Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yote, nipende kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo langu la Manonga na wananchi wote kwa ujumla wa Wilaya yetu ya Igunga, Mkoa wa Tabora kwa kunipa fursa hii adimu ya kuwawakilisha na kwa imani kubwa waliyoijenga juu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote leo tupo katika kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais na katika hotuba ile Mheshimiwa Rais alizungumza mambo mengi, mojawapo kubwa …
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali, naomba ubadilishe microphone, hiyo uliyopo inaleta mwangwi, naomba uhamie microphone nyingine.
MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake…
MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ile Mheshimiwa Rais alizungumzia mambo mengi na kwa uzito wa kipekee alizungumzia suala zima la utumbuaji wa majipu. Kwa kweli suala hili la utumbuaji wa majipu linaendana kabisa na suala zima la
rushwa na ufisadi katika nchi yetu. Pia inaendana na kauli ya Mheshimiwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipozungumzia maadui wakubwa katika nchi yetu, ambapo alitaja maadui ujinga, maradhi, umaskini na
rushwa hii sasa inaingia katika maadui wakubwa wanne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili la kutumbua majipu Mheshimiwa Rais alisema sisi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumuunge mkono na tumuunge mkono bila kujali itikadi ya vyama vyetu vya siasa. Tumuunge mkono kwa maana kazi hii si kazi ndogo, ni
kubwa na alizungumza kwa machungu makubwa. Sasa mimi nitashangaa kama kuna watu watakuwa wanazungumza kwa kubeza hotuba ile ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini anavyokuwa anatumbua wakati mwingine utumbuaji wake hauangalii chama cha siasa. Majipu hayo aliyataja yapo ndani ya CCM lakini pia yapo kwenye vyama vya CHADEMA, CUF na wananchi wa kawaida. Maana yake mtu yeyote fisadi
anajifichaficha kwenye vyama wakati mwingine hata nje ya chama ili mradi yeye aangalie namba gani atatuibia. Kwa hiyo, katika utumbuaji huu tushirikiane Wabunge wote kumuunga mkono katika jitihada ambao anazifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii si rahisi na siyo ndogo. Kwa mfano, tumeweza kupata taarifa wengine tuliziona kwenye magazeti na kwingineko kuna baadhi ya watu walioenda kufanya hitilafafu katika ofisi ya TRA na kuiba computer na taarifa zingine. Maana yake nini?
Yote hiyo ni kuficha taarifa ambazo tayari kuna watu ambao wanashiriki kwa namna moja ama nyingine kulihujumu Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati wanatumbuliwa na Mheshimiwa Rais anachukua hatua mbalimbali dhidi ya watumishi hawa maana matatizo haya ni kutokana na watumishi waliopo ndani ya Serikali kwa muda mrefu ambao kila zama zinazokuja wao wamo.
Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere walikuwepo, utawala wa Mzee Mwinyi wapo, utawala wa Mzee Mkapa wapo, utawala wa Mzee Kikwete walikuwepo na utawala wa Mheshimiwa John Pombe wapo. Sasa katika kutumbuliwa naamini kabisa kuna wafuasi ambao
wapo kwenye vyama vingine wanaumia jinsi ambavyo Rais anavyochukua hatua dhidi ya hao watapeli wetu na wahujumu uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais katika hatua mbalimbali anazochukua dhidi ya watumishi ambao siyo waaminifu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wasiseme hapa kwamba Mheshimiwa Rais anakiuka Katiba, sheria na taratibu mbalimbali hapana tumuache Rais achukue hatua dhidi ya watu hawa ambao wanatuhujumu katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hujuma hii athari yake inalikumba Taifa letu na ndiyo maana kila siku tunakuja na kauli mbiu za kuhakikisha kwamba tunawakomboa Watanzania kutokana na hali ngumu ya maisha waliyonayo. Matatizo haya yapo na yataendelea kuwepo na sisi
viongozi tutamaliza miaka mitano tutaenda kuomba kura tena, maana yake matatizo mpaka tutakufa hatutaweza kuyamaliza. Kila siku ni lazima kuangalia tunapunguzaje hizi kero zilizopo.
Ndiyo maana tunaomba kura kila baada ya miaka mitano mtuchague ili tupunguze matatizo.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika sera ya Mheshimiwa Rais ya „Hapa Kazi Tu‟ katika hotuba yake ukurasa wa 13 amesema kwamba Serikali ya Dkt. Magufuli itakuwa ya viwanda.
