Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyeniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako hili Tukufu katika kuhitimisha Hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima nikiri kwamba siyo kwa uwezo wangu wala kwa ujuzi nilionao, isipokuwa ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Ninayasema haya kwa sababu siku ya kwanza nimesimama hapa nilikuwa na one thousand MPH wanaita, wadudu 1,000 wa malaria lakini niliweza kusimama kwa sababu Mwenyezi Mungu aliniwezesha. Leo hii wamebaki takribani 220, naamini mpaka kesho, kesho kutwa watakuwa wamemalizika. Kwa hiyo, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na uzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, namshukuru tena Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini ili niwatumikie wananchi wa Tanzania katika nafasi hii ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Mafanikio ya kuwatumikia wananchi ni mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita. Kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI itafanya vizuri na Serikali yote kwa ujumla itafanya vizuri na haya yamedhihirishwa kwa maelezo mengi ya kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Spika wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa pia kuwa Rais wa Mabunge ya Dunia. Pia nakupongeza wewe, natambua katika kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Spika atakuwa hayupo, basi majukumu mengi yatakuwa ni yako. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kukupongeza pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawapongeza Wenyeviti wa Kamati za Bunge na Wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi wa Bunge. Hapa nampongeza sana Mheshimiwa Joseph Mhagama ambaye wakati nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ambayo nilidumu katika vipindi vitatu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, alikuwa ni Mjumbe wangu katika kipindi chote. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Joseph Mhagama kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii na wale ambao hawakupata fursa ya kuchangia kutokana na sababu mbalimbali, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wote utasaidia kutoa mwelekeo wa kuisimamia Serikali. Pia utatoa mwelekeo wa kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Mafungu yote 28 ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitaishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inayoongozwa na Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi na Mwenyekiti wa Kamati hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge na Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati, kwa namna ya kipekee walivyoandaa na kuwasilisha taarifa ya Kamati yenye maoni kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka 2023/2024 na uchambuzi wa Mpango na Bajeti kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2024/2025, kwa mafungu yote 28 yanayosimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Maoni yaliyotolewa yataboresha na kuimarisha utendaji wa huduma bora kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Halima Mdee, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC na Wajumbe wote. Hakuna ushauri wenu ambao mmeutoa nitauacha. Niwathibitishie kwamba ushauri wenu ni nguzo ya utendaji wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imeweza kutekeleza majukumu kwa ufanisi kutokana na ushirikiano mkubwa tulionao ambao tunapatiwa na Waheshimiwa Wabunge. Kila hoja za Waheshimiwa Wabunge wanazozitoa, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwetu ni utekelezaji tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue fursa hii niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa maoni yao. Wapo Wabunge waliozungumza na wapo waliotuandikia. Napenda pia kutambua mchango mkubwa wa viongozi wenzangu, tangu nilipowasilisha hotuba hii ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika hili Bunge lako Tukufu ambayo leo inahitimishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nawashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Festo John Dugange, Mbunge huyu wa kudumu. Pia Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Mbunge. Nawashukuru sana kwa namna walivyonisaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nichukue fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, wanachapa kazi sana ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Nawaomba endeleeni kuchapa kazi kumsaidia Mheshimiwa Rais, ninyi mkiwa ni Wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, mkiwa ni washauri wa karibu wa Mheshimiwa Rais katika Mikoa mliyopangiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru pia Wakuu wa Wilaya wote nchi nzima kwa ushirikiano wao walionipatia katika kipindi hiki. Aidha, naishukuru Menejimenti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ikiongozwa na Katibu Mkuu, Ndugu Adolf Ndunguru na Wasaidizi wake wote kwa ushirikiano mkubwa walionipatia katika uchambuzi na kuandaa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili mpango wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa Serikali ni wananchi ambao pia ndiyo waajiri wa Serikali. Hivyo, ninawashukuru sana wananchi