Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitaanza kwa kuzungumzia zahanati na vituo vya afya hasa kwa kuzingatia umuhimu wake katika jamii yetu. Ninachojua ni kwamba, lengo la zahanati kujengwa katika kila kijiji na vituo vya afya kujengwa katika kila kata ni kusogeza zaidi huduma kwa wananchi. Itakuwa haina maana kama tutaendelea kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga zahanati kila Kijiji, tukaendelea kujaza majengo na wananchi wakashindwa kupata huduma inayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kiukweli maeneo mengi hali ni mbaya. Zahanati zimejengwa na zimepakwa rangi, zinavutia, vituo vya afya vimejengwa vimepakwa rangi na vinavutia, lakini huduma katika maeneo mengi hazipatikani. Itakuwa haina maana kama tutakuwa tuna vituo vya afya na zahanati kila kijiji halafu wananchi wakaendelea kupoteza maisha kwa kukosa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia mfano mmoja, katika Zahanati ya Kijiji cha Namwangwa iliyoko katika Kata ya Hezya Wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe ni miezi mitatu mfululizo sasa wananchi wamekosa huduma ya afya kwa sababu tu ya kukosekana mhudumu wa afya kwenye ile zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa Kumi na Moja, mwaka 2023 mtumishi aliyekuwa katika ile zahanati alistaafu ikasababisha wananchi kuendelea kukosa huduma. Baada ya mwezi mmoja akaletwa mtumishi mwingine, naye akahamishwa tena baada ya mwezi mmoja. Sasa ni miezi mitatu mfululizo wananchi wa kijiji hicho hawapati huduma ilhali zahanati hiyo inahudumia zaidi ya wananchi 50 kwa siku, huku kijiji kikiwa na watu zaidi ya 1,000. Hebu fikiria, wananchi wanakosa huduma kila leo, kwa sababu tu ya zahanati kukosa mhudumu wa afya jambo ambalo siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya jana, mwanamke mmoja anaitwa Mickness Chisunga alipoteza mtoto wakati akiwa katika harakati za kutafuta huduma na ameshindwa kupata huduma kwa sababu zahanati imefungwa. Hii haikai sawa. Kuna maana gani ya kujenga zahanati kila Kijiji ikiwa wananchi wanashindwa kupata huduma? Haina maana. Hii haikai sawa, na ukizingatia hali halisi ya mvua zinazonyesha kwenye mkoa wetu. Hatimaye mume wake alivyojitahidi kwenda kutafuta huduma huku na kule akashindwa kuvuka mto kwa sababu mvua zilikuwa zimenyesha na barabara hakuna, hawezi kupita, akarudi nyumbani na mwanamke akajifungua mtoto akiwa amekufa. Hii ni hatari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja ya kuhakikisha hivi vituo vya afya tunavyovijenga kila kata na hizi zahanati tunazozijenga kila kijiji tuhakikishe kuna vifaatiba na wahudumu wa kutosha ili wananchi waweze kupata huduma iliyokusudiwa. Hatujui ni maeneo mangapi tunapoteza watu wengi sana kwa sababu tu ya kukosa huduma. Haina maana ya kujenga vitu hivi kama tutakuwa tunajaza tu majengo na huduma hamna, itakuwa haina maana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua Serikali ina lengo na nia nzuri lakini tuhakikishe kwamba kila zahanati, kituo cha afya na hospitali tunazojenga kwenye kila wilaya zinakuwa na wahudumu wa kutosha ili wananchi waweze kunufaika nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la maboma. Wamezungumza wengi sana, lakini Songwe tuna changamoto kubwa sana ambayo naomba Mheshimiwa Waziri atavyokuja kuhitimisha hoja atuambie ni lini mamboma 1,386 yaliyojengwa katika Wilaya ya Mbozi yatakamilishwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba maboma haya yamengwa kwa nguvu za wananchi. Wananchi wamejenga kwa moyo wa kupenda na kwa hiyari yao wameweza kujenga maboma 1,386. Hapa sizungumzii maboma 10, 60 au 100 kama walivyozungumza wengine, hapa nazungumzia maboma 1,386 ndani ya wilaya moja. Hii ni hali ya hatari sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba Songwe kuna mvua zinanyesha kila leo, maboma mengine yataanguka kwa sababu mvua ni nyingi sana kwenye mikoa yetu. Tunawakatisha tamaa wananchi ambao wanajitoa kwa mioyo ya kupenda kuendeleza maeneo na maendeleo katika jamii yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, atuambie mkakati wa Serikali katika kukamilisha maboma haya yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi ni upi? Sisi kama Songwe tunatamani tusikie kauli ya Serikali wanasemaje kuhusiana na hili? Kwa sababu halmashauri zetu hata zingejitahidi kwa namna gani kutenga fedha za ndani, hebu fikiria wilaya moja maboma 1,386 mnafanyaje? Labda tusimamishe kila jambo tuweze kuyapaua haya. Serikali ije na kauli, imejipangaje kuhakikisha haiwakatishi wananchi tamaa (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mengi ambayo tunaendelea nayo, hatimaye tunashindwa kuwaendea wananchi kwa sababu wanaona hata kile walichokifanya ni kama Serikali haikithamini. Tunaomba atakapokuwa anakuja kutuambia hapa atuambie mkamkati wa Serikali wa kukamilisha maboma hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ninalotaka kulizungumzia ni suala la asilimia 10 ya fedha za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Wengi wamezungumzia hapa, tunajua Serikali ina nia njema ya kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanapata mitaji ili waweze kujiendesha katika masuala mbalimbali, lakini hapa kuna kundi limesahaulika. Hili ni kundi la wanaume kuanzia miaka 45 na kuendelea. Ukienda huko sokoni hawa ndio wanaotegemewa na familia zao, lakini kundi hili limeshaulika, hatimaye wanaona kama Serikali imewatenga na haiwajali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukienda hapo Majengo, utaona asilimia kubwa sasa hivi wazee wa kuanzia miaka 45, 50 mpaka 70 ndio wako sokoni, ni wajasiriamali, lakini watu hawa hawakopesheki kwa sababu wako kwenye kundi la wazee. Ukija kwenye upande wa wanawake, tunaingia katika makundi mbalimbali. Kijana ataingia kwenye kundi la mwanamke... (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke mwenye umri wa miaka 70 mpaka 80 ataingia kwenye kundi la mwanamke, lakini vipi kuhusiana na hili kundi?
