Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu. Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, na pia nampongeza Naibu Waziri Judith Kapinga kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya Katika Wizara hii. Kwa moyo wangu wa dhati nampongeza Spika wangu, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kazi kubwa anayoifanya na jinsi anavyoliongoza Bunge letu kwa weledi. Mwenyezi Mungu akujalie Spika wetu.

Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hotuba aliyotoa Waziri wa Nishati na mipango yao. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu, mipango yenu iende ikakamilike ili Watanzania waweze kufurahia huduma hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kuhakikisha wanaleta mtandao wa umeme katika vijiji vyetu. Hata hivyo, kwa upande wa Jimbo langu la Mtwara Vijijini, jumla ya vijiji ambavyo vilitakiwa kuwashwa umeme ni vijiji 24; ambavyo vimewashwa ni vijiji 18 na ambavyo bado havijawashwa ni vijiji sita. Ni hatua kubwa sana. Nawashukuru na ninampongeza Naibu Waziri Mkuu, naipongeza Serikali, na pia nawapongeza wakandarasi ambao wanafanya kazi katika jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Mkandarasi, mpaka kufikia Mei, 25 vijiji vyote vitakuwa vimekamilika katika Jimbo la Mtwara Vijijini. Ninasisitiza na ninawaombea vijiji hivyo vilivyobaki viende vikakamilike ili wananchi wangu waweze kufurahia huduma hii muhimu ya umeme.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi katika vijiji umeme umewashwa. Hata hivyo, changamoto iliyopo ni zile kilometa mbili za kuingia ndani bado hazijawafikia wananchi. Katika vitongoji bado umeme haujasambaa vizuri. Kwa hiyo, naomba zile sentimeta mbili zifuatiliwe vizuri ili umeme uweze kusambaa vizuri katika vitongoji ambavyo bado havijawaka umeme.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la umeme katika Kijiji cha Msimbati na Madimba. Katika Bunge la Bajeti lililopita nilizungumzia sehemu ambayo inatoka gesi asilia ya Msimbati na Madimba, umeme unawaka maeneo ya Barazani tu lakini maeneo mengi ya vijiji na vitongoji vyake, maeneo mengi niliorodhesha mpaka vijiji, hakuna umeme, haujafika, sehemu ambayo inatoka gesi, ninasikitika sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali mliangalie suala hili kwa upana wake. Niwaombe Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Mheshimiwa Naibu Waziri wake mwende mkaliangalie suala hili katika Kijiji cha Msimbati na Kijiji cha Madimba, bado tuna changamoto ya umeme. Sehemu ambayo gesi ipo, sehemu ambayo gesi inachakatwa umeme hakuna. Naomba mliangalie suala hili kwa upana wake katika Kijiji cha Msimbati na Madimba.

Mheshimiwa Spika, katika Kijiji cha Msimbati na Madimba ndiko inakotoka gesi asilia. Hata hivyo kwa masikitiko makubwa sehemu ambayo kuna mradi mkubwa ambao Serikali imewekeza bado wananchi wale hawanufaiki na rasilimali hizi ambazo zipo katika vijiji vyao.

Mheshimwia Spika, wananchi wa Kijiji cha Msimbati na Madimba bado wana changamoto kubwa sana. Ukiangalia yale maeneo ambayo yamezunguka mradi mkubwa wa gesi asilia bado kuna changamoto kubwa mno. Hii CSR bado ni ndogo na hainufaishi vijiji hivi vya Msimbati na Madimba. Naomba hawa watu wa TPDC waliangalie hili. Hii CSR inayotoka pale ni ndogo…

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Shamsia, kuna taarifa kutoka kwa jirani yako hapo Mheshimiwa Stella Fiyao.

TAARIFA

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba, issue ya CSR imekuwa ni changamoto kubwa kwenye maeneo mengi yanayozungukwa na miradi mikubwa. Nashukuru sana.

SPIKA: Miradi mikubwa ya umeme au miradi yote?

MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, ni miradi yote ikiwemo ya umeme. Hata kwenye Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere bado kuna changamoto kubwa sana ya CSR.

SPIKA: Mheshimiwa umeulizwa swali na umeshalijibu. Mheshimiwa Shamsia, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaipokea taarifa hii kwa umuhimu wake mkubwa. Inaumiza, kwa sababu wananchi hawa wa Msimbati na Madimba wametupwa. Wana miradi mikubwa ambayo imewazunguka katika kijiji chao lakini hawanufaiki na chochote.

