Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Katani Ahmadi Katani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tandahimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi, kwa uhai na siha njema inayonipelekea kufanya shughuli zangu za uwakilishi kwa ufanisi mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia suluhu Hassan kwa uchapaji Kazi wake mzuri na uliotukuka kwa taifa lake na watu wake, mh.spika tangu tupate uhuru wa taifa hili nakuwa na Marais kadhaa waliomtangulia lakini hajapata kutokea Rais amefanya mambo mengi makubwa kwa muda mfupi tena yanayogusa maisha ya kila siku ya mtanzania, mh.spika namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa haya yafuatayo:-

(i) Kukamilisha mradi mkubwa wa bwawa la Mwalimu Nyerere;
(ii) Kuendeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa SGR;
(iii) kuendeleza mradi wa daraja la Busisi kule Mwanza;
(iv) Ujenzi wa hospital za rufaa za Kanda;
(v) Ujenzi wa vituo vya afya nchi mzima;
(vi) Ujenzi wa madarasa na shule mpya; na
(vii) Ujenzi wa barabara za ndani ya mikoa na wilaya kupitia TARURA na TANROADS.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Wizara hii ya TAMISEMI kwa kumkabidhi Waziri, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, kwani kijana huyu ingekuwa mchezaji wa timu ya mpira wa miguu, basi ni kiungo mkabaji na mchezeshaji mfano wa Haridi Aucho wa Dar Young African maana pasipo kiungo huyu basi ushindi wa Yanga unakuwa mgumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika TAMISEMI isipofanya vizuri, basi hata Wizara nyingine haziwezi kuonekana. Hakika Mheshimiwa Rais hajakosea kwa uteuzi huu bora kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Manaibu Mawaziri wote wawili wa TAMISEMI kwa namna wanavyoweza kumsaidia kwa umakini mkubwa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI. Pamoja na mazuri yote, bado jimbo langu la Tandahimba lina changamoto zifuatazo:-

Kwa upande wa Tarura kuna changamoto ya barabara yenye umbali wa Kilometa 1.5 kutoka Luagala - Liponde barabara ambapo Mtendaji Mkuu wa TARURA, Engineer Seff anaifahamu ubovu wake na sasa imefika miaka saba barabara hii haijajengwa kwa kiwango cha lami. Kama barabara hii haitapangiwa bajeti, basi nakusudia kushika shilingi.

Mheshimiwa Naibu Spika ipo barabara kutoka Mahuta -Lipalwe Kilometa 10.5. Barabara hii TARURA wameitembelea na kuahidi kuijenga kwa kiwango cha lami, pamoja na kufanya feasibility study na kutangaza tenda, lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea. Naomba kufahamu status ya utekelezaji wa mradi wa barabara hii.

Kwa upande wa Sekta ya Afya, naishukuru sana Serikali kwa kutupatia fedha zilizotuwezesha kujenga vituo vya afya vinne. Pamoja na kupata fedha hizo, bado jimbo hili lina kata thelathini na mbili na tarafa saba, hivyo upo uhitaji mkubwa wa vituo vya afya. Namwomba Mheshimiwa Waziri nipate fedha ya kujenga vituo vya afya angalau kila Makao Makuu ya Tarafa. Pamoja na uwepo wa vituo vya afya hivyo, ipo changamoto ya watumishi wa kada hii ya afya. Kwa hiyo, naiomba Serikali kutuongezea watumishi katika kada hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya elimu, naishukuru sana Serikali kwa kutupatia fedha zilizotuwezesha kujenga madarasa zaid ya 128 na shule ya sekondari moja mpya. Hata hivyo, bado kuna kata ya Mkwedu haina shule ya sekondari. Naiomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hii.

Baada ya maelezo haya, naungo mkono hoja.