Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kutoa ushauri wangu kwenye Wizara ya Nishati. Kwanza Waheshimiwa Wabunge naomba tupitishe bajeti hii kwa sababu ukisikiiza yaliyosemwa yanatia matumaini. Kwa hiyo, tuipitishe na ni kielelezo kwamba Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Rais inafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa leo napenda kusisitiza umuhimu wa vyanzo vipya vya umeme mwingi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wetu. Naomba nirudie hilo, umeme mwingi, kwa hiyo siyo tu energy mix, Hapana, ni umeme mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mahali ambapo tunaanzia mpango wetu wa maendeleo ambao unaisha mwakani, tulisema kufika mwakani 2025 pato letu ukiligawa kwa kila mtu kwa mwaka zifikie dola 3,000 - GDP per capital. Kwa hiyo, tunavyojadili yote haya kwenye haya mambo ya bajeti lazima tujipime tumefika wapi?
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, mipango yetu ilipangwa kwamba kufika mwakani tunapaswa kuwa tumepata Megawatt 5,000, kwa hiyo, GDP per capital hatujaifikia, Megawatt 5000 hatujafikia, lakini tunaelekea huko. Kufikia huko ni lazima uchumi wetu ukue kwa asilimia nane hadi 10%. Sasa vyanzo vipya ni hivi vifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, vyanzo vipya ni sehemu ya vyanzo vingine ambavyo vipo duniani na Mheshimiwa Waziri wa Nishati ameongelea nishati jadidifu (renewable energies), dunia yote mapambano ya tabianchi yanataka tuwekeze kwenye renewable energies. Sasa hivi vyanzo ni vingi sana, ni 10 vingine 20 lakini muhimu sana ni saba.
Mheshimiwa Spika, chanzo cha kwanza ni solar, cha pili ni wind, cha tatu geothermal, cha nne bio energies (biomass, biogas), umeme wa maji (hydro), mawimbi ya baharini (ocean tides and waves) na cha saba ni hydrogen. Samahani nikitaka kuyaweka kwenye Kiswahili nitatumia muda mwingi kujaribu kutafsiri, lakini nadhani wengi wanaelewa hydrogen ni nini.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa nini vinakuwa muhimu sana? Wanasayansi wamepiga hesabu kwamba jua lina uwezo wa kutupatia umeme wa kiasi cha 173,000 trillion watts. Sasa ukisikia nasema trillion watts maana yake ni Megawatts milioni moja. Kwa hiyo, jua linaweza likatupatia umeme ambao ni zaidi ya 10,000 ya umeme ambao tunauhitaji; jua peke yake, dunia nzima.
Mheshimiwa Spika, tukichukua upepo una uwezo wa kutupatia umeme ambao ikifika mwaka 2040 tutakuwa tuna uhitaji yaani ni zaidi ya trillion watts 36,000.
SPIKA: Profesa, ili usikike vizuri…
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Ndiyo.
SPIKA: Hicho kitabu ulichoshika ukishikie pembeni kidogo ili kile kisemeo kiwe mbele yako moja kwa moja.
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika, utaniongeza muda. Walibadili kilikuwa kirefu wakaweka kifupi, sasa naona nimesogea kwenye hiki kirefu. (Kicheko)
MBUNGE FULANI: Zima kile kimoja.
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Hapana, acha viwe viwili, leo tunaenda na viwili.
Mheshimiwa Spika, hapo unanisikia vizuri! (Kicheko)
SPIKA: Nakusikia vizuri sasa, unaweza kuendelea.
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kwamba hiki ninachokiongea ni lazima tuwekee maanani kweli kweli, maana yake tunang’ang’ana na vyanzo vingi. Mimi nataka kuwathibitishia vyanzo vya uhakika.
Mheshimiwa Spika, yaani jua linavyopiga ardhini square meter moja unapata kama bulb nne au tano za umeme; ni watts 342. Sasa nataka kuonesha kwa nini Tanzania twende huko tusiache mengine. Nimechukua mfano wa India na China.
Mheshimiwa Spika, India na China tulikuwa pamoja miaka ya 1950 na 1960, umasikini wetu ulikuwa unafanana. Sasa hivi mwezi uliopita Machi mwaka huu ule uwezo wa kuzalisha umeme (installed capacity) wa India kutokana na vyanzo hivyo; sikiliza vizuri sana. Solar ni Gigawatts 82. Kwa hiyo, ukisikia nasema Gigawatts, wewe zidisha kwa 1,000 upate Megawatts.
Mheshimiwa Spika, upepo wana Gigawatts 46, hii biomass aliyokuwa anaongea, ni karibu Gigawatts 10. Narudia tena. Gigawatts zidisha mara 1,000 halafu ukisikia Terawatts zidisha mara 1,000,000. Kwa hiyo, sisi kama Taifa tunataka kuendelea lazima tuwekeze kwenye solar, wind, biomass na vingine.
Mheshimiwa Spika, Mfano mwingine, India imepanga kufikia mwaka 2030, umeme wa kutokana na jua na upepo utakuwa Gigawatts 500 (Megawatts 500,000). Mwaka 2023 China kwenye solar walikuwa na Gigawatts 430. Siyo kwamba wanapanga, hizo ni installed capacities na mwaka huu wakichukua jua na upepo wana Gigawatts 609.