wote ambao wamekuwa wakitufuatilia toka siku ya kwanza. Tunawasilisha hotuba ya bajeti hii, nawashukuru sana wananchi. Pia wapo ambao wamekuwa wakituandikia, wapo ambao wamekuwa wakitupa taarifa na kutupa maoni mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea kuyafanyia kazi maoni mbalimbali tukitambua kwamba Wizara hii ni yao, Wizara hii ni Wizara ya wananchi. Nawashukuru sana pia kwa sababu wananchi ndio waliotupa ridhaa ya kuwatumikia. Kwa hiyo, tutahakikisha maoni yao na namna wanavyoendelea kutushauri kupitia njia mbalimbali, basi tumeyafanyia kazi ili kuendeleza ustawi wa wananchi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lilizungumzwa sana linalohusu ugatuaji wa madaraka (D by D). Ningetamani kwanza nianze na jambo hili. Mjadala wa siku tatu wa Bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, umedhihirisha bila shaka yoyote umuhimu wake wa maendeleo na ustawi wa wananchi. Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, wametoa sauti zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge hawa ni sauti ya wananchi na wametanabaisha ndani ya Bunge hili, michango yao iligusa maeneo yote mtambuka na ya kisekta, kwa maana yanavyogusa na kuhusika na maisha ya kila siku ya wananchi ambayo TAMISEMI imepewa dhamana ya kuyasimamia na kuyatekeleza. Hii ndiyo Wizara inayowahusu. Hii ndiyo Wizara inayowagusa wananchi moja kwa moja katika nyanja zote za maendeleo na maisha ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo aina mbalimbali za ugatuzi wa Madaraka. Hapa naomba nizitaje, tuna Decentralization by Deconcentration; pili, tunayo Decentralization by Delegation; tatu, tunayo Decentralization by Devolution. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ya kwanza ni pale Serikali Kuu inaposhuka katika ngazi za chini na kuweka watumishi wanaowajibika moja kwa moja kwa Wizara zao za kisekta katika Serikali Kuu. Decentralization by Delegation ni pale madaraka yanabaki kuwa ya Serikali Kuu tu na Serikali Kuu imeyakasimu kwa Serikali za Mitaa. Hii ya tatu na ya mwisho ni ya ugatuzi wa madaraka yote kwa Serikali za Mitaa ambazo zimechaguliwa na zinawajibika moja kwa moja kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaotumika sasa nchini ni wa ugatuzi wa madaraka kwa wananchi wa aina ya Decentralization by Devolution. Uamuzi wa kuchukua mfumo huu wa Decentralization by Devolution, ulipendekezwa na kukubalika utumike kutokana na uzoefu uliotokana na changamoto na matatizo ya aina za mifumo ambayo haikuipa umma (wananchi) mamlaka ya kupanga, kuendesha, kusimamia na kuwajibisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu huu wa kuimarisha madaraka ya umma mwaka 1983, Halmashauri Kuu ya CCM katika mapendekezo yake ya juu ya marekebisho ya Katiba ilipendekeza kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itamke bayana kwamba kutakuwa na Serikali za Mitaa katika kila kijiji, wilaya na mji.
Mheshimiwa Naiu Spika, aidha, Halmashauri Kuu ya CCM pia ilipendekeza kuwa, Katiba vilevile itamke majukumu makubwa ya Serikali za Mitaa pamoja na uhusiano wake kwa Serikali Kuu. Mapendekezo haya ya CCM ndiyo chimbuko la Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika 1984, kuwa na sura inayohusu Madaraka ya Umma yenye Ibara kuhusu Serikali za Mitaa na kazi za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa ugatuzi wa madaraka kwa umma nchini umo katika Ibara ya Nane ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayosisitiza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo, moja, wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii; pili, lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi wake; na tatu, wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali kwa mujibu wa masharti ya Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na msingi wa msimamo huo kuwa wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote katika nchi, Ibara ya 146(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inabainisha madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa. Hii ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Katika kutekeleza hilo, Ibara hiyo inatamka bayana kuwa vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mpango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao nchini kote kwa ujumla, kwa maana ya kwamba mamlaka inapelekwa kwa wananchi na watashiriki moja kwa moja katika maamuzi ya Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada zozote za kudogosha Mamlaka ya Serikali za Mitaa siyo tu kinyume cha sheria, lakini ni kukiuka misingi au msingi muhimu wa kutuletea maendeleo kwa wananchi. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliliona hili na aliona umuhimu huu. Kwa maneno yake alisema, kwa sauti yangu lakini nitamnukuu; “Kuna baadhi ya mambo nisingefanya tena kama ningekuwa Rais kwa mara nyingine. Mojawapo ni kufuta Mamlaka za Serikali za Mitaa na lingine ni kuvunja Vyama vya Ushirika. Tulikosea, hatukuwa na subira na uelewa mpana. Tulikuwa na taasisi hizi mbili kwa ajili ya ushirika wa wananchi, lakini tuliziondoa. Ni kweli kwamba Serikali za Mitaa zilikuwa na changamoto ya kuogopa kufanya maamuzi, lakini badala ya kuzisaidia, tulizifuta.” Huu ni mwisho wa kunukuu. Haya ni maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoyatoa wakati akihojiwa na Waandishi wa Habari mwaka 1984. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kujadili Hotuba ya Mpango wa Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, jumla ya Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 76 walipata fursa ya kuchangia. Kati yao Wabunge wanne walichangia kwa maandishi. Hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge zilifafanuliwa vizuri na Waheshimiwa Naibu Mawaziri, lakini hapa nitazungumza hoja za jumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge zipo katika maeneo yafuatayo: -
