Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya elimu na afya kwa asilimia kubwa kuliko kipindi chochote cha awamu zilizopita. Taifa lolote ili likuwe kiuchumi ni lazima kuzalisha rasilimali watu kwa kada tofauti tofauti na kuacha kuwa tegemezi ya wataalamu toka nchi za nje. Kwa sasa zile kero za michango zimepungua sana na huduma zimeongezeka na kusogezwa kwa wananchi licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri ari iongezwe kwenye shule za misingi kongwe pamoja kuhakikisha kila kata ina kituo cha afya na kila kijiji kina zahanati. Pongezi pia kwa Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake wote pamoja na watendaji wa Wizara ambao wanafanya kazi kubwa ya kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba niwapongeze aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara - Mheshimiwa Said Mtanda na Mkuu wa Wilaya ya Tarime - Kanali Michael Mtenjele ambao kwa sasa wamehamishwa vituo vya kazi, nawatakia kila la kheri huko waendako na utendaji mwema katika kulijenga Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie fursa hii kuwakaribisha Mkuu wa Mkoa mpya wa Mara Kanali Evans Mtambi pamoja na Mkuu wa Wilaya mpya wa Tarime - Kanali Maulid Surumbu, karibuni sana na tunawahakikishia ushirikiano uliotupa kwa maendeleo ya Mara yetu na Tarime yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kumpongeza Mkurugenzi wa Mji wa Tarime Mheshimiwa Gimbana Ntavyo kwa namna alivyosimamia utendaji wenye ufanisi na weledi kwenye halmashauri yetu hata kupelekea kuongezeka kwa mapato, usimamizi bora wa miradi ya kimkakati kama soko kuu la Tarime, miradi mbalimbali inayoletwa na Serikali Kuu pamoja na kuongeza mapato ya ndani. Haya yote yamewezekana kwa kuimarisha ushirikiano chanya na watendaji walio chini yake na kwa kweli utendaji na ufanisi kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo tunaouona hata Kamati ya LAAC pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu walivutiwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali hasa Soko Kuu na Jengo la Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kuchangia maeneo matatu kwenye Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili nchi iendelee lazima kama Taifa tuwekeze kwenye elimu na afya kuanzia ngazi za mitaa na vitongoji, lakini pia kuhakikisha kuwa makundi maalum yanazingatiwa kwenye miundombinu ya shule, zahanati, vituo vya afya, hospitali za miji, wilaya na mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya elimu, Halmashauri ya Mji wa Tarime inazo changamoto mbalimbali kama ambavyo naenda kuainisha:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, shule za sekondari. Uhitaji wa kupandisha hadhi Shule ya Sekondari ya Mogabiri ili iwe ya kidato cha tano na cha sita. Umuhimu wa hii shule kuwa ya kidato cha tano na sita ni ili kutoa fursa kwa mabinti zetu wanaomaliza kidato cha nne waweze kujiunga hapa na kupunguza idada ya Watanzania wanaokosa fursa ya kujiendeleza, maana kwa sasa tuna shule moja tu ya kidato cha tano na sita ambayo ni Tarime High School, hii ni shule ya wavulana tu na inafanya vyema sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Shule ya Sekondari Mogabiri ina miundombinu tayari wezeshezi kama vile zahanati, mabweni mawili ambayo yapo kwenye hatua ya umaliziaji, madarasa mawili, visima viwili vya maji. Vilevile taratibu zote zipo tayari na tulishawasilisha maombi. Hivyo tunaomba sana Serikali ipandishe shule hii hadhi na maombi haya yamedumu kwa takribani miaka saba. Hivyo tunaomba Serikali izingatie hoja hii kwa uzito wako.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni suala zima la wanafunzi kukatisha masomo (drop out) kwa sababu mbalimbali kulingana na ziara niliyofanya kwenye sekondari zote zilizopo ndani ya Halmashauri ya Mji, niligundua kuwa watoto wetu wengi wanakatisha masomo kwa upande wa wanafunzi wa kiume ni kutokana na umbali mrefu sanjari na kuona bora wajiuge na vikundi vya ku-bet, kufanya biashara migodini na vibarua ama kuvuta bangi na kwa wanafunzi wa kike wengi wao hukatisha masomo sababu ya umbali mrefu, kulagaiwa na kupata ujauzito na/au kuolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya suluhisho la kupunguza au kuondoa kabisa drop out kwenye shule zetu ni kwa kujenga hostel kwenye shule zote za kata ambazo mwanafunzi anawajibika kutembea muda mrefu. Katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kuanzia, tunaomba Shule ya Sekondari Nyagisese ambayo ni shule mpya kabisa, ina miundombinu yote kama vile madarasa ya kutosha na ya kisasa, maabara za masomo yote lakini haina wanafunzi wa kutosha sababu ya umbali. Hivyo tunaomba Serikali itutengee fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwalo na mabweni mawili ambapo tukipata kwa mwaka huu wa fedha itasaidia sana, maana shule hii ipo nje ya mji na ni mbali na makazi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ombi tuliwakilisha wakati wa ziara ya Waziri Mkuu aliyoifanya mwezi Februari mkoani Mara. Hivyo tunaomba kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na bwalo kinyume na hapo itakuwa ni uharibifu wa rasilimali maana kiuhalisia hakuna mtoto atakayesoma pale. Mahudhurio yatakuwa hafifu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni shule za msingi; Shule ya msingi Magufuli Maalum ni shule ambayo ipo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum kama vile watoto wenye ulemavu wa akili, ulemavu wa kuona na ulemavu wa kusikia. Shule hii ina jumla ya wanafunzi 120 ambapo wavulana ni 63 na wasichana ni 57 kati ya hao wanafunzi wenye ulemavu wa akili ni 51 (wavulana ni 51 na wasichana 40), ulemavu wa kusikia ni 22 (wavulana nane na wasichana 14) na ulemavu wa kuona ni saba (wavulana ni wanne na wasichana watatu). Pamoja na kwamba shule hii ambayo imekuwa mkombozi kwa watoto wenye mahitaji maalum ambao wamekuwa wakibaki nyumbani na kukosa haki yao ya kupata elimu, inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-

