Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyoweza kumimina miradi mingi kwenye Majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge hawa ni mashahidi hasa kwenye Jimbo langu la Tunduru Kaskazini, katika awamu zote, hii Awamu ya Sita kwa kweli miradi imemiminika kama maji yale yaliyoleta maafa kule Rufiji. Baada ya kusema, hayo naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja ya watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la watumishi limekuwa ni kero kubwa kweli katika Wilaya yetu ya Tunduru. Ukienda upande wa watumishi wa afya na watumishi wa elimu, ni tatizo kubwa mno. Kwa mfano, tukienda kwa watumishi walimu wa sekondari, utakuta mahitaji ya walimu wa sekondari ni tofauti na walimu waliopo. Nitakupa mfano wa sekondari kama tatu tu, kwa mfano, Shule ya Sekondari Tunduru, mahitaji ya walimu ni 70 lakini walimu waliopo ni 22 tu, na pungufu hapa ni walimu 48. Ukienda Shule ya Sekondari ya Mataka, mahitaji ya walimu ni 65, lakini waliopo ni 29 tu, upungufu ni 36. Ukienda Sekondari ya Nandembo, mahitaji ya walimu ni 61, waliopo ni 26, upungufu ni 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii nimechukua shule tatu tu kama mfano, lakini shule hizi zote ukienda labda Nandembo, Mgomba, Mtutura, Muwesi, Nakapanya, Frank Weston, Namiungo, Kungu Sekondari, Tinginya Sekondari, Mindu Sekondari, Kidodoma Sekondari, Nampungu, Maji Maji na Ligunga Sekondari mahitaji ya walimu kwa shule hizi zote ni 561 na waliopo ni 292, upungufu hapa ni 269. Hapa utagundua ni nusu ya walimu waliopo, hawapo. Hapa ndipo tunapokwenda kuona elimu hii inakwenda kushuka kwa sababu ile ikama haikamiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tumekuwa tukisikia wakisema kuna mdondoko wa elimu, lakini kuna sababu nyingi zinaelezwa, ila ukiangalia vizuri sababu namba moja kama tutaweza kuiangalia ni upungufu wa walimu. Upungufu wa walimu unasababisha mdondoko wa wanafunzi. Hili ni lazima tuliangalie kwa umakini sana na kuhakikisha walimu wanakwenda. Pia Elimu Msingi, ukiangalia mahitaji ya walimu walitakiwa wawe 225, waliopo ni 63 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala ambalo nalo ni tatizo kubwa kwa hawa watumishi. Kuna tatizo kubwa la walimu kwenda kuripoti na kuhama. Nimekuwa nikizungumza sana hapa Bungeni mara kwa mara na ilifikia wakati nikaomba angalau sisi wananchi wa Tunduru tupewe kibali maalumu cha kuajiri walimu wa kule kule Tunduru ili kukwepa hawa walimu wanaohama. Mfano mmoja, kutoka mwaka 2022 mpaka 2023 tulipokea ajira mpya walimu 225 lakini waliohama ni 63, waliostaafu ni walimu 52. Utaona hapa ni kwamba nusu ya walimu walioripoti wamehama, sasa hii elimu hapa itapatikana vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna tatizo moja ambalo wenzetu wa TAMISEMI watusaidie, Mkurugenzi pamoja na Wakuu wa Idara ya Elimu, wakipata barua angalau wanazificha ficha na kuziweka chini ya madawati huko ili wasiwahamishe wale walimu kwa sababu wanaona wamehama kwa wingi mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta kuna waraka unatoka TAMISEMI unaowataka wawaruhusu wale walimu kuhama, wakipewa ule waraka hawawezi tena kuzuia. Sasa inawezekana huko TAMISEMI kuna mtu ananufaika na kuhamahama kwa watumishi, hebu tuliangalie hili na tulidhibiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, upande huo huo wa elimu tunao uchakavu mkubwa sana kwenye shule za msingi. majengo ya shule za msingi kwa kweli ni chakavu mno. Kwenye shule za msingi hizi yako madarasa mengine ukiingia darasa la kwanza unaona mpaka darasa la tatu kutokana na nyufa zilizopo pale. Hakuna madirisha, wala hakuna milango.