Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka ya afya njema na uhai. Pia natumia fursa hii kwa dhati ya moyo wangu kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu kuendelea kuniamini kumsaidia yeye mwenyewe na pia kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mchengerwa katika kuwatumikia wananchi katika dhamana hii muhimu ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Namuahidi Mheshimiwa Rais kwamba, nitaendelea kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa na unyenyekevu wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana viongozi wetu wa kitaifa nikianza na Mheshimiwa Dkt. Philip Isdory Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Tunawashukuru sana viongozi wetu na tunawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuliongoza Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunashukuru kwa namna ambavyo mnatupa maelekezo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili tuweze kutoa huduma kwa wananchi kupitia Wizara hii ya wananchi ambayo Mheshimiwa Rais amemwaga mamia ya mabilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Waheshimiwa Wabunge mmesema, kazi yetu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni kutekeleza ili wananchi wanufaike na matunda yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati kabisa, namshukuru sana bosi wangu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa. Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa ni binadamu, ni mtu na nusu, ni mchapakazi. Kwa kweli, kwangu mimi Mheshimiwa Waziri wewe ni zaidi ya mwalimu, ni zaidi ya mlezi. Nakushukuru sana. Nakuhakikishia kwamba nitaendelea kukupa ushirikiano wa kila aina kuhakikisha unatekeleza majukumu yako uliyopewa na Mheshimiwa Rais katika kuwatumikia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Chief Whip wetu; mama mchapakazi, hodari, mwenye upendo na mnyenyekevu. Tunakushukuru sana kwa malezi yako na namna ambavyo umeendelea kutuelimisha sisi vijana wako katika kutekeleza majukumu haya. Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kukushukuru sana wewe mwenyewe kwa kazi kubwa unayoifanya kwa uhodari wa hali ya juu katika kuliongoza Bunge hili Tukufu. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa IPU. Vilevile nawashukuru sana Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Kamati kwa namna ambavyo wameendelea kutupa ushirikiano Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Wanging’ombe, wapiga kura wenzangu, kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Ninawahakikishia kupitia Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nitaendelea kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo ya Wanging’ombe, niko timamu, niko vizuri. Nawahakikishia kabisa mwaka 2025 wale wanaopashapasha wanapoteza muda. Niko timamu kweli kweli, na kwa hakika nitarudi hapa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Jimbo la Wanging’ombe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kumpa pole Mheshimiwa Waziri wetu kwa dhahama ya mafuriko katika Jimbo la Rufiji. Mheshimiwa Waziri tumekuona ulivyo na upendo mkubwa kwa wananchi wa Rufiji, pamoja na majukumu ya Wizara, tumekuona kwenye mitumbwi, tumekuona wakati wa mvua, wakati wa jua, unaendelea kuwatetea wananchi wa Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa wananchi wa Rufiji, mmempata Mheshimiwa Mbunge chuma kweli kweli. Mumtumie kweli kweli, mkimpoteza, mtajuta. Mheshimiwa Mchengerwa ana mapenzi ya dhati, ametoa shilingi milioni 40 ya posho na mshahara wake kwa ajili ya wananchi wa Rufiji. Nani kama Mheshimiwa Mchengerwa? Hongera sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri sana ambayo umeifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa shukrani nyingi sana kwa pacha wangu, Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, dada mchapakazi sana. Kwa wiki moja ameonesha uwezo wake wa hali ya juu sana katika kuitumikia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Karibu sana, nakushukuru sana kwa ushirikiano na ninakupongeza sana kwa namna ambavyo Mheshimiwa Rais amekuamini na ninakuhakikishia kwamba, tutaendelea kukupa ushirikiano ili uweze kutimiza majukumu yako vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Katibu Mkuu Ndugu Ndunguru, Naibu Makatibu Wakuu wote wanne, Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kwa kazi kubwa na ushirikiano wanaotupatia katika kuongoza Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Pia nampongeza sana pacha wangu wa zamani, rafiki yangu, kaka yangu Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi, kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Namtakia kila la heri katika majukumu yake hayo mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika Waheshimiwa Wabunge wametoa michango mingi ya muhimu sana. Nimefanya tathmini wakati Waheshimiwa Wabunge wanachangia, na katika tathmini yangu nilikuwa na observation ambayo ilikuwa na vitu vitatu. Jambo la kwanza nimejifunza kwamba Waheshimiwa Wabunge