Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nami nikushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia kuwepo hapa tukiwa na afya njema. Nimpongeze Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko na Waziri wa Nishati. Nimpongeze Katibu Mkuu, Ndugu Mramba; Naibu Katibu Mkuu, Bwana Matarajio; na Watendaji wengine wa REA na TPDC, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza hii Wizara imepata wazoefu Katibu Mkuu Mramba alianzia kuwa Meneja wa TANESCO mpaka sasa hivi amekuwa ni Katibu Mkuu. Vilevile Bwana Matarajio alikuwa TPDC na sasa hivi anaonyesha atatupa matarajio makubwa sana kwa uzoefu alioupata katika TPDC ili kutaka kutuletea maendeleo ya umeme Tanzania pamoja na gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kampeni yake kubwa ya kumtua mwanamke kuni, kwa kweli wanawake kwa niaba yao nasema Mwenyezi Mungu ambariki sana. Wanawake kwa muda mrefu wanahangaika kutafuta kuni maporini, lakini je utakapoendelea kukata kuni mwisho wake ni nini? Ni uharibifu wa mazingira na tutaifanya nchi iingie katika ukame, hivyo Mwenyezi Mungu azidi kumzidisha kumpa maisha marefu na afya njema, tushirikiane naye ili tuhakikishe hii kampeni ya kumtua mwanamke kuni inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa tuliyokuwa nayo zaidi ya 95% Tanzania iko katika umeme na haya ni maendeleo. Kuwa na umeme ni maendeleo kwa vile mahitaji ya dunia ya sasa hivi ni teknolojia ambayo inakwenda na umeme. Ukitaka maji huwezi kuanza kufua maji bila umeme, huwezi kuendesha petrol station bila umeme, huwezi kuendesha shule bila umeme, huwezi kuendesha hata Bunge bila umeme. Hivyo kwa 95% hata nchi za jirani wanaona kama kwa kweli Tanzania tumefanya kazi kubwa sana ya kupeleka umeme mpaka vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ukienda Liwale Vijijini huko Mpigamiti wote unakuta kuna umeme, kwa kweli haya ni mabadiliko makubwa na maendeleo makubwa ambayo tunayatarajia. Hata hivyo, kuna changamoto, tumepeleka umeme mwingi vijijini huo wa REA na wa kawaida, changamoto ya kwanza miundombinu mibovu, hasa waya za umeme nyingi zimeshaoza, zimeshakuwa hazifai, tuna imani kuwa katika mabadiliko haya yanayokwenda speed, kinachotakiwa ni kuhakikisha kwamba mfumo wowote ule ambao umewekwa ufanye kazi na uwe wa kisasa hii itaondoa changamoto ya kuzimika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiyo maana yake nini? Tumeleta mitambo ya kisasa, waya mbovu, hivyo zinakuwa overloaded, ndio maana inalipukalipuka na kusababisha giza. La pili, baadhi ya matumizi ya kutumia hasa hii miti, miti mingi na mvua kama hivi inaoza na kuna mchwa, hivyo inahitajika sasa hivi tubadilishe kutoka matumizi ya miti kwenda katika zege. Niwapongeze sana kwa vile wameliweka katika mojawapo ya hoja itakayoenda nayo twende kwa speed ili tuweze kubadilisha ili angalau tusizidi kuingia gharama ambazo zingeweza kurekebishika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la miradi ambayo wanaizungumzia sana wenzetu. Tunalalamika na ni kweli hii nchi ina keki na hii keki lazima iliwe na watu wote. Tuna miradi mikubwa ambayo unaona ya gesi ambayo inatoka katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani; Mradi wa Songas Kilwa, Mradi wa Madimba na miradi mingine ambayo imewekwa Mkuranga.

Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha katika mgao wa corporate social responsibility hata Mtwara haikuwekwa kabisa, utashangaa miradi ya Tanga – Hoima lakini wamepewa wao tu, Mikoa ya Lindi na Mtwara haimo, maana yake nini? Hii inatufanya Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ionekane ni mikoa maskini wakati kuna uwezo mkubwa kuivusha hii mikoa ikawa mikoa ya kitajiri. Tumeambiwa hii gesi ya LNG itatoka Lindi Mungu akijalia, lakini je, Lindi inafaidika nini? Kilwa inafaidika nini? Hakuna miradi yoyote, nitaongelea maeneo machache, mradi umepelekwa Tanga, mradi umepelekwa Dodoma, miradi mingine sitaki kuizungumzia, lakini Mtwara haimo katika mradi.

