Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja iliyopo Mezani. Kwanza kabisa, napenda kuanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya na siha njema na pia kutujaalia wote afya na siha njema mpaka wakati huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa upekee kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini katika dhamana hii ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Naendelea kumuahidi kwamba nitafanya kazi kwa bidii, kwa weledi na uadilifu. Pia, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa kwa ulezi wake na uongozi wake makini na kunipokea katika Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Festo Dugange, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, anayeshughulikia masuala ya afya kwa ushirikiano wake mkubwa sana tangu nimeingia kwenye Wizara hii. Pia, natambua ushirikiano mkubwa sana wa Katibu Mkuu, Manaibu Makatibu Wakuu na watumishi wote wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nawashukuru sana kwa mapokezi yenu. Nawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa mnaonipa ambao kimsingi nashindwa kuusimulia kwa maneno, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Spika na wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa malezi yenu na uongozi wenu kwetu sisi Wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Natambua mchango mkubwa sana wa Kamati ya TAMISEMI ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Dennis Londo. Natambua mchango na ushirikiano mkubwa sana wa Waheshimiwa Wabunge wote ambao mnatoa ushirikiano mkubwa sana kwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nachukua pia fursa hii kuwashukuru wanawake wote wa Mkoa wa Kigoma, wapiga kura wangu na wadau mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma kwa ushirikiano wao na dua zao ambazo kimsingi zinanipa utulivu katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja nyingi zinazogusa sekta ya elimu ya msingi na sekondari. Pia, wamezungumzia masuala ya barabara za wilaya, yaani TARURA. Ninachopenda kusema, kwanza tumepokea ushauri na maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge na tunaahidi kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu ukarabati wa shule kongwe na shule chakavu; na Wabunge wengi wametaka kufahamu kwamba kuna mikakati gani ya kuhakikisha kwamba shule hizi zinakarabatiwa kwa sababu zimechakaa sana? Nataka kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kurekebisha shule hizi. Katika kipindi cha mwaka 2022/2023 mpaka mwaka 2023/2024 tayari Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 70.39 kwa ajili ya ukarabati wa shule 793 za msingi na sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ni kwamba Serikali haijaishia hapo. Kwa hiyo, katika mwaka wa fedha unaokuja Serikali itaendelea kufanya ukarabati katika shule kongwe kurekebisha miundombinu chakavu katika shule 50 za msingi. Kwa hiyo, Serikali inafahamu umuhimu wa kufanya marekebisho na ukarabati wa miundombinu katika shule hizi na itaendelea kufanya hii kazi katika mwaka wa fedha unaofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu masuala ya ujenzi wa nyumba za watumishi hususan kwenye kada ya elimu. Tayari katika mwaka wa fedha huu unaoenda kwisha, kupitia miradi ya SEQUIP na BOOST, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imeendelea kujenga nyumba 253 kwa thamani ya jumla ya shilingi bilioni 25.26. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ni kwamba, Serikali haitaishia hapo. Kwa kupitia hii miradi ya SEQUIP na BOOST, katika mwaka wa Fedha 2024/2025 Serikali imepanga kujenga jumla ya nyumba 562 za Walimu wa Sekondari na Msingi ambazo zitachukua familia 1,124. Kwa hiyo, naomba kuwahakikishia kwamba, Mheshimiwa Rais anatambua umuhimu wa kujenga nyumba za watumishi wetu na hususan kwenye kada ya elimu. Ndiyo maana zinapatikana hizi fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa nyumba hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na ujenzi wa mabweni. Waheshimiwa Wabunge wameeleza ni kwa namna gani kuna uhitaji mkubwa wa kuwa na mabweni katika shule zetu za sekondari na hasa zile za kutwa. Naomba kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba, katika mwaka huu wa fedha unaoisha 2023/2024, tayari Serikali imejenga jumla ya mabweni 519 nchi nzima yenye jumla ya gharama ya shilingi bilioni 67.41.
Mheshimiwa naibu Spika, katika mwaka wa fedha ujao, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha mabweni 310. Katika mabweni hayo 310, mabweni 274 ni ya shule za sekondari na mabweni 36 ni ya shule za msingi. Aidha, Serikali itaendelea kuwashirikisha wananchi kupitia halmashauri kujenga hosteli kwenye shule za kutwa za kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne kwa kadiri ya mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wametaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miundombinu ya shule mpya inayojengwa na kukamilika ili ianze kutumika na kuepusha uchakavu, kwa sababu, shule nyingi pamoja na miundombinu mingi inajengwa katika hizi shule, lakini kwenye baadhi ya maeneo unakuta kuna madarasa hayatumiki na mwisho wake yale majengo yanaanza tena kuharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili, naomba kurejea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, ambaye amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha kuwa wanatumia utaratibu walioelekezwa wa kuhakikisha kwamba, miundombinu ya shule mpya za sekondari na msingi zilizojengwa inatumiwa na wanafunzi kuanzia Januari, 2025. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tayari Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ametoa maelekezo ambayo ni jukumu la halmashauri kuyazingatia ili haya majengo yote ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Mama Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi kuhakikisha yanajengwa, wanafunzi wetu wayatumie ili yawe na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Waheshimiwa Wabunge wamezungumza na wamechangia sana kuhusiana na suala la upandishaji wa hadhi wa shule zao kuwa kidato cha tano na sita. Kuhusiana na suala hili, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tayari imetoa maelekezo kwamba, halmashauri zifanye tathmini katika miundombinu yote kuangalia kama ni toshelevu na inakidhi mahitaji. Pale itakapothibitika kwamba miundombinu iliyojengwa inakidhi viwango na mahitaji, basi wawasilishe maombi kwenda Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kuomba kupandishwa kwa hadhi ya shule zao kuwa za kidato cha tano na sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kuendelea tu kusisitiza kwamba, utaratibu upo, unafahamika, Wakurugenzi kwenye Halmashauri waweze kufanya utaratibu huo, wakamilishe, wapeleke maombi kwenye Wizara ya Elimu kwa ajili ya kukamilisha hatua za kupandisha hadhi shule kuwa kidato cha tano na sita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kuhusiana na kulipwa kwa madeni na stahiki za walimu. Waheshimiwa Wabunge, wamechangia pia kwenye eneo hili. Naomba kutumia nafasi hii kurejea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye ameelekeza kwamba, madai yote ya likizo na uhamisho yanalipwa haraka. Serikali haitamvumilia Mkurugenzi yeyote ambaye hatatekeleza maelekezo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kurejea kwamba, Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ilishatoa maelekezo kwamba madai yote ya likizo na uhamisho yalipwe haraka. Serikali haitamvumilia Mkurugenzi yeyote ambaye hatatekeleza maelekezo hayo. Kwa hiyo, pamoja na kuwa Serikali imekuwa ikilipa madeni na stahiki za walimu ambapo hadi Desemba, 2023 jumla ya shilingi bilioni 202.43 zimelipwa ambazo ni madeni ya malimbikizo ya mishahara, bado maelekezo ya Mheshimiwa Waziri yasimamiwe ili Wakurugenzi wote wahakikishe kwamba wanalipa malimbikizo ya madai yote ya likizo na uhamisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, michango mingine ya Waheshimiwa Wabunge imeelekezwa kwenye masuala ya barabara zetu za wilaya ambazo zinasimamiwa na TARURA. Waheshimiwa wametaka TARURA iongezewe vitendeakazi kwenye baadhi ya wilaya na hasa magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 tayari TARURA imenunua na kusambaza magari 18 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za barabara. Katika mwaka wa fedha unaokuja, TARURA imepanga kutumia jumla ya shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa magari. Kwa hiyo, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge ambao wametoa hoja hii, wafahamu kwamba tayari kuna fedha zimetengwa na bila shaka vifaa vya kazi, hasa magari vitanunuliwa katika mwaka wa fedha unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza kuhusu upungufu wa watumishi TARURA. Serikali inatambua upungufu huu wa watumishi TARURA, na mpaka muda huu tayari Serikali imeajiri watumishi 27 wa kada ya uhandisi katika mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2023/2024.
Mheshimwia Naibu Spika, katika mwaka wa fedha unaokuja, Serikali imeomba kibali cha kuajiri wahandisi 97, lakini kwa hatua za muda mfupi, Wakala wa Barabara (TARURA) wametumia njia ya kutumia wahandisi 98 ambao wanaendelea kupata mafunzo kwa vitendo. Kwa hiyo, TARURA inatumia wahandisi ambao wanaoendelea kupata mafunzo kwa vitendo, lakini pia ajira za mkataba kwa wahandisi 84 zimetolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inatambua changamoto iliyopo na imechukua hatua hii ambayo ni ya dharura ikiwa ni katika kusubiri mpango wa muda mrefu na wa kudumu ambao ni wa kuajiri wahandisi wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la TARURA, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamependekeza na kutoa ushauri kwa Serikali kwamba, Sekretarieti za Mikoa zisaidie Halmashauri katika utekelezaji wa miradi ya TACTIC kwa kutoa wataalamu wake. Serikali inatambua uhitaji uliopo katika eneo hili na kwa kuzingatia taratibu, itachukua hatua za haraka. Vilevile Serikali imepokea ushauri uliotolewa na itazishirikisha kikamilifu sekretarieti za mikoa katika kuhakikisha zinasaidia utekelezaji wa miradi ya hii ya TACTIC katika halmashauri zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo lilizungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo la halmashauri kubaki na jukumu lake la msingi la kutoa elimu kwa usawa na kuachana na utoaji wa elimu kupitia shule za English Medium. Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetoa ushauri, napenda kusema kuwa ushauri umepokelewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Serikali itazingatia mapendekezo mahususi ambayo yametolewa na kamati kuhusiana na uendeshwaji wa shule hizi za English Medium.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imepokea mapendekezo yote ambayo yametolewa na Kamati ya USEMI kuhusiana na namna ya kuzisimamia hizi shule na hasa kwa sababu Waheshimiwa Wabunge mmetoa maoni na kuona kwamba kunakuwa hakuna usawa kati ya shule za kawaida na hizi za English Medium na kwamba Serikali ibaki na jukumu lake la msingi la kutoa elimu ambayo itakuwa ina usawa na iachane na utoaji wa elimu kupitia English Medium. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema kwamba, tumepokea maoni na ushauri wote na tunaahidi kuwa tutaufanyia kazi. Tunatambua kwamba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni Wizara ya wananchi na pia tunatambua kwamba Mheshimiwa Rais kwa nia ya dhati na mapenzi yake kwa Watanzania, ameweza kutafuta fedha nyingi za miradi ya maendeleo na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza na kutoa ushuhuda wa mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayafanya katika majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anagusa mioyo ya Watanzania, hivyo, inahitaji tuendelee kumuunga mkono na kumtia moyo ili aweze kuendelea na kazi kubwa ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Kwa muktadha huo, ninaomba sisi wote, kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja alichangia hapa, Mheshimiwa Dkt. Kigwangwalla alisema tuunge mkono kampeni ile ya “Nasimama na Mama Samia.” Naomba tuitangazie dunia kwamba sisi Watanzania tunasimama na Dkt. Mama Samia na hakuna mbadala. Tumtie nguvu Mheshimiwa Rais ambaye tayari anafanya kazi kubwa ili aweze kuendelea kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)