(i) Serikali ilipe stahiki za watumishi ikiwa ni pamoja na mafao na fedha za likizo wanazodai walimu ili wafanye kazi vizuri;
(ii) Serikali iongeze fedha TARURA kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara;
(iii) Serikali kuajiri watumishi wa kada ya afya, elimu na ujenzi ili kukabiliana na upungufu uliopo katika maeneo mbalimbali nchini katika sekta za elimu, afya na ujenzi;
(iv) Ukamilishaji wa ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya na elimu katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ukamilishwe;
(v) Ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya utawala kwa wakati;
(vi) Serikali ijenge nyumba za watumishi ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, hususan kada za afya na elimu;
(vii) Ofisi ya Rais, TAMISEMI iandae mwongozo utakaowezesha Halmashauri kuwatumia kwa mkataba wataalamu waliostaafu na kwa kujitolea, wenye utaalamu wa kutumia vifaa vya kisasa kwa kuwa vifaa vingi havitumiki kwa kukosa wataalamu wenye ujuzi wa kuvitumia;
(viii) Fedha za CSR zina matumizi mabaya kutokana na ukosefu wa mwongozo wa kusimamia matumizi ya fedha hizo;
(ix) Serikali iongeze lengo la kukusanya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, baada ya kufungamanisha mifumo kwa kuwa bado kuna mianya ya upotevu wa mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa;
(x) Utekelezaji wa ahadi za viongozi;
(xi) Ukarabati wa shule kongwe;
(xii) Halmashauri na wananchi kujengewa uwezo wa kufanya biashara ya kaboni ili kuongeza mapato ya ndani; (Makofi)
(xiii) Watumishi wanaofanya makosa ya kiutendaji katika kituo kimoja wasihamishwe kupelekwa kituo kingine hadi hatua za kinidhamu zitakapochukuliwa na Mabaraza yao ya Taaluma yahusishwe; (Makofi)
(xiv) Serikali iwajengee uwezo Wakuu wa Wilaya kuhusu utawala bora na majukumu katika Wilaya zao; na
(xv) Fedha za mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ziwafikie wananchi zitakapoanza kutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia maeneo niliyoyataja hapo juu, napenda nitoe ufafanuzi wa hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge wakati wa kujadili mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2024/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja za jumla; kutowasilishwa kwa wakati michango ya watumishi kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, natambua uwepo wa changamoto za Mikoa na Halmashauri kushindwa kuwasilishwa kwa wakati michango ya watumishi kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Hadi kufikia Oktoba, 2023 Mikoa saba na Halmashauri 177 zilikuwa hazijawasilisha michango na tozo za shilingi yenye thamani ya shilingi bilioni 132.86 baada ya punguzo ya tozo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, kuanzia Julai, 2024 Serikali imeridhia kulipa mishahara ya watumishi waliokuwa wakilipwa kwa mapato ya ndani kwa Halmashauri zenye mapato ya ndani yasiyozidi shilingi bilioni 10 na michango yote ya watumishi italipwa moja kwa moja na Hazina. Vilevile ili kupunguza deni kwa waajiri, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeridhia kutoa punguzo ya tozo kwa 88%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kutoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kulipa deni la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa mujibu wa makubaliano waliyofikia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii. Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi watakaoshindwa kulipa michango ya madeni watachukuliwa hatua za kinidhamu wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni utaratibu wa wataalamu wanaojitolea katika sekta za afya na elimu. Natambua uwepo wa watalaamu wanaojitolea kwenye sekta ya afya na elimu katika Halmashauri mbalimbali. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imeandaa mwongozo wa walimu wa kujitolea katika elimu ya awali, msingi, sekondari pamoja na vyuo vya maendeleo ya wananchi wa Tanzania Bara uliotolewa Juni, 2023. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeandaa mwongozo wa Watalaamu wa Afya wanaojitolea uliotolewa Julai, 2021. Miongozo hiyo inatoa utaratibu wa mgawanyo wa majukumu ya wadau katika kuwapata na kuwasimamia watalam husika. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara za kisekta itasimamia utekelezaji wa mwongozo huo, pamoja na miongozo mingine inayotolewa ili kusaidia kupunguza ombwe la uhaba wa watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, natambua uwepo wa ahadi mbalimbali ambazo zinatolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi wakati wa ziara na mikutano. Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea kusimamia utekelezaji wa ahadi hizi za viongozi wetu ambako katika sekta ya barabara. Naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba ujenzi wa barabara za lami za halmashauri 64 nchini za kilometa moja kwa kila Halmashauri kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 32 umekamilika. Ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa tano kuelekea Kiwanda cha Mbolea kule Nala kwa kiwango cha lami umekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2024/2025 Serikali itakamilisha utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya vya Nkome katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ngimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Kijiji cha Mingumaro, Kata ya Usagali katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Hizi zote ni sehemu ya ahadi za viongozi. Ahadi nyingine za Viongozi Wakuu zitaendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na ahadi ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa hivi karibuni alipotembelea kule Nzega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea pia mchango wa Mheshimiwa Hussein Bashe na hii ni kukumbushia ahadi ya Mheshimiwa Rais kuhusu ujenzi wa soko, stendi pamoja na maeneo mengine. Hapa namwagiza Katibu Mkuu kuhakikisha kwamba anafuatilia suala hili kupitia Ofisi ya Mheshimiwa Rais mwenyewe, pia kupitia Wizara ya Fedha ili utekelezaji wa mpango huu, ahadi hii ya Mheshimiwa Rais ianze mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukamilishaji wa maboma ya miundombinu ikiwemo ya elimu na afya, natambua uwepo wa maboma ya miundombinu yakiwemo ya elimu pamoja na afya, Novemba, 2023 Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilifanya tathmini na kubaini uwepo wa maboma 21,914 ya sekta ya elimu na sekta ya afya. Maboma haya 21,914 yanahitaji takribani shilingi bilioni 455.51 kwa ajili ya ukamilishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, katika kipindi cha miaka mitatu, 2020/2021, 2023/2024, Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 255.55 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma katika sekta ya elimu na sekta za afya, ambapo jumla ya maboma yenye 1,795 ya zahanati yenye thamani ya shilingi milioni 89.75 na maboma 12,700 ya sekta ya elimu yenye thamani ya shilingi bilioni 165.8 yamekamilishwa. Kati ya maboma hayo, maabara za masomo ya sayansi ni 2,745, madarasa ni 9,397, mabwalo ni 87 na mabweni ni 471. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji huu wa Serikali ni kwa sababu wananchi walionesha mfano. Wao kwa kushirikiana na Wabunge wamejitolea na kujenga maboma na Serikali ikasema haitakuwa nyuma na kuwaacha wawakilishi wa wananchi waliowashawishi na kuwashauri wananchi kujenga maboma na ndiyo sababu Serikali imetoa kiwango hiki cha fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu, kwa mwaka 2024/2025, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepanga kukamilisha maboma 6,415 ya miundombinu katika sekta ya afya na sekta ya elimu. Maboma haya 6,415 yatagharimu takribani shilingi bilioni 183.63. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 52.86 ni fedha za ruzuku ya Serikali Kuu na shilingi bilioni 130.77 ni fedha za mapato ya ndani ya halmashauri. Aidha, ukamilishaji wa maboma mengine yaliyobaki utaendelea kadiri ya upatikanaji wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ninawaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Uanzishwaji wa maboma ili kuzuia uanzishaji wa maboma usiozingatia mwongozo kwa lengo la kuwa na uratibu mzuri wa michango ya wananchi na wadau. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu ujenzi wa majengo ya utawala kwenye mikoa na halmashauri. Natambua uwepo wa majengo ya utawala ya mikoa na halmashauri ambayo yanaendelea na ujenzi. Katika mwaka 2023/2024, takribani shilingi bilioni 171.34 ziliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi, ukamilishwaji na ukarabati wa Ikulu ndogo nane, ofisi 16 za Wakuu wa Mikoa, ukarabati wa ofisi 22 za Wakuu wa Wilaya, ujenzi wa majengo ya utawala katika halmashauri 72 na ofisi 19 za Maafisa wa Tarafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Machi, 2024, majengo ya utawala katika halmashauri 12 yamekamilika na yanatumika na majengo 60 yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Hadi Machi, 2024 ukamilishaji na ukarabati wa nyumba 57 za viongozi ngazi za Tawala za Mikoa ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba mbili za Wakuu wa Wilaya zimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda, naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba, katika mwaka 2024/2025, Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea na ujenzi na ukamilishaji wa miradi 78 ya majengo ya utawala. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, omba pesa. Mheshimiwa Waziri, malizia hitimisho, omba pesa. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa taarifa hii nimeichapa vizuri, naomba taarifa yote iingie kwenye Kumbukumbu Rasmi za Bunge. Nihitimishe kwa kusema kwamba, naomba Bunge lako likubali kuidhinisha matumizi ya mafungu 28 ya shilingi 10,125,220,403,767. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)