Viwanda hivi tunavizungumza hapa vilikuwepo toka enzi ya Mwalimu lakini vingine vilikufa toka enzi hiyo ya Mwalimu, vingine vilikufa enzi ya Mzee Mwinyi na vingine vilibinafsishwa enzi ya Mzee Mkapa na vingine vilibinafsishwa enzi ya Kikwete na watendaji wengine ambao wapo
dhama zote na wamefanya kazi miaka yote hii na katika ubadhirifu huu wameshiriki kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, katika uchukuaji hatua, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais aendelee kuyatumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili suala la viwanda, tuwaombe Mawaziri washirikiane na Rais kuhakikisha kwamba vile viwanda vilivyokuwepo awali tuanze navyo hivyo kwanza.
Tujue status yake, tujue tunawezaje kuanza na hivyo kabla hatujaanza kufungua viwanda vingine. Kwa mfano, kwenye Jimbo letu la Manonga tulikuwa na ginnery ya pamba inaitwa Manonga Ginnery ambayo ilikuwa inasaidia na ku-stimulate wananchi wa maeneo yale kulima kwa wingi zao la pamba. Matokeo yake toka kubinafsishwa kwa kiwanda kile hata uzalishaji wa zao la pamba umepungua. Mwisho wa siku zao hili litapotea maana wananchi sasa wanakwenda kulima mazao ya chakula badala ya biashara na mazao ya biashara yanasaidia
kuongeza pato la nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika hotuba ile ya Mheshimiwa Rais alizungumzia matatizo makubwa ya maji ambayo wananchi tunayo. Kila Mbunge humu anazungumzia tatizo la maji, hilo ni kweli ni tatizo sugu katika nchi yetu na tunatambua tuna vyanzo vingi vya maji.
Niiombe Wizara ya Maji kwa sababu Mheshimiwa Rais anakwenda na kasi ya viwango na yenyewe ikimbie haraka, tuchimbe mabwawa kwenye maeneo ambayo ni makame ili yasaidie kutunza maji kwa kipindi chote cha masika na kiangazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Choma Chankola, Tarafa ya Manonga, walikuja watu wa Kanda ya Magharibi kufanya survey wakatuhakikishia watachimba bwawa kubwa ambalo litahifadhi maji na kilimo cha umwagiliaji kitafanyika. Ni miaka mitatu toka wamekuja wale wataalam hatujasikia lolote.
Tunaiomba sasa hii kasi ya Mheshimiwa Rais na hawa waliopo chini kwenye Wizara waendane nayo sawa, wasipishane. Siyo Rais anakimbia wao wanatembea, hatuwezi tukalikubali na kuliunga mkono na tutalisema hili kuhakikisha kwamba na wao wanakimbia
ikiwezekana wakimbie kuliko Rais. Tena Rais ifike hatua awaambie punguzeni kasi maana ameshawazidi kasi kwa mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia aliahidi kusaidia wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu. Kwenye Jimbo la Manong, kwenye Kata ya Mwashiku, Ntogo na Ngulu kuna wachimbaji wadogo wadogo. Tunaiomba Wizara pia iangalie namna gani itaweza
kuwasaidia hawa wachimbaji kuhakikisha kwamba wanajikwamua kutokana na hali ngumu ya maisha waliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote, kuna mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria ambao unatoka Mwanza kupitia Nzega unaenda Tabora lakini ukifika Nzega unakwenda Igunga, ukiwa unakwenda Igunga unapita pale katikati panaitwa Ziba ambako ni
junction ya kwenda makao makuu ya Tarafa ya Manonga na Tarafa ya Simbo. Tuliahidiwa kwamba yale maji yataweza kufika katika maeneo yale. Tunaiomba Wizara maana tuliona tayari fungu lilishatengwa kwa ajili ya kazi ya kupeleka maji lakini leo kwenye taarifa zetu inaonekana kwamba usanifu utaanza mwaka 2016/2017. Niiombe Wizara ipitie upya taarifa zao ili kuhakikisha kwamba…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali muda wako umeisha, naomba ukae tafadhali.
MHE. SEIF KHAMIS GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafsi hii. (Makofi)