Mheshimiwa Spika, kwa moyo wangu wa dhati namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, nilikwenda ofisini kwake nikamlilia shida iliyopo katika vijiji hivi viwili vya Msimbati na Madimba. Nashukuru Mwenyezi Mungu Mheshimiwa Dkt. Doto alikuja. Mheshimiwa Dkt. Doto, Mwenyezi Mungu akujalie na akuweke uishi maisha marefu na afya nzuri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Doto alikuja kwenye Jimbo langu la Mtwara Vijijini akajionea hali halisi iliyokuwepo kwenye jimbo langu. Yeye ndiye mtu wa kwanza aliyekwenda kuweka alama kwenye vijiji hivi. Baada ya kuzungumza ndipo tukaiona hiyo CSR inatoka na kwa mara ya kwanza sasa kituo cha afya kinajengwa ilhali mradi huu katika Jimbo la Mtwara Vijijini upo kwa muda mrefu, lakini hakuna chochote ambacho kinanufaisha vijiji hivi viwili vya Msimbati na Madimba. Ni hatari sana.

Mheshimiwa Spika, wale wananchi wako katika mazingira duni na wanaona Serikali imewekeza mradi mkubwa pale. Tunaona kwa wenzetu wanakochimba madini wananufaika na miradi yao, lakini sisi kule hakuna kinachoendelea. Inatia uchungu na inatia hasira. Sasa hivi Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko amekuja kule kuweka alama ndipo kituo cha afya kimeanza kujengwa. Mheshimiwa Dkt. Doto Mwenyezi Mungu akujalie sana.

Mheshimiwa Spika, katika Vijiji hivi vya Madimba na Msimbati wanakuja wanasema wanataka watuwekee taa za barabarani. Hiyo barabara ya kutuwekea taa za barabarani iko wapi? Sehemu ambayo inatoka gesi asilia barabara ni mbovu na hazipitiki. Ukienda hali yake inatia uchungu. Siku moja uje utembelee jimbo langu ujionee hali halisi iliyopo huko inakotoka gesi. Hali ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, yaani ukiangalia maisha ya wananchi walioko kule ni duni. Sasa hivi ndiyo Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko amekuja kutuwekea kituo cha afya. Baada ya kuja yeye, sijui hiyo CSR ilikuwa inakwenda wapi? Pia hiyo CSR inayotoka ni ndogo. Watu wa TPDC mliangalie hili…

MHE HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Shamsia Mtamba, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mtenga.

TAARIFA

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, eneo linalozungumzwa kutoka Mtwara Mjini mpaka unaelekea Msimbati lina kilometa 35. Pia tunapozungumza mradi wa gesi wa mabilioni ya shilingi, hasa tunazingatia miundombinu ya barabara. Leo likitokea tatizo lolote mfano moto, gari la fire haliwezi kufika Msimbati kwa wakati na mradi ule tunaweza tukaupoteza, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Shamsia Mtamba, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. Hiyo ndiyo hali halisi iliyopo katika Kijiji cha Madimba na Msimbati, kumetupwa kabisa. Serikali imewekeza miradi mikubwa kule (billions of monies) lakini hakuna kinachoendelea. Inasikitisha sana.
Mheshimiwa Spika, nije kuzungumzia suala la Mtambo wa Turbine na hapa nimshukuru Naibu Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa kweli amekuwa mkombozi wa watu wa kusini sasa acha nimshukuru, nimpe maua yake tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Mtwara tuna changamoto kubwa sana ya umeme changamoto ambayo imetusumbua kwa muda mrefu lakini Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu tulikaa naye kikao tukamweleza changamoto iliyopo katika Mkoa wetu changamoto kubwa ya umeme, kwa usikivu wake Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko akasema Wabunge wa Mtwara nimewasikia kilio chenu nitawaleteeni mtambo kwa ajili ya kupunguza tatizo la umeme katika Mkoa wa Mtwara na Lindi. (Makofi)

SPIKA: Sekunde 30 malizia kengele ya pili imeshagonga.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante katika Mkoa wa Mtwara na Lindi tunashukuru mtambo ule umefika katika Mkoa wetu wa Mtwara na umeanza kufanya kazi ili kuhakikisha wanamaliza tatizo la umeme katika Mkoa wa Mtwara na Lindi kwa hili tunakushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu lakini ninachokuomba na ninachoshauri endelea kufuatilia mtambo ili huduma ya umeme katika Mkoa wa Mtwara na Lindi uweze kukaa sawasawa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)