wote waliosimama kuchangia kwa 100% wamempongeza na kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika kuleta maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru sana na ninawaunga mkono. Tumekuwa mashahidi, tumekuja kwenye majimbo yenu, kwenye kata zenu na kwenye vijiji vyenu, tumeona kazi kubwa ambayo inafanyika. Nawashukuru sana ninyi Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano na mafanikio haya ya Mheshimiwa Rais. Kwa hakika ninyi ni sehemu ya mafanikio hayo kwa sababu mmewasemea wananchi na pia mmesimamia utekelezaji wa miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitafanya kosa nikisahau kumshukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISEMI, Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Makamu Mwenyekiti Nyamoga na Kamati nzima ya TAMISEMI kwa ushauri mzuri. Pia, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Mheshimiwa Halima James Mdee na Kamati nzima wanatusaidia sana kuhakikisha kwamba tunaboresha utendaji wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kundi la pili baada ya lile kundi la kwanza 100% ambao wamepongeza kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais, kundi la pili wametoa ushauri, mapendekezo na maoni muhimu sana ambayo sisi kazi yetu ni kuyachukua na kwenda kuyafanyia kazi ili wananchi wetu waone matunda ya Wabunge, waone matunda ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia, waone matunda ya Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumepokea maoni, mapendekezo na ushauri wenu kwa mikono miwili. Kazi yetu ni kwenda kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, observation yangu ya tatu, Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia wamekuwa na maombi mahususi na maombi hayo kwa kiasi kikubwa ni ya miradi ya maendeleo, miradi kwa ajili ya vituo vya afya, miradi kwa ajili ya zahanati, miradi kwa ajili ya hospitali za halmashauri, majengo ya utawala pia na nyumba za watumishi na miundombinu nyingine za huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati kabisa, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge kusema, katika historia ya nchi yetu, tangu nchi hii imezaliwa hakuna kipindi ambacho kwa kweli kimefanya kazi kubwa ya kuleta huduma za jamii kwa kujenga miundombinu ya huduma za afya, elimu, maji na barabara kama Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitasema tu kwa uchache. Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali hii ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua changamoto za huduma za afya kwa wananchi kwamba wanasafiri umbali mrefu kwenda kufuata huduma, wengine tunawapoteza kabla hawajapata huduma hizo, alitoa fedha shilingi bilioni 191.7 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya za halmashauri 129 katika nchi yetu. Hospitali hizi zimejengwa, wananchi wetu wanatibiwa, ninyi ni mashahidi, tumepunguza sana vifo vya akina mama wajawazito kutoka 556 mpaka 104. Tumevunja rekodi, kasi ya ajabu sana kwa sababu ya uwekezaji mkubwa kwenye vituo hivi vya huduma za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa ninavyoongea, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha shilingi bilioni 55.3 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa hospitali nyingine za halmashauri 73. Kazi inaendelea, fedha iko site, wakandarasi wako site, local fundi wako site wanatekeleza miradi hiyo kusogeza huduma karibu kabisa na wananchi. Tayari hospitali kongwe za zamani 19 zimeshakarabatiwa kwa gharama ya shilingi bilioni 16.6. Fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatukuishia kwenye hospitali za halmashauri, Waheshimiwa Wabunge wamesema na mpango wa Serikali ni kuwa na vituo vya afya vya kimkakati katika maeneo yetu ili wananchi wakitoka kwenye zahanati wapate rufaa ngazi ya vituo vya afya, wakitoka kwenye vituo vya afya wapate rufaa ngazi ya hospitali za halmashauri. Tayari Mheshimiwa Rais ametoa fedha na tayari vituo vya afya 423 vimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 297.3 kote nchini. Waheshimiwa Wabunge mmesema mmepokea vituo hivi, mmesimamia ujenzi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wameongea sana kuhusiana na suala la ukamilishaji wa maboma ya zahanati. Ni kweli, nasi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tulitambua kwamba tuna uhitaji wa kukamilisha maboma ya zahanati. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwapongeza sana wananchi wote, Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, kote nchini kwa kusimamia wananchi kujenga maboma haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Mheshimiwa Rais alishatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma 1,790 ya zahanati kote nchini ambayo yamegharimu shilingi bilioni 88.1. Maboma yaliyo mengi yamekamilika, zahanati hizi zinatoa huduma kwa Watanzania. Niwahakikishie kwamba zoezi hili ni endelevu, na kwenye bajeti ya mwaka huu kuna maboma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, bajeti zinazofuata tutaendelea kutenga kwa ajili ya maboma ili kile kilio cha Waheshimiwa Wabunge kwamba tuna maboma mengi yamekaa muda mrefu, kiendelee kupungua na hatimaye tuje tumalize; tuwe na maboma ambayo yote yamekamilishwa kuwa zahanati na wananchi wetu wanapata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwenye sekta tu ya miundombinu kwenye majengo, Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya shilingi bilioni 528 katika kipindi cha miaka mitatu, haijapata kutokea. Mheshimiwa Rais amevunja rekodi kwa kweli, anastahili kupewa maua yake kwa kazi kubwa sana ambayo ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu nchi yetu imezaliwa pamoja na upungufu wa hospitali za halmashauri, hatukuwahi kuwa na hospitali ya halmashauri hata moja ambayo ina jengo mahususi la wagonjwa wa dharura (Emergency Medical Department). Ndani ya miaka mitatu Mheshimiwa Rais ameshajenga majengo 83 ya Medical Emergency kwa ajili ya hospitali zetu za halmashauri kwa gharama ya shilingi bilioni 24.9. Majengo haya yanatoa huduma, yanahudumia wananchi na kwa hakika yanaokoa maisha ya wananchi wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, hatukuwahi kuwa na jengo maalumu kwenye ngazi ya halmashauri kwenye hospitali zetu za wilaya la intensive care unit (ICU) wagonjwa mahututi. Mheshimiwa Rais ameliona hilo, ameshajenga majengo ya ICU 29 kwa gharama ya shilingi bilioni 7.2 na tulienda pale Nachingwea nakumbuka kwa Mheshimiwa Chinguile, tuliona ICU bora kabisa. Ukiwa pale unafikiri labda uko Muhimbili, wananchi wanapata huduma nzuri kabisa. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa uwekezaji mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya nyuma wagonjwa mahututi walikuwa wakihitaji hewa safi ya oxygen kama sehemu ya matibabu na tulikuwa tunawapoteza wagonjwa wengi sana. Mheshimiwa Rais kwa kutambua hilo, ameshajenga mitambo ya kusafishia hewa safi ya oxygen katika hospitali za kimkakati za halmshauri kote nchini ambazo zinaendelea kuzalisha hewa safi ya oxygen. Wananchi wanapata hewa hiyo katika maeneo hayo, vituo vya afya vinapata kiurahisi badala ya kufuata mkoani au katika hospitali za kanda. Amenunua mashine za kidigitali za x-ray (digital x-ray) 133, hatukuwahi kuwa na hata moja katika halmashauri zetu. Hivi sasa tunazo zaidi ya 133 kwa thamani ya shilingi bilioni 93.88. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa sana imefanyika katika eneo la vifaatiba. Hivi sasa ninavyoongea, halmashauri zetu zote 184 zimepelekewa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda, kila halmashauri ina shilingi milioni 200, shilingi milioni 300, shilingi milioni 500, au shilingi milioni 600 kulingana na mahitaji ya vifaatiba katika halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kama wawakilishi wa wananchi, walipaza sauti ya changamoto ya magari ya wagonjwa, lakini pia changamoto ya magari ya kusimamia (supervision) katika sekta ya afya. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu, Mohamed Omary Mchengerwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi ni mashahidi, Bunge lililopita tulifanya demonstration ya kugawa magari hapa 115, kwa Waheshimiwa Wabunge. Kila jimbo limepata gari la wagonjwa, kila halmashauri imepata angalau magari mawili; gari moja la wagonjwa, gari lingine la usimamizi. Kuna halmashauri zinapata magari zaidi ya mawili. Haijapata kutokea magari mengi kununuliwa kwa wakati mmoja, na hii ni kwa kuwa tunajali afya za wananchi wetu waweze kupata huduma bora sana za afya na kuendelea kupunguza vifo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa maelezo tu haya ni dhahiri tuna ushahidi wa kutosha kwamba kazi kubwa sana imefanyika na hatimaye tuna uhakika hata haya ambayo tumeyasema leo yatakwenda kufanyiwa kazi, kwa sababu tuna ushahidi, tuna evidence kila sehemu kazi kubwa sana imeshafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa nielezee kuhusiana na upungufu wa watumishi. Waheshimiwa Wabunge wameeleza changamoto ya upungufu wa watumishi katika vituo vyetu. Ukifanya tathmini ya haraka unaona kabisa kwamba sababu za ongezeko la gap ya watumishi katika halmashauri zetu na katika sekta ya afya ni ongezeko la vituo vya huduma vilivyojengwa kusogeza huduma kwa wananchi. Maana yake katika kipindi cha miaka hii mitatu ya Dkt. Samia, jumla ya vituo zaidi ya 1,900 vimeongezeka, havikuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuongezeka kwa vituo zaidi ya 1,900, hospitali za halmashauri zaidi ya 139, vituo vya afya zaidi ya 500, automatically watumishi wataonekana ni wachache zaidi. Safari ni hatua tumeanza kwa kusogeza miundombinu, tunakwenda sasa kupeleka watumishi na ndiyo maana Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki cha miaka mitatu tayari ameshaajiri watumishi wa sekta ya afya kwa kada mbalimbali 18,418. Watumishi hawa wamepelekwa kwenye vituo vyetu, wanaendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema ni kwamba Mheshimiwa Waziri wa Utumishi amesema na Waziri wetu wa TAMISEMI, atasema, lakini