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mzuri anaoendelea nao Mheshimiwa Stella, naomba nimpe taarifa kwamba miaka 45 siyo wazee.
NAIBU SPIKA: Taarifa hiyo.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, hawa hawakopesheki, hawana sifa za kukopesheka huko kwenye maeneo yetu. Basi tuyaache hayo ya miaka 40. Tuzungumzie 50 mpaka 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili kundi limewekwa kwenye eneo gani? Hawa ni walipakodi wazuri kwenye nchi yetu, nao wanastahili kupokea mikopo kama wanavyopokea makundi mengine. Tusilitenge kundi hili. Mwisho wa siku ndiyo tegemezi kwenye familia zao. Wanapata wapi mitaji ya kuendesha biashara zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ituambie, hili kundi imeliweka kwenye maeneo gani? Kwa sababu mwisho wa siku ukienda hata huko mitaani wananchi wa namna hii wanaona kama Serikali imewatenga na haiwajali. Waziri akija hapa atuambie, hili kundi linanufaikaje na kodi za nchi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, naomba kuzungumzia suala la changamoto ya maji kwenye shule za sekondari na msingi. Kumekuwa kuna changamoto kubwa mno, na hasa ukizingatia mpango uliopo sasa hivi wa kupata chakula shuleni. Shule nyingi wanafunzi wanaacha masomo, wanahangaika kwenda kutafuta maji kwa ajili ya kupikia chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja, atuambie ana mpango wa kuhakikisha wanajenga mifumo ya uvunaji maji ya mvua ili kila shule ziweze kuvuna maji ili waondokane na changamoto ya maji, hasa kwenye mikoa yetu. Ukienda kwetu mvua zinanyesha, lakini maji yanapotea tu. Mpango wa Serikali ni upi kuhakikisha wanavuna maji ya mvua ili tuepukane na hiyo changamoto kwenye shule zetu za msingi na sekondari? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kabisa niseme, wengi wamezungumza sana kwa habari ya kikokotoo. Wananchi wa Mkoa wa Songwe wamenituma niseme, issue ya kikokotoo imekuwa ni mateso na janga kwa watumishi walioitumikia Serikali hii kwa uaminifu. Hizi fedha siyo hisani ya Serikali kwamba mnawapa watumishi kwa huruma, siyo kwamba mnawapa wastaafu kwa huruma, ni haki yao. Ni fedha zao ambazo wamekatwa na wanastahili kupewa kwa uaminifu kama wanavyotaka wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunashangaa hii asilimia 33, watu hadi wanakufa kabla ya umri wao! Hebu fikiria, mtu anastaafu anapata shilingi milioni 17, anaenda kufanyia nini huko mtaani kama siyo kuongeza magonjwa mwilini? Serikali ituambie, mpango wao ni upi? wananchi na wastaafu wanataka walipwe fedha zao kama wanavyohitaji wao na tusiwapangie, kwa sababu mwisho wa siku watu wanakufa kabla ya umri wao, watu wanazeeka kabla ya muda wa kuzeeka. Sasa hivi mtu akikaribia kustaafu, anaanza kuugua, maana anajua adha anayoenda kukumbana nayo huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ituambie, mpango ni upi? Wananchi wanataka fedha zao. Wengi wanasema, mtupe chetu tufe mapema. Wengine wanasema mtupe chetu kila mtu atembee, kwa sababu kama Serikali tumeitumikia kwa uaminifu, kwa nini muanze kutupangia kwenye suala la kutulipa? Hizo fedha ni za kwao wala siyo hisani ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema haya, nashukuru sana. Ahsante. (Makofi)