Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia afya sote ya kuendelea kuwepo Bungeni tukihudumu.

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu, na kwa kweli matunda yake tunaendelea kuyaona.

Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa dhati Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika nchi yetu hasa ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na nishati ya kutosha. Vilevile namshukuru Naibu Waziri, Mheshimiwa Judith Kapinga ambaye naye anasaidia kazi na wanaendelea vizuri. Pia, naishukuru timu nzima ya Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Spika, ukitaka kuona nchi yoyote ambayo inaendelea kwa kasi, moja ya factor ambazo utaziona pale ni uhakika wa umeme katika nchi hiyo. Nadhani hilo ndilo jambo ambalo nasi tunatakiwa kujikita sana. Nchi yetu inahitaji kuwa na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonesha nia ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba tatizo la umeme katika nchi yetu linatatulika. Ukitaka kujua hilo, utaona jinsi ambavyo miradi mingi ya kuzalisha umeme inaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano hapa umetolewa wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambalo linatarajia kutoa Megawatt 2115. Vilevile kuna ile Kinyerezi I ambayo tunategemea itumie natural gas ambayo itatoa Megawatt 185, lakini ule Mto Kagera kule Rusumo tunategemea kutoa Megawatt 85 na miradi mingine ambayo inaendelea mahali pale.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho ningechukua fursa kuwashauri Wizara ya Nishati ni kuendelea kutafuta vyanzo vipya. Vyanzo vilivyopo bado havitoshi. Sisi kama nchi, tunatarajia tuwe na umeme wa kutosha, lakini pia tupate fursa ya kuuza katika nchi Jirani. Kwa namna hiyo tutahakikisha uchumi wetu utakuwa unaenda mbele.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini ambao unatekelezwa na REA. Mradi huu umekuwa mzuri sana, na kwa kweli ukienda vijijini, leo vile vijiji ambavyo tayari vina umeme, hata kama katika lile eneo dogo lakini vijana tayari wamejiajiri. Vijana wamejiajiri wanafanya biashara, wameanzisha viwanda vidogo vidogo na kwa kufanya hivyo wamekuza pato la familia zao na Pato la Taifa kwa ujumla. Kwa hiyo, jambo hili ni la muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, shida kubwa iliyoko sasa kwenye REA ni kasi ndogo ya kutekeleza mradi huu. Wamesema wengine kwamba ukienda kwenye kijiji utakuta kuna nguzo 20, 25. Kwa hiyo ni watu wachache ambao wamefikiwa na umeme huu, lakini asilimia kubwa ya wananchi wa vijijini kwenye kijiji husika utakuta hawana umeme. Kwa hiyo, hilo limekuwa tatizo na kumekuwa na kelele nyingi.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa upande wa vitongoji nilikuwa nafikiri tusianze kwenda kwenye vitongoji kwanza, tumalizie zile nyumba za kwenye kijiji. Zile nyumba zinazotakiwa kupata umeme katika Kijiji, zipate umeme ndipo twende kwenye vitongoji vyake. Hiyo itatusaidia sana kuliko kuruka kwenda kwenye kitongoji, wakati huku kwenye vijiji kuna watu kumi tu ndio wenye umeme.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni muhimu kwa sababu umeme ukipatikana kwa maeneo yote, hata kelele za kuilaumu Serikali zitapungua sana. Kwa hiyo, nilikuwa nawashauri watu wa REA waongeze kasi ya utekelezaji wa mradi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, pia nichukue fursa hii kuwashukuru Wizara ya Nishati katika Jimbo langu la Mpwapwa ambapo bado vijiji vitatu na mkandarasi yuko site. Vijiji vyote vimepata umeme isipokuwa shida ni ile kasi ya vile vijiji vitatu, mkandarasi haendi kwa kasi inayotakiwa. Hata hivyo ninaamini Wizara itaweka msukumo ili hivyo vijiji vitatu vilivyobaki viweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni huduma za TANESCO. Miaka ya nyuma kulikuwa na huduma ambazo hazikuwa nzuri na hivyo zilisababisha wananchi kuilaumu sana Serikali, lakini nawapongeza kwamba leo wamekuja na solution. Sasa wanatumia mifumo kwa ajili ya mawasiliano, na kuna call centers. Mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma nilipata fursa ya kutembelea hii miradi ninayoisema ya kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Spika, pia tumetembelea Makao Makuu ya TANESCO na tumeona mifumo ambayo imewekwa, kuna call centers na mawasiliano yako vizuri na wateja. Zamani ilikuwa tukipata shida ya umeme tunaweza kusafiri kutoka nyumbani mpaka kwenye Ofisi ya TANESCO ndipo upate huduma. Leo unapiga simu mara moja na tatizo linatatulika ukiwa nyumbani kwako.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa hili nawapongeza, ni hatua kubwa, lakini bado tunataka kuendelea kuboresha huduma kwa wateja, hii itatusaidia sana. Kwanza shirika lenyewe litapata fedha kwa wingi kwa sababu litatoa huduma kwa haraka na watakusanya mapato kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni uchakavu wa miundombinu. Kule Mpwapwa tumekuwa na shida ya kukatikakatika umeme, nadhani ni maeneo mengi katika nchi hii. Umeme unakatikakatika sana katika Wilaya yetu ya Mpwapwa kwa sababu ile miundombinu inayosafirisha umeme kutoka kwenye kituo chetu cha zuzu imechakaa na kwa hiyo, unakuta kila siku umeme unakatika bila taarifa na mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, napenda sana Wizara ya Nishati iangalie jambo hili sana, tunahitaji umeme wa uhakika. Ili uweze kufanya shughuli zako za kiuchumi lazima umeme uwe wa uhakika, uwe na uhakika kwamba leo unataka kufanya kazi masaa 12, basi ufanye kazi masaa 12, lakini unapanga masaa 12 umeme unakatika, unafanya kazi masaa mawili. Kwa kufanya hivyo, hatuwezi kukua kiuchumi, tutaendelea kudidimia, tutakuwa maskini.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji umeme kuliko kitu kingine chochote. Kwa hiyo, tatizo la kukatikakatika umeme bila sababu za msingi, naomba Wizara ishughulike nalo sana, kwa sababu vinginevyo hatuwezi kusonga mbele.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja, nashukuru sana.