(i) Kukosekana kwa gari ambalo lingetumika kuwafuata watoto hasa wanaoishi maeneo ya mbali na shule, kwa sasa wanatumia bajaji ambayo haikidhi mahitaji na hivyo kupelekea watoto wengi kukosa fursa maana hawawezi kuja shuleni na kwa mazingira ya mji wa Tarime hauna huduma za daladala na hata kama zingekuwepo isingeweza kuwabeba watoto hawa wenye mahitaji maalum.

(ii) Uzio kwa ajili ya kuimalisha usalama wa watoto wawapo maana ilivyo sasa na upungufu wa wafanyakazi inakuwa siyo salama kwa watoto hawa kwani wanaweza ondoka shuleni na kusababisha matatizo makubwa kwa jamii na kwa watoto wenyewe.
(iii) Chumba cha matibabu kwa ajili ya huduma ya kwanza ikiwa ni pamoja na kupatiwa wataalamu wa mazoezi na matamshi. Kwa sasa watoto hawa wanasoma kwenye mazingira magumu sana ambapo walimu unakuta tena ndio wanatumika kutoa huduma hii ambayo siyo sawa.

(iv) Bweni la wavulana ikiwa ni pamoja na kumalizia bweni la wasichana ambalo limekamilika imebakia hatua za umaliziaji na kuweka vitanda. Ujenzi wa bweni hili ni muhimu sana maana utasaidia kuongeza uangalizi kwa watoto hawa na kupelekea ufanisi katika mafunzo yao na usalama wao.

(v) Mahitaji ya bwalo, jengo la utawala pamoja na walau nyumba tatu za walimu ikiwa ni moja kwa kila kundi la mahitaji maalum kwa maana ya walemavu wa akili, kuona na kusikia.

(vi) Mashine ya kubadilisha maandishi ya kawaida kwenda kwenye nukta nundu kwa maana ya embosser machine.