tayari kuna mpango wa kibali kutoka, kwa ajili ya ajira nyingine za watumishi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge mnaona jitihada za wazi kabisa za Serikali yetu katika kuhakikisha kwamba tunapunguza gap la watumishi katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wameongelea sana suala la miundombinu ya majengo ya utawala katika ngazi za mikoa, wilaya na pia katika ngazi za halmashauri. Pia wameongelea suala la nyumba za viongozi wetu, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na pia Wakuu wa Idara. Naomba niwape taarifa njema kabisa ya kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya ndani ya miaka mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hiki cha miaka mitatu, Serikali imeshajenga nyumba na majengo ya utawala kuanzia ngazi ya mkoa mpaka halmashauri majengo 390 ambayo yamegharimu shilingi bilioni 398.1. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba kazi kubwa sana imefanyika, majengo ya Wakuu wa Mikoa, nyumba za Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na za Wakuu wa Idara zimeendelea kujengwa. Katika bajeti ya mwaka huu pia kazi hiyo itaendelea ili tuhakikishe watumishi wenzetu wanafanya kazi katika mazingira mazuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha bado kuna miradi ambayo itakwenda kutekelezwa ikiwemo ujenzi na ukarabati wa hospitali za halmashauri. Kazi hiyo bado itaendelea. Pia, kazi ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya itaendelea, kazi ya ujenzi na ukarabati wa zahanati itaendelea, pia ununuzi wa vifaatiba, ajira kwa watumishi na majengo ya utawala na majengo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maneno haya, kila mwenye masikio anasikia, kila mwenye macho anaona kazi kubwa sana iliyofanywa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hakika mimi ni Mbunge wa kipindi cha kwanza, lakini ninasema kama mwaka 2025 Waheshimiwa Wabunge sote tuna kila sababu ya kurudi Bungeni kwa kazi nzuri sana ambayo imefanywa na Serikali hii. Sisi tukiwa sehemu ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, tumefanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafikiri Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, bosi wangu, atupe mbinu tu, maana yake miradi ipo, kila kitu kipo, imebaki tu mbinu. Naamini kwa mbinu, tutarudi vizuri kabisa na tutarudi sote kwa ajili ya kujenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu ni Rais msikivu, Mheshimiwa Rais wetu ni Rais mchapakazi, Mheshimiwa Rais wetu ni Rais mnyenyekevu, anajali shida za Watanzania. Kila tukipaza sauti, anaona kabisa tuna uhitaji. Mheshimiwa Rais hajawahi kusita kutuletea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya ziara siku moja Kanda ya Ziwa nikapata taarifa ya miradi ya fedha zilizopokelewa kwa ajili ya miradi mbalimbali. Sasa nilianza Kijiji cha kwanza wakaniambia Mheshimiwa Naibu Waziri, kijiji chetu kimepokea shilingi laki kumi kwa ajili ya utekelezaji na umaliziajia wa zahanati. Sasa sikuelewa, lakini nikaenda kata nyingine wakaniambia Mheshimiwa Naibu Waziri kata yetu imepokea shilingi laki mia tano kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye nilikaa nikafanya tathmini, nikajifunza kwamba walikuwa hawajawahi kuzoea kupata shilingi milioni 500, milioni 50, milioni 10, wao walizoea kupata laki tano, laki saba, laki sita. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amevunja rekodi kwa kupeleka mabilioni na kwa kupeleka mamilioni katika vijiji vyetu, katika zahanati zetu na katika halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tuna kila sababu ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Tuna kila sababu ya kumwomba Mheshimiwa Rais, tuna kila sababu ya kumsemea Mheshimiwa Rais. Mimi pia naungana kabisa na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ambaye alinipokea pale Muhimbili University kwa kusema; “Hashtag - Ninasimama na Mama,” kwa sababu mama kwa kweli ametenda haki katika Taifa hili, amefanya kazi kubwa katika Taifa hili. Kila mtu anaona, kila mtu ni shuhuda, huhitaji kuambiwa, na kwa kweli wanasema, “Kama hujui kusoma, basi hata picha tu huwezi kuona?” Picha inaonekana ya wazi, kazi kubwa sana imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nahitimisha, kwa dhati kabisa nirudie kukushukuru sana wewe mwenyewe, umeendelea kutusaidia sana sisi TAMISEMI kila siku tunajibu maswali hapa, umeendelea kutu-manage vizuri, lakini pia tumeendelea kuwa na fursa nzuri sana ya kuwatumikia wananchi kupitia Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu, namshukuru sana Naibu Waziri mwenzangu, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa ushirikiano mkubwa sana ambao mnanipa. Nirejee kusema hashtag, Simama na Mama Samia, Mama Samia analipa, amefanya kazi kubwa kila mtu ni shahidi. Tuendelee kumwombea Rais wetu ili wananchi wa Tanzania waendelee kuneemeka na maendeleo ambayo Mheshimiwa Rais ameyaleta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana, nashukuru sana. (Makofi)