Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba nami nianze kwa kusema kwamba naunga mkono Hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri. Kipekee nianze kwa kutambua na kupongeza kazi nzuri ambayo inafanywa na Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wote.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, kwa hiyo pia naomba kupongeza na kutambua Hotuba nzuri ya Mwenyekiti wangu wa Kamati na kwamba yale yote yaliyosemwa na Kamati, nayaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana Wizara ya Nishati, kwanza kwa ubunifu waliokujanao kwenye Wiki ya Nishati. Naweza kusema ile Wiki ya Nishati imemaliza hotuba yangu kama asilimia 80 na itakuwa hivyo karibu kwa Wabunge wote kwa sababu tulipata nafasi ya kutosha ya ku-interact na Mameneja wetu, lakini tulipata majibu mengine sahihi kwenye Wiki ya Nishati. Kwa hiyo, sasa ninachotaka kusema hapa, kwa kweli tofauti sana na Mwalimu wangu Profesa Muhongo, yeye alikuwa anafundisha, lakini mimi kidogo nitazungumza shida za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Waziri amesema umeme umeongezeka kwa takribani asilimia 14 na hali ya umeme sasa imetulia. Tunaipongeza sana Serikali kwa juhudi kubwa ambayo imefanya na niipongeze pia Serikali kwa kujibu kiu ya wananchi. Wananchi walikuwa wanalalamika sana na maeneo mengi sasa hivi malamiko yamepungua. Kwa hiyo, nina uhakika kwamba hali hii itaendelea kuwa hivyo hata baada ya hizi mvua nyingi ambazo zinaendelea sasa hivi kwisha.

Mheshimiwa Spika, kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri, amesema karibu wanakamilisha usambazaji wa umeme kwenye vijiji vyote Tanzania. Napongeza sana juhudi hizo. Kipekee mimi nianze kwenye Jimbo langu kwamba ninaishukuru sana Serikali. Sasa Jimbo langu la Geita Mjini lina vijiji 15 na mitaa 65, karibu katika kila kijiji, vijiji vyote umeme umefika, na pia mitaa yote kazi inaendelea. Mheshimiwa Waziri, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa hatua iliyokuja ya kupeleka umeme kwenye vitongoji. Sasa hapa nina maoni. Kule kwenye vijiji ambako tumepeleka umeme tumepeleka takribani watu wasiozidi 10 au 15. Kwa hiyo, unakuta katika kijiji kile kile ambacho umeme upo, wanaotaka umeme ni watu karibu 50, umeme umefikia watu 10 mpaka 15. Taasisi nyingi za eneo lile unakuta umeme haujafika, lakini tayari hesabu ya Serikali ni kwamba umeme umefika kwenye kila Kijiji.

Mheshimiwa Spika, kilio cha wananchi wa eneo lile ni kwamba umeme umefikia watu wachache. Sasa ombi langu ni kwamba mpango wa diversification ambao ulizungumzwa na Waziri, ungewekewa mkakati maalum ili wote wanaohitaji umeme kwenye vijiji ambavyo tumeshafikisha umeme wa REA waweze kupatiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi namna ilivyo, umeme huu unatuchonganisha sana kwa sababu inabidi Diwani na Mwenyekiti wa Kijiji wawe wa mwisho, maana hao ni rahisi kumwambia Mkandarasi wapelekee kuliko wananchi kukosa halafu akapata Diwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maeneo mengi umeme umeenda. Walioomba ni wengi kuliko uwezo wa mkandarasi. Sasa naiomba Serikali, wakati tunafikiria kwenda kwenye vitongoji, Mheshimiwa Waziri na hapa nilitaka niweke kumbukumbu vizuri. Vitongoji vingi wananchi wako scattered na nimeona kwa experience ya kwenye vijiji nguzo zinazaoenda ni chache, kwa hiyo, matokeo yake umeme unakuwa concentrated kwenye center peke yake.