(vii) Mahitaji ya haraka ya walimu kwa maana kwa sasa tuna walimu 12 tu kati ya walimu 25 wanaohitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upungufu wa walimu katika kada zote za mahitaji maalamu kama ifuatavyo; walimu wanne kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili, walimu watatu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kuona na walimu sita kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii shule ni dhahili Serikali lazima iipe kipaumbele hata ikiwezekana watupe fedha za BOOST ili kuweza kukamilisha changamoto za miundombinu kama ambavyo nimeainisha hapo juu, vilevile Serikali ione umuhimu wa kuleta wataalamu waliombwa na walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shule za Msingi za Ronsoti pamoja na Bomani ni muhimu sana zikajengwa maana kwa sasa watoto wanaotoka maeneo haya wanagongwa na magari wanapovuka barabara kwenda kusoma upande wa pili kwenye shule ambazo zipo mitaa mingine, kwa mfano wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Tarime wanatoka Mtaa wa Ronsoti ambapo tumepoteza wanafunzi wengi wakiwa wanavuka barabara kuu ya Mwanza kwenda Kenya na pia wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Buhemba wakitokea Bomani wakiwa wanavuka barabara kuu inayoinga Tarime Mjini wanagongwa na kupoteza maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati sasa Serikali kwenye mwaka wa fedha 2024/2025 tuweze kupata fedha za BOOST ili tuweza kujenga hizi shule mbili, kwa maana halmashauri imetenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa shule za Sekondari za Ikolo na Sabasaba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuna shule kongwe za msingi ambazo kwa kweli ni hatarishi kwa maisha ya watoto wetu pamoja na walimu, kwani majendo mengi yamebomoka, ni mafupi na hayana hadhi ya kuwa shule za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nyakati tofauti nimesimama na kuongelea kuhusu shule hizi hususan Shule ya Msingi Kiongera, Kikomori na Nyabirongo zilizopo Kata ya Susuni ambazo ni kongwe na chakavu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilienda mbali na kuleta vielelezo mbalimbali kama picha na video kuonesha uchakavu wa Shule ya Msingi Nyabirongo ambayo ni hatarishi sana na hawajawahi kupata fedha zozote zile toka Serikalini, tunaomba sana kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 Serikali iweze kutupatia fedha za BOOST ili kunusuru maisha ya hawa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyabirongo. Vielelezo na maombi nilipeleka kwa Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri Mheshimiwa Ndejembi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la mchango wangu ni kuhusu malalamiko ya muda mrefu ya mapunjo kwa walimu kwenye kupandishwa madaraja na kulipa mishahara/maslahi stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ziara yangu ya kikazi niligundua kuna walimu wengi hawajalipwa, mfano Mwalimu Samwel Mwita Mogaiga wa Shule ya Msingi Buhemba iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime ambaye tarehe 01 Aprili, 2013 alipewa cheo cha TGTS D mshahara ukabadilika mwezi wa nane, hakuwahi kulipwa licha ya kudai bila mafanikio. Baada ya hapo, tarehe 01 Mei, 2019 akapewa cheo cha TGTS E akabadilishiwa mshahara tena mwezi wa nane, lakini hajawahi kulipwa na hajui atalipwa lini hizi stahiki zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa afya Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime imekuwa na changamoto kubwa ya kuweza kumudu uhitaji mkubwa wa kuhudumia wananchi wanaotoka nje ya Mji wa Tarime ambao kwa kweli ni mzigo na unapoka haki ya wananchi wa Tarime Mji kupata huduma stahiki. Tunapokea wagonjwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Wilaya ya Rorya, baadhi kutoka Wilaya ya Serengeti na wengine kutoka nchi jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko hospitali hii ambayo ilitakiwa kupandishwa hadhi na kuwa ya wilaya na siyo mji ili kuweza kupata mgao halisia kuliko ilivyo sasa. Mfano Kituo cha Afya cha Magena kilichopo Kata ya Nkende, Halmashauri ya Mji kwa mwezi Oktoba na Novemba, 2023 wanawake waliojifungulia pale walikuwa 59 kati ya hao 33 sawa na 56% walitoka Tarime DC huku 26 sawa na 44% tu ndio waliotoka Tarime TC hii ni kutokana na jiografia ya majimbo haya mawili kwa maana Kata ya Susuni na Mwema za Tarime DC hazina vituo vya afya na hivyo kituo au hospitali iliyo karibu ni Kituo cha Afya cha Magena na Hospitali ya Tarime Mji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana niliwahi kuiomba Serikali kutujengea kituo cha afya kwa kupandisha hadhi Zahanati ya Kiongera kuwa kituo cha afya kwa Kata ya Susuni sanjari na kujenga Kituo cha Afya kwenye Kata ya Mwema. Hii itapunguza mzigo kwa Kituo cha Afya Magena, lakini kwa upande wa Hospitali ya Miji wanawake waliojifungua ni 1059 kati ya hao 386 sawa na 36% walitoka nje ya Tarime TC kati ya Oktoba na Desemba, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu tuongezewe gari moja la wagonjwa kutokana na kupokea wagonjwa wengi kutoka Halmashauri ya Wilaya ambao hulazimika kuwapeleka Mwanza kwa Rufaa kwenda Hospitali ya Bugando. Pia Serikali iweze kutuongezea fedha za dawa kutokana na asilimia kubwa kulipwa kutokana na idadi kubwa ya watu waliopo 70 MSD na 60 Busket Fund.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mchango wangu huu ambao nina imani utafanyiwa kazi naomba kuwasilisha