Mheshimiwa Spika, sasa tunajiuliza, ndio unakuta watu wa Mtwara wanataka wanufaike na ule mradi hata wa kuwajengea mahospitali, kuwainua vijana kiuchumi, lakini miradi ile haikupelekwa kule imepelekwa maeneo mengine ambayo kila siku wananufaika. Kuna muda niliwahi kuuliza Miradi ya TANAPA ilikuwa haiendi Lindi na Mtwara wanasema ninyi hamko katika ujirani mwema, sasa kwa nini miradi ya kule inapelekwa maeneo mengine?
Mheshimiwa Spika, ukiangalia miradi katika maeneo ya uchimbaji wa madini, haipelekwi Lindi na Mtwara wakasema zamani, kwa vile Lindi na Mtwara hamkuwa katika hiyo sekta. Sasa tunaomba tafadhali kama ni keki hawa wanaopanga mipango wasilete ubaguzi, itatufanya tuone kama kuna mikoa ya kunufaika zaidi na kuna mikoa inaachwa nyuma na inaonekana kama mikoa ya kimaskini. Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani mpaka Morogoro siyo mikoa maskini, tunahitaji sasa hivi wakakae tena, warekebishe hii hali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii miradi ya corporate social responsibility ikatengenezwe tena upya na wafanye tathmini yake, matokeo yake hii itatugawa kwa kuonekana kwamba imepelekwa mingi katika maeneo ambayo hawana masuala haya ya gesi asilia.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia mabadiliko ya tabianchi na athari itakayoifanya Wizara ya Nishati na Madini kuingia katika athari kubwa sana. Tunataka Wizara nne zishirikiane, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Madini na Wizara ya Mazingira. Mimi ni mwana mazingira na napenda sana kufuatilia mabadiliko ya tabianchi kwa ukamilifu na Mheshimiwa Rais kama mdau namba moja katika mabadiliko ya tabianchi na hii nitaizungumzia kwa mapana. Bunge linaendeshwa kwa Mabaraza yake, Madiwani wanaendeshwa kwa Mabaraza yao, lakini vilevile Rais anakwenda kwa Mabaraza yake na Spika katika Mikutano yake ya IPU anakwenda kwa Mabaraza yao, nini maana yake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anapokwenda katika mikutano ya mabadiliko ya tabianchi anakwenda na delegation haendi kama anakawenda kuzurura, anakwenda kule kufuata sheria inasema nini na masuala ya mikataba mbalimbali ya kimataifa. Kama Rais anakwenda kuhudhuria lakini bado kuna wataalam wanakwenda, lakini hatuna ripoti za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaweza zikatusaidia.

Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Mhongo kuwa tunataka vyanzo hivi viendelee, lakini kama vyanzo hivi havisimamiwi nchi itaingia katika disaster kubwa sana. Kwa mfano, nataka nizungumzie kuna suala la adaptation ya mabadiliko ya tabianchi inasema una-adapt mito kwenda katika Bahari, adaptation of the rivers to the sea, je, tumeisimamia hiyo adaptation? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo unaiona Rufiji imeingia katika gharika ya maji (floods) kwa nini imeingia katika gharika? Imechafuliwa mito huko juu wafugaji wamechukua mito wakulima wame bypass mito imeingia katika mashamba yao matokeo yake maji yakawa blocked. Baada ya kuwa yame-block maeneo ya Rufiji hasa katika Daraja la Mkapa maji yanasambazwa kwa wanavijiji ambao wanaathirika na wanakuwa maskini kwa ajili gani? Hatukusimamia kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukajifunze wenzetu India walikuwa katika mabadiliko, hawakusimamia mabadiliko ya tabianchi, ilikuwa kila siku unasikia milima mito ya Ganges na mito mbalimbali, watu wanakufa kwa sababu gani? Hatukusimamia. Siyo hivyo tu tunaipeleka hii hali siyo katika Wizara hii peke yake, leo Wizara ya Ujenzi ikishirikiana na Wizara itajua madaraja yao yote yanafanya kazi na je, yale madaraja hayana mchanga. Nilizungumza Bunge lililopita, nimepita Rufiji tuta limejaa, ina maana maji yakitoka huko hayawezi kupita pale, hivyo yatahama yatakwenda Muhoro, yatakwenda Kibiti, hivyo wale wenzetu watakuwa katika mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii siyo kwa ajili ya Mto Rufiji peke yake, nenda Dar es Salaam, pale Magomeni watu wameuharibu ule mto. Baada ya kuuharibu ule mto maji yanaingia katika Mradi wa Mwendokasi, nchi imeingia katika gharika, mwendokasi haifanyi kazi tena, majengo yameshakufa pale, tunatafuta tena mindombinu mingine ya kuirekebisha, lakini je, wanaokwenda kwenye mikutano hii ya mabadiliko ya tabianchi wanatuletea ripoti? Mheshimiwa Rais anakwenda katika mabadiliko ya tabia nchi na mikutano yake, hatuna ripoti tunayopata ndani ya Bunge. Matokeo yake, tunajikuta maazimio na ajenda mbalimbali ambazo zinapitishwa katika Umoja wa Mataifa haziji chini na kama haziji kwetu sisi tumekaa hatujui kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoomba, wewe ni kiongozi mzuri na unakwenda unaona unayoyaona, tunataka ajenda zote zinazopitishwa na maazimio yapitishwe kwa wakati, siyo leo. Ajenda ya mwaka 2012 ndio inakuja kupitishwa hapa, ina maana tumepitwa na wakati, hii ni Tanzania siyo kisiwa, tunahitaji maendeleo ambayo yataendana na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo wakae na Wizara ya Nishati wahakikishe wanaolima kuanzia Morogoro kule kote, kilimo chao hakileti uharibifu wa mazingira. Wafugaji waliokimbilia kwenye mito wanakata miti na wanafanya vitu mbalimbali, vilevile waangaliwe je, haitaleta mazingira mabaya ili kufanya Wizara hii ya Nishati na Madini ambayo tunategemea Mradi mkubwa wa Mwalimu Nyerere na mradi ule ambao hautaathirika na mabadiliko ya tabianchi waufanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, nina imani sana na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, kwa hili ninalolizungumzia tulifanyie kazi ili angalau pale mito yote ambayo inataka kumwaga maji baharini, narudia tena mito yote ambayo inataka kumwaga maji baharini inazibuliwa na hii itatusaidia baadhi ya Wizara nyingine zisiathirike na haya. Tunaiona leo Magomeni tunakuja Mbezi, Mto Mbezi ule umezibwa nyumba zote za NSSF zimeingia katika maji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, malizia Mheshimiwa.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na ninachoomba tu kuwa ushirikiano wa Wizara wa mabadiliko ya tabianchi ni mzuri na utasaidia kutunza vyanzo ambavyo vitalisaidia Bwawa la Mwalimu Nyerere hata Bwawa la Mtera lisipoteze asili yake na liweze kufanya kazi na kuleta uchumi wa kinchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nasema ahsante na Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)