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kupitia bajeti hii, kama ilivyokwenda kwenye elimu yA sekondari na tumeweka miundombinu mizuri, basi tuhamie na upande wa elimu msingi ili tuweke miundombinu sawa sawa ili elimu yetu iende sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu tumepata shule tatu mpya za sekondari ambazo ni Maji Maji Sekondari, Kungu Sekondari na Tinginya Sekondari, hizi shule zimekamilika sawasawa. Pamoja na upungufu wa walimu hao, pia tunalo tatizo kubwa kwamba zile shule kwa sasa hazina mabweni. Sometimes wanafunzi wanaosoma pale wengine wanatoka kilometa 20, kilometa 30 na wanakwenda kusoma katika zile shule. Sasa kuna changamoto kubwa sana ya wanafunzi wa kike ambao wengine wanakwenda kupanga mitaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi wa kike wakipanga mitaani kukamilisha ndoto zao za elimu ni ngumu mno. Kwa hiyo, kwa kuwaokoa wanafunzi hawa wa kike ni lazima tuhakikishe zile shule zinapata mabweni na hatimaye wanafunzi wale waweze kulala pale pale shuleni na hatimaye waweze kutimiza ndoto zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie upande wa miundombinu, tunalo Daraja la Muhesi ambalo linaunganisha takribani mikoa mitatu ama minne. Ukitoka Tunduru, Mkoa wa Mtwara, Mkoa wa Lindi na Pwani. Mwanzoni tulikuwa na daraja refu ambalo lilikuwa halijai maji kwa haraka, lakini kwa sasa baada ya kujenga daraja jipya inawezekana wataalamu hawakuzingatia viwango ama hawakuzingatia ukubwa wa Mto Muhesi uliopo pale, kwa sababu daraja lile mvua ikinyesha kidogo tu au Morogoro lile daraja linafunikwa kabisa, hakuna alama yoyote inayoonekana pale, magari yanasimama kwa muda wa siku tatu hadi nne hayapiti pale. Kwa hiyo, sasa tunakwenda kushusha uchumi wa Tunduru na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba, sasa kama ikiwezekana, daraja lile libomolewe na lijengwe upya, linyanyuliwe liwe refu ili maji yasiweze kufunika daraja lile, pia ikiwezekana litanuliwe liwe pana. Ninaamini lile daraja limejengwa likiwa fupi mno kwa sababu siku tatu, siku nne linafunikwa. Tunaomba lizingatiwe, waende kutengeneza daraja jipya na kulinyanyua ili yale maji yasiwe yanajaa na hatimaye kuweza kuisaidia hii mikoa ambayo inaunganishwa na daraja lile ili tuweze kufanya kazi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la afya namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tulipokea shilingi milioni 900 na tumefanya ukarabati wa ile Hospitali kongwe ya Wilaya. Hospitali ile toka imejengwa haikuwahi kupokea fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ukarabati, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea shilingi milioni 900. Majengo tumeyajenga pale, sasa hivi akina mama wa Tunduru wanafurahi. Wakienda wanasema kwa kweli hii Hospitali kwa sasa siyo Hospitali ya Wilaya, ina hadhi ya Hospitali ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo changamoto ambayo tumekuwa nayo pale. Sasa majengo yale yako ya aina mbili tofauti. Mfano wa dawa kama vile Kidonge cha tetracycline, upande kina rangi nyekundu upande mwingine rangi nyeusi. Nini namaanisha hapa? Ninachomaanisha ni kwamba yako majengo ambayo yanavutia sana na yako majengo mengine machakavu ambayo yanafanana, afadhali hata ya hadhi ya kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu hapo ni kwamba twende tukakamilishe yale majengo mengine ambayo yamechoka ambayo yanawauliza madaktari na wagonjwa kwamba nikuue saa ngapi? Nikubomokee saa ngapi? Twende tukayakarabati ili yafanane na yale mengine ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyajenga yaweze kwenda sawasawa na hatimaye mwaka 2025 tuweze kurudisha shukurani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Hospitali hiyo hiyo, bado hatuna majengo mawili. Ni Hospitali ya Wilaya, lakini hatuna jengo la pharmacy na hatuna jengo la utawala. Tunaomba twende tukamilishe pale ili Hospitali ile iweze kuonekana kama inavyotakikana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Zidadu.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.