Mheshimiwa Spika, sasa sina uhakika na study iliyofanyika kwa sababu kwenye vitongoji vingi utakuta wanaotaka umeme wako zaidi ya mita 200 au 400 kutoka kwenye mji mwingine. Sasa hawa wote wanahitaji kupata haki hii ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa vizuri kabisa na Kamati, tulipofanya ziara tumegundua kwamba sehemu nyingi ambazo umeme wa REA umefika na baada ya REA kuondoka, wanapoanza kuomba TANESCO wanakutana na bei kubwa kwa sababu mkandarasi wa REA ameshaondoka, ambayo siyo tena shilingi 27,000 na kwa sababu ni bei ghali, wanakijiji wengi hawawezi kulipia shilingi 300,000.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba uje mpango ambao utaendeleza, siyo tu ionekane hawa watu 10 ndio waliopata hiyo bahati, hata baada ya wale wakandarasi wa REA kuondoka, basi uje mpango mahususi ambao utawawezesha wananchi katika maeneo yale kuendelea kupata umeme wa shilingi 27,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuongea kwenye eneo hili, tumekuwa na mpango wa kusambaza mitungi ya gesi. Tunakushukuru sana tulipata bahati ya kwenda India, tukafanya ziara kubwa na ya kutosha kama Kamati, tukajifunza namna ambavyo zoezi hili limeratibiwa na linafanyika vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi mitungi ambayo tunaisambaza kama kuchochea wananchi wengi kwenda kwenye nishati safi ni mitungi midogo ya kilo sita. Kwenye familia zetu huko vijijini, watu wachache ni watano. Mitungi hii inaweza kutumika kwa wiki mbili au wiki moja. Sasa shida iko wapi? Moja, nadhani sasa Wizara inatakiwa kujipanga vizuri kuhakikisha kwamba upatikanaji wa hii gesi hasa kwenye vijiji unaratibiwa vizuri ipatikane kwa wingi ili kusudi mtu asifuate mtungi wa gesi kwa gharama kubwa kuliko gesi yenyewe anayoifuata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule India tulijifunza nini? Kwanza walitambua watu ambao wanataka kuwapa punguzo la mitungi ya gesi na hawa ni karibu ya 50% ya population ya India. Kwa hiyo, Serikali ilichokifanya, iliwatambua na baada ya kuwatambua ikawasajili, ilipowasajili ikapeleka ile mitungi ya kati ya kilo 15.

Mheshimiwa Spika, ile mitungi ya kilo 15, hao watu waliopewa waliposajiliwa wamewekwa kwenye mfumo. Wale wasambazaji wote wamesajiliwa na wamepewa namba na wale watumiaji wamesajiliwa. Kwa hiyo, kuna token ambayo inamwendea mtumiaji kila mwezi ambayo hii token ni punguzo la Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maana yake ni nini? Kwenye mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanakwenda kwenye energy safi, wametengeneza token ambayo Serikali ime-subsidize. Kwa hiyo, mtungi huo hauwi tena na gharama kubwa, unakuwa na gharama ndogo kwa sababu huyu mwananchi unapoisha akipeleka ile token huyu muuzaji wa gesi moja kwa moja anaweza kumpa gesi kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, sasa hili limewezesha asilimia tatu peke yake ya population ya watu wa India ambao ndio bado wanachanganya aina mbalimbali za nishati, lakini the rest wote wanatumia gesi safi kwa ajili ya matumizi ya majumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili la usambazaji likisimamiwa vizuri, kama tunalenga kuhakikisha kwamba tunapunguza matumizi ya kuni, mkaa na uharibifu wa mazingira, ni lazima Serikali ifahamu kwamba inatakiwa kutengeneza mpango wa kudumu kama ulivyo mpango wa TASAF na REA ambao utafanya wananchi waliopo kijijini waipate hii nishati kwa ukaribu na kwa gharama nafuu. Wakati huo huo wasambazaji wahakikishe kwamba wana soko lao la uhakika. Hapo ndipo jambo litaweza kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tulipofanya ziara Dar es Salaam, tukatembelea vituo vingi ambavyo vinauza compressed natural gas. Kwanza naipongeza Serikali na Wizara kwa hatua hiyo ambayo imefikiwa. Hata hivyo, jambo tulilojifunza ni kwamba, vituo ni vichache, hamasa ni kubwa. Kwa hiyo, matokeo yake ni nini? Matokeo yake ni kwamba foleni ya kusubiri kuwekewa gesi ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tulikwenda kwenye kituo kimoja tukakuta gari ya shule inasubiri kuwekewa gesi. Sisi tumefika pale takribani saa saba tukakuta gari lile limefika pale saa 12.00 linasubiri kuwekewa gesi na foleni bado ni ndefu. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba eneo hili tunatakiwa tuongeze juhudi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunajielekeza katika kuhakikisha kwamba Serikali inakuwa mfano, ushauri wangu ni kwamba pengine tulegeze masharti ya uwekezaji kwenye eneo hili ili tuhamasishe zaidi wawekezaji binafsi waje waungane na hawa waliopo, kama tulivyokwenda kwenye viwanda mbalimbali na tukakuta vinatumia natural gas na viwanda hivi vinasema vinaokoa gharama kubwa sana ya umeme.

Mheshimiwa Spika, jambo hili lifanyike kwa speed kubwa ili kuwafanya wananchi ambao wangetamani kutumia gesi kwenye gari zao, kwa sababu kwa kweli kwa foleni ya Dar es Salaam, mtu anayefanya biashara ya taxi au UBA, au usafirishaji kama anatumia diesel au petrol huyu ni lazima anakula hasara, lakini wale wanaotumia gesi, hata ukizungumza nao kwenye foleni, yeye amewasha AC, anapiga mziki na hana wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maoni yangu ni kwamba, naomba Wizara kufanya mkakati huu kuwa mkakati kabambe ili kuokoa mazingira na kuongeza matumizi ya gesi. Nakushukuru sana.