Mheshimiwa Spika, sasa hapa nitoe shukurani kwa REA, wameanza kuona umuhimu wa umeme wa jua na ninadhani mfano mzuri utakuwa Jimboni kwangu, watakuja kuweka kule kisiwani umeme wa jua. Kwa hiyo, nitakuwa nao kwa ukaribu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aina ya pili ni upepo. Upepo ambao unaweza kuzalisha umeme lazima speed yake iwe karibu mita nne kwa sekunde, yaani kilometa kwa saa ziwe ni kati ya 12 na 14. Ikiwa 50 mpaka 60 kama speed ya gari uzalishaji unakuwa ni mkubwa sana, ikiwa zaidi ya 90 inaharibu turbines.
Mheshimiwa Spika, sasa angalia mfano wa nchi nyingine na ndiyo tunapaswa kwenda huko. India wana umeme wa upepo Gigawatts karibu 43, kwa hiyo ni Megawatts 43,000. Wanataka ikifika mwaka 2030 wafikishe Gigawatts 170 na hii tutaongea kwenye mipango. Tusiende na hizi Megawatts ndogo ndogo, haziwezi kukimbiza uchumi sana.
Mheshimiwa Spika, nakuja China, kwenye upepo wana Gigawatts 440 na wanategemea ikifika mwaka 2030 upepo na jua uweze kuzalisha umeme wa Gigawatts 1,300 (1,300,000 Megawatts). Kwa hiyo, siyo ajabu mkaenda kununua vitu India na China kwa sababu huu umeme wao ni wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, siyo kwamba jua na upepo hauwezi kutoa umeme wa viwanda. India na China wanatuonesha hapa, mwaka 2050 China inategemea ifikishe umeme wa upepo Gigawatts 1,000 (Megawatts 1,000,000). Kwa upande wa Afrika na Watanzania tujifunze kwa wenzetu Wakenya, wao ndio wana umeme mwingi kwa bara zima la Afrika, wana Megawatts karibu 440 na ni kule Lake Turkana Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, aina nyingine niliyotaka kuongelea, nimechukua tatu tu, yaani jua, upepo na joto ardhi (geothermal). Nyuzi yaani temperature ambazo zinahitajika kuzalisha geothermal, maji yale yawe yanachemka kwa kiwango siyo chini ya 50 to 100 Degree Celsius. Ni kama majimoto, lakini yanaongezeka kabisa.
Mheshimiwa Spika, sasa kufikia mwaka 2023 joto ardhi duniani capacity yake ilikuwa karibu gigawatts 17 (Megawatts karibu 17,000) na mfano mzuri kwetu sisi Afrika tunaenda kuuchukua Kenya. Kenya ni ya kwanza kwa bara la Afrika, Kenya ni ya sita duniani kwa umeme unaotokana na joto ardhi. Wanazo Megawatts za joto ardhi karibu 1,000 ni 988, lakini potential yaani uwezo uliopo kwenye Bonde na unazalishwa kwenye bonde ni kati ya Megawatts 5,000 na Megawatts 10,000 kwa Kenya.
Mheshimiwa Spika, sasa ukichukulia Bonde la Ufa la Kenya ukilinganisha na la Tanzania, sisi tuna Bonde la Ufa refu zaidi, lakini hicho siyo kigezo muhimu, muhimu ni ule upana (thickness). Ili upate joto ardhi zuri ni lazima ule upana wa ardhi yako uwe chini ya kilometa mbili, ndiyo wanaweza wakachimba, wakafika chini na kutoa huo mvuke ambao utaendesha turbines na kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi umeme wa Kenya ukilinganisha na wa Tanzania, zamani tulikuwa tunawazidi, au tunalingana nao lakini wao kwa ujumla umeme wao sasa hivi wana Megawatts 3,300. Kwa hiyo, ni karibu na Gigawatts 3.3. Sasa ukilinganisha za Kenya ambaye ana uchumi mkubwa Afrika Mashariki Gigawatts tatu, linganisha na nilizowapatia za China na India.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine ni Ethiopia. Wenyewe walianza kuzalisha jotoardhi mwaka 1998, lakini sasa hivi wana Megawatts kidogo tu 7.5.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania, kwa mipango mizuri tuliyoisikiliza, tulitengeneza ramani inayoonesha maeneo ambayo tunaweza tukavuna umeme wa jua kwa wingi sana na eneo lililokuwa linaongoza ni Shinyanga, sasa inabidi hiyo ramani ipitiwe kwa sababu ya tabianchi, tunahitaji panels zifanye kazi. Tunahitaji 15 – 35 degree Celsius, hiyo ndiyo temperatures za chini kabisa za solar panel kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napendekeza wataalamu wetu wa TANESCO na REA wapitie solar map, wind map hata ikiwemo ile ya Makambako, speed yake ya umeme tupitie halafu na Singida. Geothermal Map, nawaambia geologists wapitie tena ile ramani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kumalizia ni kwamba hivi vyanzo ambavyo tunavyo kama tunataka kufikia hiyo GDP per capita ya 3,000 US Dollars ni lazima tuwe na umeme wa zaidi ya Megawatts 10,000 ambayo ni Gigawatts moja na tutaipata kutoka vyanzo hivyo nilivyovitaja ambavyo ni solar, wind na geothermal, ahsante. (Makofi)