inahusika na mambo yote. Kama tunavyojua, suala la mazingira limekuwa ni jambo linaloleta janga la mabadiliko ya tabianchi duniani. Sasa tunafahamu hali hii imetokana na ongezeko la joto duniani na kila mwaka inazidi kuongezeka, mwaka huu inaonekana limeongezeka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii agenda ya kupanda miti wenzetu wa TAMISEMI kwa maana ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Maafisa Tarafa waichukulie serious kwa sababu miti kwa asili yake inapunguza joto. Pia kwenye maeneo haya ya mmomonyoko nilishauri na ninafahamu kwamba kule kwetu Iringa kuna mianzi, hii mianzi ni maarufu sana kwa kushika ardhi, ukipanda kwenye korongo, inalifukia kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu Mungu alitupatia mianzi katika nchi hii, tungechukua hiyo kama trial katika yale maeneo ambayo mianzi inakubali, ni nzuri sana kushika mazingira. Ukipanda mianzi, unazuia kabisa mmomonyoko wa ardhi. Kwa hiyo, hili lizingatiwe, wenzetu wanaweza wakasimamia hili na mambo yakaenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika vituo vya afya vya zamani ambavyo vilijengwa miaka ya nyuma vilikuwa havina mochwari. Kwa mfano, mimi nina Kituo cha Kiponzelo na Kituo cha Nzihi, lakini hatukujenga wodi za akina baba. Jamani siku hizi akina baba nao wanaumwa sana, pengine zamani tuliwapendelea akinamama kwa sababu ya kazi yao ile nyeti ambayo Mwenyezi Mungu aliwapa, lakini ni muhimu sasa tukaangalia na akina baba. Serikali ione namna gani itatuletea mochwari kwenye hivi vituo pia, itujengee wodi za akina baba.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)